2
Kutangatanga Jangwani
Kisha tukageuka nyuma na kusafiri kuelekea jangwani kwa njia inayoelekea Bahari ya Shamu, kama Bwana alivyonielekeza. Kwa muda mrefu tulitembea kuzunguka vilima katika nchi ya Seiri.
Kisha Bwana akaniambia, “Umetembea kuzunguka hii nchi ya vilima kwa muda wa kutosha; sasa geukia kaskazini. Wape watu maagizo haya: ‘Mko karibu kupita katikati ya nchi ya ndugu zako ambao ni wazao wa Esau, ambao wanaishi Seiri. Watawaogopa, lakini mwe waangalifu. Msiwachokoze kwa vita kwa maana sitawapa ninyi sehemu yoyote ya nchi yao, hata sehemu ya kutosha kuweka wayo wenu juu yake. Nimempa Esau nchi ya vilima ya Seiri kama yake mwenyewe. Mtawalipa fedha kwa chakula mtakachokula na maji mtakayokunywa.’ ”
Bwana Mungu wenu amewabariki kwa kazi yote ya mikono yenu. Amewalinda katika safari yenu katikati ya jangwa hili kubwa. Kwa miaka hii arobaini Bwana Mungu wenu amekuwa pamoja nanyi, na hamkupungukiwa na kitu chochote.
Basi tulipita kwa ndugu zetu wazao wa Esau ambao wanaishi Seiri. Tuligeuka kutoka njia ya Araba ambayo inatokea Elathi na Esion-Geberi, tukasafiri kufuata njia ya jangwa la Moabu.
Kisha Bwana akaniambia, “Usiwasumbue Wamoabu kwa vita, kwa kuwa sitawapa sehemu yoyote ya nchi yao. Nimetoa nchi ya Ari kwa wazao wa Loti kama milki yao.”
10 (Waemi walikuwa wakiishi huko hapo zamani, watu wenye nguvu na wengi, warefu kama Waanaki. 11 Kama walivyokuwa Waanaki, hao pia walikuwa kama Warefai, lakini Wamoabu waliwaita Waemi. 12 Wahori waliishi Seiri, lakini wazao wa Esau waliwafukuza. Waliwaangamiza Wahori na kukaa mahali pao, kama Waisraeli walivyofanya katika nchi ambayo Bwana aliwapa kama milki yao.)
13 Bwana akasema, “Sasa ondokeni mvuke Bonde la Zeredi.” Hivyo tukavuka bonde.
14 Miaka thelathini na minane ilipita tangu wakati tulipoondoka Kadesh-Barnea mpaka tulipovuka Bonde la Zeredi. Kwa wakati huo kile kizazi chote cha wanaume kuanzia wale wawezao kwenda vitani kilikuwa kimekufa, kama Bwana alivyokuwa amewaapia. 15 Mkono wa Bwana uliwakabili hadi alipowaangamiza wote huko kambini.
16 Ikawa baada ya mtu wa mwisho kuanzia wale wawezao kwenda vitani kufa, 17 Bwana akaniambia, 18 “Leo utapita katika nchi ya Moabu huko Ari. 19 Utakapokuja kwa Waamoni, msiwasumbue wala kuwachokoza kwa vita, kwa kuwa sitawapa ardhi yoyote iliyo ya Waamoni kuwa milki yenu. Nimeitoa kama milki ya wazao wa Loti.”
20 (Hiyo pia ilidhaniwa kuwa nchi ya Warefai waliokuwa wakiishi huko, lakini Waamoni waliwaita Wazamzumi. 21 Walikuwa watu wenye nguvu na wengi, warefu kama Waanaki. Bwana akawaangamiza kutoka mbele ya Waamoni, ambao waliwafukuza na kukaa mahali pao. 22 Bwana alikuwa amefanya vivyo hivyo kwa wazao wa Esau, ambao waliishi Seiri, wakati alipowaangamiza Wahori watoke mbele yao. Waliwafukuza na wao wakaishi mahali pao mpaka leo. 23 Nao Waavi ambao waliishi katika vijiji mpaka Gaza, Wakaftori waliokuja kutoka Kaftori waliwaangamiza na kukaa mahali pao.)
24 “Ondoka sasa na uvuke Bonde la Arnoni. Tazama, nimemweka mikononi mwako Sihoni Mwamori, mfalme wa Heshboni na nchi yake. Anza kuimiliki nchi hiyo na umwingize katika vita. 25 Siku hii ya leo nitaanza kuwatia hofu na woga mataifa yote chini ya mbingu wawaogope ninyi. Watakaposikia taarifa zenu, watatetemeka na kufadhaika kwa sababu yenu.”
Kushindwa Kwa Sihoni Mfalme Wa Heshboni
(Hesabu 21:21-30)
26 Kutoka jangwa la Kedemothi nilituma wajumbe wenye maneno ya amani kwa Sihoni mfalme wa Heshboni kusema, 27 “Turuhusu tupite katika nchi yako. Tutapita katika barabara kuu, hatutageuka kuume wala kushoto. 28 Tuuzie chakula tule na maji tunywe kwa thamani yake katika fedha. Turuhusu tu tupite kwa miguu, 29 kama wazao wa Esau ambao wanaishi Seiri na Wamoabu ambao wanaishi Ari walivyotufanyia, mpaka tuvuke Yordani kuingia nchi ambayo Bwana Mungu wetu anatupatia.” 30 Lakini Sihoni mfalme wa Heshboni alikataa kuturuhusu kupita. Kwa kuwa Bwana Mungu wako alikuwa ameifanya roho yake kuwa ngumu na moyo wake kuwa mkaidi ili amweke kwenye mikono yenu, kama alivyofanya sasa.
31 Bwana akaniambia, “Tazama, nimeanza kuwapa Mfalme Sihoni na nchi yake kwako. Sasa anzeni kuishinda na kuimiliki nchi yake.”
32 Wakati Sihoni pamoja na jeshi lake lote walipokuja kukutana nasi katika vita huko Yahazi, 33 Bwana Mungu wetu alimweka mikononi mwetu, nasi tukamwangamiza pamoja na wanawe na jeshi lake lote. 34 Kwa wakati ule tuliteka miji yake yote na kuiangamiza kabisa: wanaume, wanawake na watoto. Hatukumwacha yeyote. 35 Lakini mifugo na nyara tulizoziteka kutoka ile miji tulijichukulia wenyewe. 36 Kutoka Aroeri kwenye ukingo wa Bonde la Arnoni, kutoka mji ulio ndani ya bonde, hata mpaka Gileadi, hapakuwa na mji hata mmoja uliokuwa na nguvu kutushinda. Bwana Mungu wetu alitupa yote. 37 Lakini kulingana na amri ya Bwana Mungu wetu, hamkujiingiza katika nchi yoyote ya Waamoni, wala katika sehemu yoyote iliyo kandokando ya Mto Yaboki, wala katika miji iliyoko katika vilima.