Safari Ya Kwanza Ya Paulo Kueneza Injili
13
(13:1–14:28)
Barnaba Na Sauli Wanatumwa
1 Katika kanisa huko Antiokia ya Shamu walikuwako manabii na walimu, yaani: Barnaba, Simeoni aitwaye Nigeri, Lukio Mkirene, Manaeni aliyekuwa amelelewa pamoja na Mfalme Herode Agripa, na Sauli. 2 Walipokuwa wakimwabudu Bwana na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, “Nitengeeni Sauli na Barnaba kwa kazi ile maalum niliyowaitia.” 3 Ndipo baada ya kufunga na kuomba, wakawawekea mikono yao na wakawatuma waende zao.
Barnaba Na Sauli Waenda Kipro
4 Hivyo, wakiwa wametumwa na Roho Mtakatifu, wakashuka kwenda Seleukia na kutoka huko wakasafiri baharini mpaka kisiwa cha Kipro. 5 Walipowasili katika mji wa Salami, wakahubiri neno la Mungu katika sinagogi la Wayahudi. Pia walikuwa na Yohana Marko kuwa msaidizi wao.
6 Walipokwisha kupita katika nchi zote hizo wakafika Pafo, ambapo walikutana na Myahudi mmoja mchawi aliyekuwa nabii wa uongo, jina lake Bar-Yesu. 7 Mtu huyu alikuwa pamoja na Sergio Paulo, mtu mwenye hekima aliyekuwa msaidizi wa mwakilishi wa mtawala wa kile kisiwa. Sergio Paulo akawaita Sauli na Barnaba akitaka kusikia neno la Mungu. 8 Lakini Elima yule mchawi (hii ndiyo maana ya jina lake), aliwapinga Barnaba na Sauli na kujaribu kumpotosha yule mkuu wa kile kisiwa aiache imani. 9 Ndipo Sauli, ambaye pia aliitwa Paulo, akiwa amejawa na Roho Mtakatifu, akamkazia macho Elima huyo mchawi, 10 akamwambia, “Ewe mwana wa ibilisi, wewe ni adui wa kila kilicho haki! Umejaa kila aina ya udanganyifu na ulaghai. Je, hutaacha kuzipotosha njia za Bwana zilizonyooka? 11 Nawe sasa sikiliza, mkono wa Bwana u dhidi yako. Utakuwa kipofu, wala hutaona jua kwa muda.”
Mara ukungu na giza vikamfunika, naye akaenda huku na huko akitafuta mtu wa kumshika mkono ili amwonyeshe njia. 12 Yule mkuu wa kile kisiwa alipoona yaliyotukia, akaamini kwa sababu alistaajabishwa na mafundisho kuhusu Bwana.
Paulo Na Barnaba Huko Antiokia Ya Pisidia
13 Kisha Paulo na wenzake wakasafiri toka Pafo wakafika Perga huko Pamfilia. Lakini, Yohana Marko akawaacha huko, akarejea Yerusalemu. 14 Kutoka Perga wakaendelea hadi Antiokia ya Pisidia. Siku ya Sabato wakaingia ndani ya sinagogi, wakaketi. 15 Baada ya Sheria ya Mose na Kitabu cha Manabii kusomwa, viongozi wa sinagogi wakawatumia ujumbe wakisema, “Ndugu, kama mna neno la kuwafariji watu hawa, tafadhali lisemeni.”
16 Paulo akasimama, akawapungia mkono na kusema: “Enyi wanaume wa Israeli na ninyi nyote mnaomcha Mungu. 17 Mungu wa watu hawa wa Israeli aliwachagua baba zetu, akawafanya kustawi walipokuwa huko Misri, kwa uwezo mwingi akawaongoza na kuwatoa katika nchi ile. 18 Kwa muda wa miaka arobaini alivumilia matendo yao walipokuwa jangwani. 19 Naye baada ya kuyaangamiza mataifa saba waliokuwa wakiishi katika nchi ya Kanaani, akawapa Waisraeli nchi yao iwe urithi wao. 20 Haya yote yalichukua kama muda wa miaka 450.
“Baada ya haya, Mungu akawapa waamuzi mpaka wakati wa nabii Samweli. 21 Ndipo watu wakaomba wapewe mfalme, naye Mungu akawapa Sauli mwana wa Kishi wa kabila la Benyamini, aliyetawala kwa miaka arobaini. 22 Baada ya kumwondoa Sauli katika ufalme, akawainulia Daudi kuwa mfalme wao. Mungu pia alimshuhudia, akisema, ‘Nimemwona Daudi mwana wa Yese, mtu anayeupendeza moyo wangu, atakayetimiza mapenzi yangu yote.’
