4
Uonevu, Taabu, Uadui
Nikatazama tena nikaona uonevu wote uliokuwa unafanyika chini ya jua:
Nikaona machozi ya walioonewa,
wala hawana wa kuwafariji;
uwezo ulikuwa upande wa wale wanaowaonea,
wala hawana wa kuwafariji.
Nami nikasema kwamba wafu,
waliokwisha kufa,
wana furaha kuliko watu walio hai,
ambao bado wanaishi.
Lakini aliye bora kuliko hao wawili
ni yule ambaye hajazaliwa bado,
ambaye hajaona ule uovu
unaofanyika chini ya jua.
Tena nikaona kuwa kazi zote na mafanikio yote huchipuka kutokana na wivu wa mtu kwa jirani yake. Hili nalo ni ubatili, ni kukimbiza upepo.
Mpumbavu hukunja mikono yake
na kujiangamiza mwenyewe.
Afadhali konzi moja pamoja
na utulivu kuliko konzi mbili pamoja na taabu
na kukimbiza upepo.
Tena nikaona kitu kingine kilicho ubatili chini ya jua:
Kulikuwepo mwanadamu aliye peke yake,
hakuwa na mwana wala ndugu.
Hapakuwa na mwisho wa kazi yake,
hata hivyo macho yake
hayakutosheka na utajiri wake.
Aliuliza, “Ninajitaabisha hivi kwa ajili ya nani,
nami kwa nini ninajinyima kufurahia?”
Hili pia ni ubatili,
ni shughuli yenye taabu!
 
Wawili ni afadhali kuliko mmoja,
kwa sababu wana malipo mazuri kwa kazi yao:
10 Kama mmoja akianguka,
mwenzake atamwinua.
Lakini ni jambo la kuhuzunisha
kwa mtu yule aangukaye
naye hana wa kumwinua!
11 Pia, kama wawili wakilala pamoja
watapashana joto.
Lakini ni vipi mtu aweza
kujipasha joto mwenyewe?
12 Ingawa mtu mmoja aweza kushindwa,
watu wawili wanaweza
kumkabili adui na kumshinda.
Kamba ya nyuzi tatu
haikatiki kwa urahisi.
Maendeleo Ni Ubatili
13 Afadhali kijana maskini mwenye hekima kuliko mfalme mzee mpumbavu ambaye hajui tena kupokea maonyo. 14 Kijana huyo angeweza kutokea gerezani akapata ufalme, au angeweza kuwa amezaliwa katika umaskini kwenye huo ufalme. 15 Nikaona kwamba wote walioishi na kutembea chini ya jua walimfuata kijana, aliyepokea ufalme. 16 Hapakuwa na kikomo cha watu wote aliowatawala. Lakini wale waliokuja baadaye hawakufurahia kazi ya yule aliyepokea ufalme. Hili nalo pia ni ubatili, ni kukimbiza upepo.