11
Mpende Na Umtii Bwana
1 Mpende Bwana Mungu wako na kushika masharti yake, amri zake, sheria zake na maagizo yake siku zote. 2 Kumbuka hivi leo kwamba sio watoto wako walioona na kujua adhabu ya Bwana Mungu wako: utukufu wake, mkono wake wenye nguvu, mkono wake ulionyooshwa; 3 ishara alizozifanya na mambo aliyoyafanya katikati ya Misri, kwa Farao mfalme wa Misri na kwa nchi yake yote; 4 lile alilolifanyia jeshi la Wamisri, farasi na magari yake, jinsi alivyowafurikisha na maji ya Bahari ya Shamu walipokuwa wakiwafuatilia ninyi, na jinsi Bwana alivyowaletea angamizo la kudumu juu yao. 5 Sio watoto wenu walioyaona yale Mungu aliyowafanyia huko jangwani mpaka mkafika mahali hapa, 6 wala lile Mungu alilowafanyia Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu wa kabila la Reubeni, wakati ardhi ilipofungua kinywa chake katikati ya Israeli yote, ikawameza pamoja na walio nyumbani mwao, hema zao na kila kitu kilichokuwa hai ambacho kilikuwa mali yao. 7 Bali ilikuwa ni macho yenu wenyewe ambayo yaliyaona mambo haya yote makuu Bwana aliyoyatenda.
8 Kwa hiyo fuateni maagizo yote ninayowapa leo, ili mpate kuwa na nguvu za kuingia na kuiteka nchi ile ambayo mnavuka Yordani kuimiliki, 9 ili mpate kuishi siku nyingi katika nchi ile ambayo Bwana aliapa kuwapa baba zenu na wazao wao, nchi itiririkayo maziwa na asali. 10 Nchi mnayoiingia kuimiliki haifanani na nchi ya Misri mlikotoka ambako mlipanda mbegu yenu na kuinywesha, kama bustani ya mboga. 11 Lakini nchi mnayovuka Yordani kuimiliki ni nchi ya milima na mabonde inywayo mvua kutoka mbinguni. 12 Ni nchi ambayo Bwana Mungu wenu anaitunza; macho ya Bwana Mungu wenu yanaitazama daima kutoka mwanzo wa mwaka hadi mwisho wa mwaka.
13 Hivyo kama mkiyatii maagizo yangu ninayowapa leo kwa uaminifu, yaani kwa kumpenda Bwana Mungu wenu, na kumtumikia kwa moyo wako wote na kwa roho yenu yote, 14 ndipo atawanyweshea mvua katika nchi yenu kwa majira yake, mvua ya masika na ya vuli, ili mpate kuvuna nafaka zenu, divai mpya na mafuta. 15 Nitawapa majani kwa ajili ya ngʼombe wenu, nanyi mtakula na kushiba.
16 Jihadharini, la sivyo mtashawishika kugeuka na kuabudu miungu mingine na kuisujudia. 17 Ndipo hasira ya Bwana itawaka dhidi yenu, naye atafunga mbingu ili mvua isinyeshe nayo ardhi haitatoa mazao, nanyi mtaangamia mara katika nchi nzuri ambayo Bwana anawapa. 18 Yawekeni haya maneno yangu katika mioyo yenu na akili zenu, yafungeni kama alama juu ya mikono yenu na kwenye paji za nyuso zenu. 19 Wafundisheni watoto wenu, yazungumzeni wakati mketipo nyumbani na wakati mtembeapo njiani, wakati mlalapo na wakati mwamkapo. 20 Yaandikeni juu ya miimo ya nyumba zenu na juu ya malango yenu, 21 ili kwamba siku zenu na siku za watoto wenu zipate kuwa nyingi katika nchi ile Bwana aliyoapa kuwapa baba zenu, kama zilivyo nyingi siku za mbingu juu ya nchi.
22 Kama mkishika kwa makini maagizo haya yote ninayowapa kuyafuata, ya kumpenda Bwana Mungu wenu, kuenenda katika njia zake zote na kushikamana naye kwa uthabiti, 23 ndipo Bwana atawafukuza mataifa haya yote mbele yako, nawe utawafukuza mataifa yaliyo makubwa na yenye nguvu kukuliko wewe. 24 Kila mahali mtakapoweka mguu wenu patakuwa penu: Nchi yenu itaenea kutoka jangwa la Lebanoni, na kutoka mto wa Frati hadi bahari ya magharibi*Yaani Bahari ya Mediterania. 25 Hapatakuwa na mtu atakayeweza kusimama dhidi yenu. Bwana Mungu wenu, kama alivyoahidi, ataweka juu ya nchi yote utisho na hofu kwa ajili yenu popote mwendako.
26 Tazama, leo ninaweka mbele yenu baraka na laana: 27 baraka kama mtatii maagizo ya Bwana Mungu wenu, ambayo ninawapa leo; 28 laana kama hamtatii maagizo ya Bwana Mungu wenu na kuacha njia ambayo ninawaamuru leo kwa kufuata miungu mingine, ambayo hamkuijua. 29 Wakati Bwana Mungu wenu atakapokuwa amewaleta katika nchi mnayoiingia kuimiliki, mtatangaza baraka kutoka Mlima Gerizimu, na kutangaza laana kutoka Mlima Ebali. 30 Kama mnavyofahamu, milima hii ipo ngʼambo ya Yordani, magharibi ya barabara, kuelekea machweo ya jua, karibu na miti mikubwa ya More, katika nchi ya wale Wakanaani wanaoishi Araba, jirani na Gilgali. 31 Karibu mvuke ngʼambo ya Yordani kuingia na kuimiliki nchi ambayo Bwana Mungu wenu anawapa. Wakati mtakapokuwa mmeichukua na mnaishi humo, 32 hakikisheni kwamba mnatii amri na sheria zote ninazoziweka mbele yenu leo.