8
Maono Ya Danieli Ya Kondoo Dume Na Beberu
Katika mwaka wa tatu wa utawala wa Mfalme Belshaza, mimi Danieli, nilipata maono, baada ya maono ambayo yalikuwa yamenitokea mbeleni. Katika maono yangu, nilijiona nikiwa ndani ya ngome ya Shushani katika jimbo la Elamu. Katika maono nilikuwa kando ya Mto Ulai.*Mto Ulai ni mfereji uliokuwa kati ya Shushani na Elymaisi; sasa unaitwa Mto Karuni. Nikatazama juu, na hapo mbele yangu kulikuwa na kondoo dume mwenye pembe mbili, akiwa amesimama kando ya mto, nazo pembe zake zilikuwa ndefu. Pembe moja ilikuwa ndefu kuliko hiyo nyingine, lakini iliendelea kukua baadaye. Nikamtazama yule kondoo dume alivyokuwa akishambulia kuelekea magharibi, kaskazini na kusini. Hakuna mnyama yeyote aliyeweza kusimama dhidi yake, wala hakuna aliyeweza kuokoa kutoka nguvu zake. Alifanya kama atakavyo, naye akawa mkuu.
Nilipokuwa ninatafakari hili, ghafula beberu mwenye pembe moja kubwa sana katikati ya macho yake alikuja kutoka magharibi, akiruka kasi juu ya dunia yote bila kugusa ardhi. Alikuja akimwelekea yule kondoo dume mwenye pembe mbili niliyemwona akisimama kando ya mto, akamshambulia kwa hasira nyingi. Nikamwona akimshambulia yule kondoo dume kwa hasira nyingi, akimpiga yule kondoo dume na kuvunja pembe zake mbili. Yule kondoo dume hakuwa na nguvu za kumzuia yule beberu, hivyo akamwangusha yule kondoo dume chini na kumkanyaga, wala hakuna aliyeweza kumwokoa yule kondoo dume kutoka nguvu za huyo beberu. Yule beberu akawa mkubwa sana, lakini katika kilele cha nguvu zake ile pembe yake ndefu ilivunjika, na mahali pake pakaota pembe nne kubwa kuelekea pande nne za dunia.
Kutoka mojawapo ya zile pembe nne palitokea pembe ndogo ukaongezeka nguvu kuelekea kusini, na kuelekea mashariki, na kuelekea Nchi ya Kupendeza. 10 Pembe hiyo ikaendelea kukua hadi kufikia jeshi la mbinguni, nayo ikalitupa baadhi ya jeshi la vitu vya angani hapa chini duniani, na kulikanyaga. 11 Pembe hiyo ikajikweza ili iwe kama Mkuu wa hilo jeshi; ikamwondolea dhabihu ya kila siku, napo mahali pake patakatifu pakashushwa chini. 12 Kwa sababu ya uasi, jeshi la watakatifu na dhabihu za kila siku vikatiwa mikononi mwake. Ikafanikiwa katika kila kitu ilichofanya, nayo kweli ikatupwa chini.
13 Kisha nikamsikia mtakatifu mmoja akizungumza na mtakatifu mwingine, akamwambia, “Je, itachukua muda gani maono haya yatimie: maono kuhusu dhabihu ya kila siku, uasi unaosababisha ukiwa, kutwaliwa kwa mahali patakatifu, na jeshi litakalokanyagwa chini ya nyayo?”
14 Akaniambia, “Itachukua siku 2,300. Ndipo mahali patakatifu patawekwa wakfu tena.”
Tafsiri Ya Maono
15 Mimi Danieli nilipokuwa ninaangalia maono na kujaribu kuelewa, mbele yangu alisimama mmoja aliyefanana na mwanadamu. 16 Kisha nikasikia sauti ya mwanadamu kutoka Mto Ulai ikiita, “Gabrieli, mwambie mtu huyu maana ya maono haya.”
17 Alipokuwa akikaribia pale nilipokuwa nimesimama, niliogopa, nikaanguka kifudifudi. Akaniambia, “Mwana wa mwanadamu, fahamu kuwa maono haya yanahusu siku za mwisho.”
18 Alipokuwa akinena nami, nilikuwa katika usingizi mzito, huku nimelala kifudifudi. Ndipo aliponigusa na kunisimamisha wima.
19 Akaniambia, “Nitakuambia yale yatakayotokea baadaye wakati wa ghadhabu, kwa sababu maono haya yanahusu wakati wa mwisho ulioamriwa. 20 Kondoo dume mwenye pembe mbili ambaye ulimwona anawakilisha wafalme wa Umedi na Uajemi. 21 Yule beberu mwenye nywele nyingi ni mfalme wa Uyunani, nayo ile pembe ndefu katikati ya macho yake ni mfalme wa kwanza. 22 Zile pembe nne zilizoota badala ya ile pembe iliyovunjika zinawakilisha falme nne ambazo zitatokea kutoka taifa lake, lakini hakuna hata mmoja utakaokuwa na nguvu kama ule uliovunjika.
23 “Katika sehemu ya mwisho ya utawala wao, wakati waasi watakapokuwa waovu kabisa, atainuka mfalme mwenye uso mkali, aliye stadi wa hila. 24 Atakuwa na nguvu nyingi, lakini si kwa uwezo wake mwenyewe. Atasababisha uharibifu wa kutisha, na atafanikiwa kwa chochote anachofanya. Atawaangamiza watu maarufu na watu watakatifu. 25 Atasababisha udanganyifu ustawi, naye atajihesabu mwenyewe kuwa bora. Wakati wajisikiapo kuwa wako salama, atawaangamiza wengi, na kushindana na Mkuu wa wakuu. Lakini ataangamizwa, isipokuwa si kwa uwezo wa mwanadamu.
26 “Maono kuhusu jioni na asubuhi ambayo umepewa ni kweli, lakini yatie muhuri maono haya, kwa maana yanahusu wakati mrefu ujao.”
27 Mimi Danieli nilikuwa nimechoka sana, na nikalala nikiwa mgonjwa kwa siku kadhaa. Ndipo nikaamka, nikaenda kwenye shughuli za mfalme. Nilifadhaishwa na maono hayo, nami sikuweza kuyaelewa.

*8:2 Mto Ulai ni mfereji uliokuwa kati ya Shushani na Elymaisi; sasa unaitwa Mto Karuni.