5
Maombolezo Na Wito Wa Toba
Sikia neno hili, ee nyumba ya Israeli, ombolezo hili ninalifanya kuwahusu ninyi:
“Bikira Israeli ameanguka,
kamwe hatainuka tena,
ameachwa pweke katika nchi yake,
hakuna yeyote wa kumwinua.”
Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo:
“Wakati mmoja wa miji yako utakapopeleka watu elfu moja vitani kwa ajili ya Israeli,
mia moja tu watarudi;
wakati mji utakapopeleka mia moja,
kumi tu ndio watarudi hai.”
Hili ndilo Bwana asemalo kwa nyumba ya Israeli:
“Nitafuteni mpate kuishi;
msitafute Betheli,
msiende Gilgali,
msisafiri kwenda Beer-Sheba.
Kwa maana kwa hakika Gilgali itakwenda uhamishoni,
na Betheli itafanywa kuwa si kitu.”*Yaani Aveni kwa Kiebrania, kumaanisha Beth-Aveni, jina lingine la Betheli kwa dhihaka.
Mtafuteni Bwana mpate kuishi,
au atafagia nyumba ya Yosefu kama moto;
utawateketeza, nayo Betheli
haitakuwa na yeyote wa kuuzima.
 
Ninyi ambao mnageuza haki kuwa uchungu
na kuiangusha haki chini
(yeye ambaye alifanya Kilimia na Orioni,
ambaye hugeuza giza kuwa mapambazuko
na mchana kuwa usiku,
ambaye huyaita maji ya bahari
na kuyamwaga juu ya uso wa nchi:
Bwana ndilo jina lake;
yeye hufanya maangamizo kwenye ngome
na kufanya mji uliozungushiwa ngome kuwa ukiwa),
10 mnamchukia yule akemeaye mahakamani,
na kumdharau yule ambaye husema kweli.
 
11 Mnamgandamiza maskini
na kumlazimisha awape nafaka.
Kwa hiyo, ingawa mmejenga majumba ya mawe ya fahari,
hamtaishi ndani yake;
ingawa mmepanda mashamba mazuri ya mizabibu,
hamtakunywa divai yake.
12 Kwa kuwa ninajua hesabu ya makosa yenu
na ukubwa wa dhambi zenu.
 
Mmewaonea wenye haki na kupokea rushwa
na kuzuia haki ya maskini mahakamani.
13 Kwa hiyo mtu mwenye busara hunyamaza kimya nyakati kama hizo,
kwa kuwa nyakati ni mbaya.
 
14 Tafuteni mema, wala si mabaya,
ili mpate kuishi.
Ndipo Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote atakuwa pamoja nanyi,
kama msemavyo yupo nanyi.
15 Yachukieni maovu, yapendeni mema;
dumisheni haki mahakamani.
Yamkini Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote
atawahurumia mabaki ya Yosefu.
16 Kwa hiyo hili ndilo Bwana, Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote, asemalo:
“Kutakuwepo maombolezo katika barabara zote
na vilio vya uchungu katika njia kuu zote.
Wakulima wataitwa kuja kulia,
na waombolezaji waje kuomboleza.
17 Kutakuwepo kuomboleza katika mashamba yote ya mizabibu,
kwa kuwa nitapita katikati yenu,”
asema Bwana.
Siku Ya Bwana
18 Ole wenu ninyi mnaoitamani
siku ya Bwana!
Kwa nini mnaitamani siku ya Bwana?
Siku hiyo itakuwa giza, si nuru.
19 Itakuwa kama vile mtu aliyemkimbia simba
kumbe akakutana na dubu,
kama vile mtu aliyeingia nyumbani mwake
na kuupumzisha mkono wake kwenye ukuta,
kumbe akaumwa na nyoka.
20 Je, siku ya Bwana haitakuwa giza, na si nuru:
giza nene, bila mwonzi wa mwanga?
 
21 “Ninachukia, ninazidharau sikukuu zenu za dini;
siwezi kuvumilia makusanyiko yenu.
22 Hata ingawa mnaniletea sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka za nafaka,
sitazikubali.
Ingawa mnaniletea sadaka nzuri za amani,
sitazitambua.
23 Niondoleeni kelele za nyimbo zenu!
Sitasikiliza sauti za vinubi vyenu.
24 Lakini acheni haki itiririke kama mto,
na uadilifu uwe kama kijito kisichokauka!
 
25 “Je, mliniletea dhabihu na sadaka
kwa miaka arobaini kule jangwani,
ee nyumba ya Israeli?
26 Mmeyainua madhabahu ya mfalme wenu,
Sikuthi mungu wenu mtawala,
na Kiuni mungu wenu wa nyota,
ambao mliwatengeneza wenyewe.
27 Kwa sababu hiyo nitawapeleka uhamishoni mbali kupita Dameski,”
asema Bwana, ambaye jina lake ni Mungu Mwenye Nguvu Zote.

*5:5 Yaani Aveni kwa Kiebrania, kumaanisha Beth-Aveni, jina lingine la Betheli kwa dhihaka.