22
Ulinzi Wa Mali
1 “Kama mtu akiiba maksai au kondoo na kumchinja au kumuuza, ni lazima alipe ngʼombe watano badala ya maksai mmoja na kondoo wanne badala ya kondoo mmoja.
2 “Kama mwizi akishikwa anavunja nyumba akapigwa hata akafa, aliyemuua hana hatia ya kumwaga damu; 3 lakini jambo hilo likitokea wakati jua limechomoza, huyo mtu atakuwa na hatia ya kumwaga damu.
“Mwizi huyo sharti alipe, lakini kama hana kitu, lazima auzwe ili alipe kwa ajili ya wizi wake.
4 “Kama mnyama aliyeibwa akikutwa hai mikononi mwake, ikiwa ni maksai au punda au kondoo, lazima alipe mara mbili.
5 “Kama mtu akichunga mifugo yake katika shamba au shamba la mizabibu, na akawaachia wajilishe katika shamba la mtu mwingine, ni lazima alipe vitu bora kutoka kwenye shamba lake mwenyewe au kutoka shamba lake la mizabibu.
6 “Kama moto ukiwaka na kuenea kwenye vichaka vya miiba na kuteketeza miganda ya nafaka au nafaka ambayo haijavunwa, au kuteketeza shamba lote, mtu yule aliyewasha moto lazima alipe.
7 “Kama mtu akimpa jirani yake fedha au mali nyingine amtunzie, na kama vikiibwa kutoka nyumba ya huyo jirani, kama mwizi atashikwa, lazima alipe mara mbili. 8 Lakini mwizi asipopatikana, mwenye nyumba atafika mbele ya waamuzi ili kuthibitisha kuwa hakuchukua mali ya mwenzake. 9 Pakiwepo jambo lolote la mali isiyo halali, ikiwa ni maksai, punda, kondoo, mavazi, ama mali yoyote iliyopotea ambayo fulani atasema, ‘Hii ni mali yangu,’ pande zote mbili wataleta mashauri yao mbele ya waamuzi. Yule ambaye waamuzi watamwona kuwa na hatia atamlipa jirani yake mara mbili.
10 “Kama mtu akimpa jirani yake punda, ngʼombe, kondoo au mnyama mwingine yeyote amtunzie, akifa au akijeruhiwa au akichukuliwa wakati haonekani na mtu yeyote, 11 jambo hili kati yao wawili litaamuliwa kwa kuapa kiapo mbele za Bwana, kwamba huyo jirani hakuhusika na wizi wa mali ya jirani yake. Mwenye mali itampasa akubali jambo hili, na hakuna malipo yatakayohitajika. 12 Lakini kama mnyama aliibwa kwa jirani, itampasa amlipe mwenye mnyama. 13 Kama ameraruliwa na mnyama pori, ataleta mabaki ya mnyama kama ushahidi, naye hatadaiwa kulipa mnyama aliyeraruliwa.
14 “Kama mtu akimwazima mnyama kutoka kwa jirani yake, na kama akiumia au akafa na mwenye mnyama hayupo, lazima amlipe huyo mnyama. 15 Lakini mwenye mnyama akiwa angalipo na mnyama wake, mwazimaji hatalazimika kumlipa. Kama mnyama alikuwa amekodishwa, fedha iliyolipwa kwa kukodisha inatosha kwa kufidia hasara.
Uwajibikaji Wa Kijamii
16 “Kama mtu akimshawishi bikira ambaye hajaposwa na akilala naye, lazima alipe mahari, kisha atamwoa msichana huyo. 17 Baba wa msichana akikataa katakata kumpa huyo mtu huyo msichana wake, bado ni lazima huyo mtu atalipa mahari kama inavyostahili malipo ya ubikira.
18 “Usiruhusu mwanamke mchawi aishi.
19 “Mtu yeyote aziniye na mnyama lazima auawe.
20 “Mtu awaye yote anayemtolea mungu mwingine dhabihu isipokuwa Bwana, lazima aangamizwe.
21 “Usimtendee mgeni vibaya au kumwonea, kwa kuwa nanyi mlikuwa wageni huko Misri.
22 “Usimdhulumu mjane wala yatima. 23 Kama ukifanya hivyo nao wakinililia, hakika nitasikia kilio chao. 24 Hasira yangu itawaka, nami nitawaua kwa upanga, wake zenu watakuwa wajane na watoto wenu watakuwa yatima.
25 “Kama ukimkopesha mmojawapo wa watu wangu fedha ambaye ni mhitaji, usiwe kama mtu mkopesha fedha; usimtoze riba. 26 Kama ukichukua vazi la jirani kama rehani, ulirudishe kwake kabla jua kuzama, 27 kwa kuwa vazi lake ndilo pekee alilo nalo la kumfunika mwili wake. Ni nini kingine atajifunika nacho? Atakaponililia, nitasikia, kwa kuwa nina huruma.
28 “Usimkufuru Mungu au kumlaani mtawala wa watu wako.
29 “Usiache kutoa sadaka kutoka ghala lako au mapipa yako.
“Lazima unipe mzaliwa wa kwanza wa wana wako. 30 Ufanye vivyo hivyo kwa ngʼombe wako na kwa kondoo wako. Waache wakae na mama zao kwa siku saba, lakini siku ya nane unipe.
31 “Ninyi mtakuwa watu wangu watakatifu. Kwa hiyo msile nyama ya mnyama aliyeraruliwa na wanyama pori; mtupieni mbwa.