39
Mavazi Ya Kikuhani
(Kutoka 28:1-14)
Kutokana na nyuzi za rangi ya buluu, ya zambarau na nyekundu akatengeneza mavazi yaliyofumwa kwa ajili ya kuhudumu katika mahali patakatifu. Pia akamshonea Aroni mavazi matakatifu, kama Bwana alivyomwagiza Mose.
Kisibau
Akatengeneza kisibau cha dhahabu, na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na nyekundu na kitani iliyosokotwa vizuri. Akafua vipande vyembamba vya dhahabu kwa nyundo na kutengeneza nyuzi nyembamba ili kuzifuma pamoja na hizo nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu na kitani safi, kazi ya fundi stadi. Akatengeneza vipande vya mabegani vya kisibau, vilivyoshikizwa kwenye pembe zake mbili ili kukifungia kisibau. Mshipi wa kiunoni uliofumwa kwa ustadi ulifanana nacho: ulikuwa kitu kimoja na hicho kisibau, nao ulitengenezwa kwa dhahabu na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na nyekundu na kwa kitani iliyosokotwa vizuri, kama Bwana alivyomwagiza Mose.
Akatengeneza vito vya shohamu vilivyowekwa katika vijalizo vya dhahabu, navyo vilichorwa na majina ya wana wa Israeli kama vile muhuri huchorwa. Kisha akavifungia kwenye vipande vya mabega ya kisibau kuwa vito vya ukumbusho kwa wana wa Israeli, kama Bwana alivyomwagiza Mose.
Kifuko Cha Kifuani
(Kutoka 28:15-30)
Akafanyiza kifuko cha kifuani, kazi ya fundi stadi. Akakitengeneza kama kile kisibau: cha dhahabu, na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu, cha kitani safi iliyosokotwa. Kifuko hicho kilikuwa cha mraba, chenye urefu wa shibiri moja*Shibiri moja ni sawa na sentimita 22. na upana wa shibiri moja, nacho kilikunjwa mara mbili. 10 Kifuko hicho kilipambwa kwa safu nne za vito vya thamani. Safu ya kwanza ilikuwa na akiki, yakuti manjano na zabarajadi; 11 safu ya pili ilikuwa na almasi, yakuti samawi na zumaridi; 12 safu ya tatu ilikuwa na hiakintho, akiki nyekundu na amethisto; 13 katika safu ya nne ilikuwa na krisolitho, shohamu na yaspi. Vito hivyo vilitiwa kwenye vijalizo vya dhahabu. 14 Palikuwa na vito kumi na viwili, kila kimoja kikiwa na jina mojawapo la wana wa Israeli; kila kimoja kilichorwa kama muhuri kikiwa na jina mojawapo la yale makabila kumi na mawili.
15 Kwa ajili ya kile kifuko cha kifuani akakitengenezea mikufu ya dhahabu safi, iliyosokotwa kama kamba. 16 Akatengeneza vijalizo viwili vya dhahabu na pete mbili za dhahabu, na kuzifungia pete hizo kwenye pembe mbili za hicho kifuko cha kifuani. 17 Akafunga hiyo mikufu miwili ya dhahabu kwenye hizo pete katika pembe za hicho kifuko cha kifuani, 18 nazo zile ncha nyingine za mkufu akazifunga kwenye vile vijalizo viwili, na kuzishikamanisha na vile vipande vya mabega vya kile kisibau upande wa mbele. 19 Akatengeneza pete mbili za dhahabu na kuzishikamanisha kwenye pembe mbili za chini, upande wa ndani wa kifuko cha kifuani karibu na kisibau. 20 Kisha akatengeneza pete nyingine mbili za dhahabu na kuzishikamanisha sehemu ya chini ya vipande vya mabega upande wa mbele wa kile kisibau, karibu na pindo juu kidogo ya mshipi wa kiunoni wa kisibau. 21 Akafunga pete za hicho kifuko cha kifuani kwenye pete za kisibau kwa kamba ya buluu, wakiziunganisha na ule mshipi wa kiunoni, ili kifuko cha kifuani kisisogee kutoka kwenye kile kisibau, kama Bwana alivyomwagiza Mose.
