17
Tai Wawili Na Mizabibu
Neno la Bwana likanijia kusema: “Mwanadamu, tega kitendawili, ukawaambie nyumba ya Israeli fumbo. Waambie hivi, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Tai mkubwa mwenye mabawa yenye nguvu, yaliyojaa manyoya marefu ya rangi mbalimbali, alikuja Lebanoni. Akatua kwenye kilele cha mwerezi, akakwanyua ncha yake na kuichukua mpaka nchi ya wafanyabiashara, akaipanda huko katika mji wa wachuuzi.
“ ‘Akachukua baadhi ya mbegu za nchi yako na kuziweka katika udongo wenye rutuba. Akazipanda kama mti umeao kando ya maji mengi, nazo zikaota na kuwa mzabibu mfupi, unaoeneza matawi yake. Matawi yake yakamwelekea huyo tai, mizizi yake ikabaki chini ya huo mzabibu. Kwa hiyo ukawa mzabibu na kutoa matawi na vitawi vyenye majani mengi.
“ ‘Lakini kulikuwa na tai mwingine mkubwa, mwenye mabawa yenye nguvu yaliyojaa manyoya. Tazama! Huu mzabibu ukatoa mizizi yake kumwelekea huyo tai kutoka mle kwenye shamba lile ulikopandwa na kutanda matawi yake kumwelekea kwa ajili ya kupata maji. Ulikuwa umepandwa katika udongo mzuri wenye maji mengi ili uweze kutoa matawi, kuzaa matunda na uweze kuwa mzabibu mzuri sana.’
“Waambie, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Je, utastawi? Je, hautangʼolewa na kuondolewa matunda yake, ili uweze kunyauka? Majani yake mapya yanayochipua yote yatanyauka. Hautahitaji mkono wenye nguvu au watu wengi kuungʼoa na mizizi yake. 10 Hata kama utapandwa pengine, Je, utastawi? Je, hautanyauka kabisa wakati upepo wa mashariki utakapoupiga, yaani, hautanyauka kabisa katika udongo mzuri ambamo ulikuwa umestawi vizuri?’ ”
11 Ndipo neno la Bwana likanijia kusema: 12 “Waambie nyumba hii ya kuasi, ‘Je, mnajua hii ina maana gani?’ Waambie: ‘Mfalme wa Babeli alikwenda Yerusalemu na kumchukua mfalme na watu maarufu, akarudi nao na kuwaleta mpaka Babeli. 13 Ndipo akamchukua mmoja wa jamaa ya mfalme na kufanya mapatano naye, akamfanya aape. Akawachukua pia viongozi wa nchi, 14 ili kuudhoofisha ufalme huo, usiweze kuinuka tena, ila uweze kuendelea tu chini ya mapatano yake. 15 Lakini mfalme aliasi dhidi yake kwa kutuma wajumbe wake kwenda Misri ili kupatiwa farasi na jeshi kubwa. Je, atashinda? Je, atafanikiwa? Je, mtu afanyaye mambo kama hayo ataokoka? Je, atavunja mapatano na bado aokoke?
16 “ ‘Hakika kama niishivyo, asema Bwana Mwenyezi, atafia huko Babeli, katika nchi ya mfalme aliyemketisha katika kiti cha enzi, ambaye alidharau kiapo chake na kuvunja mapatano yake. 17 Farao na jeshi lake kubwa, na wingi wake wa watu hawataweza kusaidia chochote katika vita, wakati watakapozungukwa na jeshi ili kukatilia mbali maisha ya watu wengi. 18 Alidharau kiapo kwa kuvunja Agano. Kwa sababu aliahidi kwa mkono wake mwenyewe na bado akafanya mambo haya yote, hataokoka.
19 “ ‘Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Hakika kama niishivyo, nitaleta juu ya kichwa chake kiapo changu, alichokidharau na Agano langu lile alilolivunja. 20 Nitautandaza wavu wangu kwa ajili yake, naye atanaswa katika mtego wangu. Nitamleta mpaka Babeli na kutekeleza hukumu juu yake huko kwa kuwa hakuwa mwaminifu kwangu. 21 Askari wake wote wanaotoroka wataanguka kwa upanga, nao watakaonusurika watatawanyika katika pande zote za dunia. Ndipo utakapojua kuwa Mimi Bwana nimesema.
Hatimaye Israeli Kutukuzwa
22 “ ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Mimi mwenyewe nitachukua chipukizi kutoka kwenye kilele cha juu sana cha mwerezi na kukipanda, nitavunja kitawi kichanga kutoka matawi yake ya juu kabisa na kukipanda juu ya mlima mrefu ulioinuka sana. 23 Katika vilele vya mlima mrefu wa Israeli nitakipanda, kitatoa matawi na kuzaa matunda na kuwa mwerezi mzuri sana. Ndege wa kila aina wataweka viota vyao ndani yake, nao watapata makazi katika kivuli cha matawi yake. 24 Miti yote ya kondeni itajua kuwa Mimi Bwana ninaishusha miti mirefu na kuikuza miti mifupi kuwa miti mirefu. Mimi naikausha miti mibichi na kuifanya miti mikavu istawi.
“ ‘Mimi Bwana nimesema, nami nitatenda.’ ”