Ezekieli
1
Viumbe Hai Na Utukufu Wa Bwana
Katika mwaka wa thelathini, mwezi wa nne, siku ya tano ya mwezi, wakati nilipokuwa miongoni mwa hao waliokuwa uhamishoni kando ya Mto Kebari, mbingu zilifunguka nami nikaona maono ya Mungu.
Katika siku ya tano ya mwezi, ilikuwa mwaka wa tano wa kuhamishwa kwa Mfalme Yehayakini, neno la Bwana lilimjia Ezekieli kuhani, mwana wa Buzi, kando ya Mto Kebari, katika nchi ya Wakaldayo. Huko mkono wa Bwana ulikuwa juu yake.
Nilitazama, nikaona dhoruba kubwa ikitoka kaskazini, wingu kubwa sana pamoja likiwa na umeme wa radi likiwa limezungukwa na mwanga mkali. Katikati ya huo moto kulikuwa kama rangi ya manjano ya chuma kinapokuwa ndani ya moto. Katika ule moto kulikuwa na kitu kinachofanana na viumbe vinne vyenye uhai. Katika kuonekana kwake vilikuwa na umbo mfano wa mwanadamu, lakini kila kimoja kilikuwa na nyuso nne na mabawa manne. Miguu yao ilikuwa imenyooka, nyayo za miguu yao zilikuwa kama kwato za miguu ya ndama, nazo zilimetameta kama shaba iliyosuguliwa. Chini ya mabawa yao katika pande zao nne walikuwa na mikono ya mwanadamu. Wote wanne walikuwa na nyuso na mabawa, nayo mabawa yao yaligusana. Kila mmoja alikwenda kuelekea mbele moja kwa moja, hawakugeuka walipokuwa wanatembea.
10 Kuonekana kwa nyuso zao kulikuwa hivi: Kila mmoja wa wale wanne alikuwa na uso wa mwanadamu na kwa upande wa kulia kila mmoja alikuwa na uso wa simba, upande wa kushoto alikuwa na uso wa ngʼombe pia kila mmoja alikuwa na uso wa tai. 11 Hivyo ndivyo zilivyokuwa nyuso zao. Mabawa yao yalikunjuliwa kuelekea juu, kila mmoja alikuwa na mabawa mawili ambayo kila moja liligusa bawa la mwenzake kila upande na mabawa mengine mawili yakifunika mwili wake. 12 Kila mmoja alikwenda kuelekea mbele moja kwa moja. Popote roho alipotaka kwenda, ndipo walipokwenda pasipo kugeuka. 13 Kuonekana kwa vile viumbe hai katikati kulikuwa kama makaa ya mawe yanayowaka au kama mienge. Moto ule ulikuwa ukienda mbele na nyuma katikati ya vile viumbe, ulikuwa na mwangaza mkali na katikati ya ule moto kulitoka kimulimuli kama umeme wa radi. 14 Vile viumbe vilipiga mbio kwenda na kurudi, kama vimulimuli vya umeme wa radi.
15 Nilipokuwa nikitazama vile viumbe hai, niliona gurudumu moja juu ya ardhi kando ya kila kiumbe kikiwa na nyuso zake nne. 16 Hivi ndivyo ilivyokuwa kuonekana kwa hayo magurudumu na muundo wake: yalingʼaa kama zabarajadi, nayo yote manne yalifanana. Kila gurudumu lilikuwa na gurudumu jingine ndani yake. 17 Yalipokwenda yalielekea upande wowote wa pande nne walipoelekea wale viumbe, magurudumu hayakuzunguka wakati viumbe vile vilipokwenda. 18 Kingo zake zilikuwa ndefu kwenda juu na za kutisha, nazo zote nne zilijawa na macho pande zote.
19 Vile viumbe hai vilipokwenda, magurudumu yaliyokuwa kando yao yalisogea na wakati hivyo viumbe hai vilipoinuka kutoka ardhini magurudumu nayo yaliinuka. 20 Mahali popote roho alipokwenda wale viumbe nao walikwenda, nayo magurudumu yaliinuka pamoja navyo, kwa sababu roho ya vile viumbe hai alikuwa ndani ya hayo magurudumu. 21 Wakati viumbe vile viliposogea, nayo magurudumu yalisogea, viumbe viliposimama kimya, nayo pia yalisimama kimya, viumbe vilipoinuka juu ya nchi magurudumu yaliinuliwa pamoja navyo kwa kuwa roho ya hivyo viumbe hai alikuwa ndani ya hayo magurudumu.
22 Juu ya vichwa vya hao viumbe hai palikuwa na kitu mfano wa eneo lililokuwa wazi, lililokuwa angavu kabisa na lenye kutisha. 23 Chini ya hiyo nafasi mabawa yao yalitanda moja kuelekea jingine, kila mmoja alikuwa na mabawa mengine mawili yaliyofunika mwili wake. 24 Viumbe wale waliposogea nilisikia sauti ya mabawa yao, kama ngurumo ya maji yaendayo kasi, kama sauti ya Mwenyezi,* Mwenyezi hapa ina maana ya Shaddai kwa Kiebrania. kama makelele ya jeshi. Waliposimama kimya walishusha mabawa yao.
25 Ndipo ikaja sauti toka juu ya ile nafasi ya wazi iliyokuwa juu ya vichwa vyao, waliposimama mabawa yao yakiwa yameshushwa. 26 Juu ya ile nafasi ya wazi iliyokuwa juu ya vichwa vyao kulikuwa na kitu mfano wa kiti cha enzi cha yakuti samawi. Na juu ya kile kiti cha enzi kulikuwa na umbo mfano wa mwanadamu. 27 Nikaona kwamba kutokana na kile nilichoona kama kiuno chake kuelekea juu alionekana kama chuma inayowaka kana kwamba imejaa moto na kuanzia kiuno kwenda chini alionekana kama moto na mwanga mkali ulimzunguka. 28 Kama vile kuonekana kwa upinde wa mvua mawinguni siku ya mvua, ndivyo ulivyokuwa ule mngʼao uliomzunguka.
Hivi ndivyo ilivyokuwa kuonekana kwa utukufu wa Bwana. Nilipouona, nikaanguka kifudifudi, nikasikia sauti ya mtu anaongea.

*1:24 Mwenyezi hapa ina maana ya Shaddai kwa Kiebrania.