Mavazi Mengine Ya Kikuhani
(Kutoka 28:31-43)
22 Akashona joho la kisibau lote kwa kitambaa cha rangi ya buluu tupu, kazi ya mfumaji, 23 na lilikuwa na nafasi ya shingo katikati ya joho lile iliyofanana na ukosi, na utepe ulioshonwa kuizunguka nafasi hiyo ili isichanike. 24 Akatengeneza makomamanga ya nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na nyekundu na ya kitani iliyosokotwa vizuri kuzunguka pindo la hilo joho. 25 Kisha akatengeneza vikengele vya dhahabu safi na kuvishikamanisha kuzunguka pindo hilo kati ya hayo makomamanga. 26 Hivyo vikengele na makomamanga vilipishana kuzunguka upindo wa joho ili livaliwe kwa kuhudumu, kama Bwana alivyomwagiza Mose.
27 Pia akamtengenezea Aroni na wanawe makoti ya kitani safi, kazi ya mfumaji, 28 na kilemba cha kitani safi, tepe za kichwani za kitani, na nguo za ndani za kitani iliyosokotwa vizuri. 29 Mshipi ulikuwa wa kitani iliyosokotwa vizuri ya rangi ya buluu, na zambarau, na nyekundu, kazi ya mtarizi, kama Bwana alivyomwagiza Mose.
30 Kisha akatengeneza lile bamba, taji takatifu, kwa dhahabu safi na kuchora juu yake maneno haya kama vile muhuri huchorwa: Mtakatifu kwa Bwana. 31 Kisha wakalifunga kwa kamba ya rangi ya buluu ili kulishikamanisha na kile kilemba kama Bwana alivyomwagiza Mose.
Mose Akagua Maskani Ya Mungu
(Kutoka 35:10-19)
32 Kwa hiyo kazi yote ya maskani, Hema la Kukutania ikakamilika. Waisraeli wakafanya kila kitu sawasawa kama vile Bwana alivyomwagiza Mose. 33 Ndipo wakaleta maskani kwa Mose: hema pamoja na vifaa vyake vyote, vibanio vyake, mihimili yake, mataruma yake, nguzo na vitako vyake; 34 kifuniko cha ngozi za kondoo dume kilichotiwa rangi nyekundu, kifuniko cha ngozi za pomboo,Pomboo hapa ina maana ya mnyama mwenye ngozi laini aishiye kwenye milima yenye misitu, au pengine nguva au sili. pazia la kufunikia; 35 Sanduku la Ushuhuda pamoja na mipiko yake na kiti cha rehema, 36 meza pamoja na vyombo vyake vyote na mikate ya Wonyesho; 37 kinara cha taa cha dhahabu safi, safu zake za taa pamoja na vifaa vyake vyote pamoja na mafuta kwa ajili ya taa; 38 madhabahu ya dhahabu, mafuta ya upako, uvumba wenye harufu nzuri na pazia la ingilio la hema; 39 madhabahu ya shaba, pamoja na wavu wa shaba, nguzo zake na vyombo vyake vyote, sinia, na tako lake; 40 mapazia ya ua pamoja na nguzo na vitako vyake, pia na pazia kwa ajili ya ingilio la kwenye ua; kamba zake na vigingi vya hema kwa ajili ya ua; vyombo vyote vilivyohitajiwa kwa ajili ya maskani, Hema la Kukutania; 41 na mavazi yaliyofumwa yanayovaliwa wakati wa huduma katika mahali patakatifu, yaani mavazi matakatifu ya kuhani Aroni na mavazi kwa ajili ya wanawe watakapokuwa wakihudumu katika kazi ya ukuhani.
42 Waisraeli walikuwa wamefanya kazi yote sawasawa na vile Bwana alivyokuwa amemwagiza Mose. 43 Mose akakagua kazi na kuona kuwa walikuwa wameifanya sawasawa kama vile Bwana alivyokuwa ameagiza. Kwa hiyo Mose akawabariki.

*39:9 Shibiri moja ni sawa na sentimita 22.

39:34 Pomboo hapa ina maana ya mnyama mwenye ngozi laini aishiye kwenye milima yenye misitu, au pengine nguva au sili.