15
Yerusalemu Mzabibu Usiofaa
Neno la Bwana likanijia kusema: “Mwanadamu, je, ni vipi mti wa mzabibu unaweza kuwa bora zaidi kuliko tawi la mti mwingine wowote ndani ya msitu? Je, mti wake kamwe huchukuliwa na kutengeneza chochote cha manufaa? Je, watu hutengeneza vigingi vya kuningʼinizia vitu kutokana na huo mti wake? Nao baada ya kutiwa motoni kama nishati na moto ukateketeza ncha zote mbili na kuunguza sehemu ya kati, je, unafaa kwa lolote? Kama haukufaa kitu chochote ulipokuwa mzima, je, si zaidi sana sasa ambapo hauwezekani kufanyishwa chochote cha kufaa baada ya moto kuuchoma na kuuunguza?
“Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Kama nilivyoutoa mti wa mzabibu miongoni mwa miti ya msituni kuwa nishati kwa ajili ya moto, hivyo ndivyo nitakavyowatendea watu waishio Yerusalemu. Nitaukaza uso wangu dhidi yao. Ingawa watakuwa wameokoka kwenye moto, bado moto utawateketeza. Nami nitakapoukaza uso wangu dhidi yao, ninyi mtajua kwamba Mimi ndimi Bwana. Nitaifanya nchi kuwa ukiwa kwa sababu wamekuwa si waaminifu, asema Bwana Mwenyezi.”