17
Maji Kutoka Kwenye Mwamba
(Hesabu 20:1-13)
Jumuiya yote ya Israeli ikaondoka kutoka Jangwa la Sini, ikisafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine kama Bwana alivyoagiza. Wakapiga kambi huko Refidimu, lakini hapakuwa na maji ya watu kunywa. Kwa hiyo wakagombana na Mose wakisema, “Tupe maji ya kunywa.”
Mose akajibu, “Mbona mnagombana nami? Kwa nini mnamjaribu Bwana?”
Lakini watu walikuwa na kiu huko, wakanungʼunika dhidi ya Mose, wakisema, “Kwa nini ulitutoa kule Misri, ukatuleta hapa utuue kwa kiu sisi, watoto wetu na mifugo yetu?”
Kisha Mose akamlilia Bwana, akasema, “Niwafanyie nini watu hawa? Sasa wanakaribia kunipiga kwa mawe.”
Bwana akamjibu Mose, “Pita mbele ya watu. Wachukue pamoja nawe baadhi ya wazee wa Israeli, ichukue mkononi mwako ile fimbo uliyopiga nayo Mto Naili, nawe uende. Huko nitasimama mbele yako karibu na mwamba wa Horebu. Uupige mwamba na maji yatatoka ndani yake kwa ajili ya watu kunywa.” Kwa hiyo Mose akafanya haya mbele ya wazee wa Israeli. Naye akapaita mahali pale Masa,*Masa maana yake ni Kujaribu. na MeribaMeriba maana yake ni Kugombana. kwa sababu Waisraeli waligombana na kumjaribu Bwana wakisema, “Je, Bwana yu pamoja nasi au la?”
Vita Na Waamaleki
Waamaleki wakaja na kuwashambulia Waisraeli huko Refidimu. Mose akamwambia Yoshua, “Chagua baadhi ya watu wetu na uende kupigana na Waamaleki. Kesho nitasimama juu ya kilima nikiwa na fimbo ya Mungu mkononi mwangu.”
10 Kwa hiyo Yoshua akapigana na Waamaleki kama Mose alivyomwagiza, nao Mose, Aroni na Huri wakapanda juu ya kilima. 11 Ikawa wakati wote Mose alipokuwa amenyanyua mikono yake, Waisraeli walikuwa wakishinda, lakini kila aliposhusha mikono yake Waamaleki walishinda. 12 Mikono ya Mose ilipochoka, wakachukua jiwe na kumpa alikalie. Aroni na Huri wakaishikilia juu mikono ya Mose, mmoja upande huu na mwingine upande huu. Wakaitegemeza mikono yake ikabaki thabiti mpaka jua lilipozama. 13 Kwa hiyo Yoshua akalishinda jeshi la Waamaleki kwa upanga.
14 Kisha Bwana akamwambia Mose, “Andika mambo haya katika kitabu ili yakumbukwe, na uhakikishe kwamba Yoshua amesikia, kwa sababu nitafuta kabisa kumbukumbu la Amaleki chini ya mbingu.”
15 Mose akajenga madhabahu na kuiita Yehova Nisi.Yehova Nisi maana yake ni Bwana ni Bendera yangu. 16 Mose akasema, “Kwa maana mikono iliinuliwa mpaka kwenye kiti cha enzi cha Bwana. Bwana atakuwa na vita dhidi ya Waamaleki kutoka kizazi hata kizazi.”

*17:7 Masa maana yake ni Kujaribu.

17:7 Meriba maana yake ni Kugombana.

17:15 Yehova Nisi maana yake ni Bwana ni Bendera yangu.