23 “Kutoka uzao wa mtu huyu, Mungu amewaletea Israeli Mwokozi Yesu, kama alivyoahidi. 24 Kabla ya kuja kwa Yesu, Yohana alihubiri toba na ubatizo kwa watu wote wa Israeli. 25 Yohana alipokuwa anakamilisha kazi yake, alisema: ‘Ninyi mnadhani mimi ni nani? Mimi si yeye. La hasha, lakini yeye yuaja baada yangu, ambaye mimi sistahili kufungua kamba za viatu vya miguu yake.’
26 “Ndugu zangu, wana wa Abrahamu, nanyi watu wa Mataifa mnaomcha Mungu, ujumbe huu wa wokovu umeletwa kwetu. 27 Kwa sababu wakaao Yerusalemu na viongozi wao hawakumtambua wala kuelewa maneno ya manabii yasomwayo kila Sabato, bali waliyatimiza maneno hayo kwa kumhukumu yeye. 28 Ijapokuwa hawakupata sababu yoyote ya kumhukumu kifo, walimwomba Pilato aamuru auawe. 29 Walipokwisha kufanya yale yote yaliyoandikwa kumhusu, walimshusha kutoka msalabani na kumzika kaburini. 30 Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu. 31 Naye kwa siku nyingi akawatokea wale waliokuwa pamoja naye kuanzia Galilaya hadi Yerusalemu. Nao sasa wamekuwa mashahidi wake kwa watu wetu.
32 “Nasi tunawaletea habari njema, kwamba yale Mungu aliyowaahidi baba zetu 33 sasa ameyatimiza kwetu sisi watoto wao, kwa kumfufua Yesu, kama ilivyoandikwa katika Zaburi ya pili:
“ ‘Wewe ni Mwanangu;
leo mimi nimekuzaa.’
34 Kwa kuwa Mungu alimfufua kutoka kwa wafu asioze kamwe, alitamka maneno haya:
“ ‘Nitakupa wewe baraka takatifu zilizo za hakika
nilizomwahidi Daudi.’
35 Kama ilivyosemwa mahali pengine katika Zaburi,
“ ‘Hutamwacha Aliye Mtakatifu wako kuona uharibifu.’
36 “Kwa maana Daudi akiisha kulitumikia kusudi la Mungu katika kizazi chake, alilala; akazikwa pamoja na baba zake na mwili wake ukaoza. 37 Lakini yule ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu hakuona uharibifu.
38 “Kwa hiyo ndugu zangu, nataka ninyi mjue kwamba kwa kupitia huyu Yesu msamaha wa dhambi unatangazwa kwenu. 39 Kwa kupitia yeye, kila mtu amwaminiye anahesabiwa haki kwa kila kitu ambacho asingeweza kuhesabiwa haki kwa sheria ya Mose. 40 Kwa hiyo jihadharini ili yale waliyosema manabii yasiwapate:
41 “ ‘Angalieni, enyi wenye dhihaka,
mkastaajabu, mkaangamie,
kwa maana nitatenda jambo wakati wenu
ambalo hamtasadiki,
hata kama mtu akiwaambia.’ ”
42 Paulo na Barnaba walipokuwa wakitoka nje ya sinagogi, watu wakawaomba wazungumze tena mambo hayo Sabato iliyofuata. 43 Baada ya kusanyiko la Sinagogi kutawanyika, wengi wa Wayahudi na waongofu wa dini ya Kiyahudi wakawafuata Paulo na Barnaba, wakazungumza nao na kuwahimiza wadumu katika neema ya Mungu.
44 Sabato iliyofuata, karibu watu wote wa mji walikuja kusikiliza neno la Bwana. 45 Lakini Wayahudi walipoona ule umati mkubwa wa watu walijawa na wivu, wakayakanusha maneno Paulo aliyokuwa akisema.
46 Ndipo Paulo na Barnaba wakawajibu kwa ujasiri, wakisema, “Ilitupasa kunena nanyi neno la Mungu kwanza. Lakini kwa kuwa mmelikataa, mkajihukumu wenyewe kuwa hamstahili uzima wa milele, sasa tunawageukia watu wa Mataifa. 47 Kwa maana hili ndilo Bwana alilotuamuru:
“ ‘Nimewafanya ninyi kuwa nuru kwa watu wa Mataifa,
ili mpate kuuleta wokovu hadi miisho ya dunia.’ ”
48 Watu wa Mataifa waliposikia haya wakafurahi na kulitukuza neno la Bwana; nao wote waliokuwa wamekusudiwa uzima wa milele wakaamini.
49 Neno la Bwana likaenea katika eneo lile lote. 50 Lakini Wayahudi wakawachochea wanawake wenye kumcha Mungu, wenye vyeo pamoja na watu maarufu katika mji, wakachochea mateso dhidi ya Paulo na Barnaba na kuwafukuza kutoka eneo hilo. 51 Hivyo Paulo na Barnaba wakakungʼuta mavumbi ya miguu yao ili kuwapinga, nao wakaenda Ikonio. 52 Wanafunzi wakajawa na furaha na Roho Mtakatifu.