22
Dhambi Za Yerusalemu
Neno la Bwana likanijia kusema: “Mwanadamu, je, wewe utauhukumu? Je, utauhukumu huu mji umwagao damu? Basi uujulishe juu ya matendo yake yote ya machukizo uuambie: ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Ee mji ule ujileteao maangamizi wenyewe kwa kumwaga damu ndani yake na kujinajisi wenyewe kwa kutengeneza sanamu, umekuwa na hatia kwa sababu ya damu uliyomwaga na umetiwa unajisi kwa sanamu ulizotengeneza. Umejiletea mwisho wa siku zako na mwisho wa miaka yako umewadia. Kwa hiyo nitakufanya kitu cha kudharauliwa kwa mataifa na kitu cha mzaha kwa nchi zote. Wale walio karibu na wale walio mbali watakudhihaki, Ewe mji wenye sifa mbaya, uliyejaa ghasia.
“ ‘Ona jinsi kila mkuu wa Israeli aliyeko ndani yako anavyotumia nguvu zake kumwaga damu. Ndani yako wamewadharau baba na mama, ndani yako wamewatendea wageni udhalimu na kuwaonea yatima na wajane. Mmedharau vitu vyangu vitakatifu na kuzinajisi Sabato zangu. Ndani yako wako watu wasingiziaji, watu walio tayari kumwaga damu, ndani yako wako wale wanaokula vyakula vilivyotolewa mahali pa ibada za miungu kwenye milima, na kutenda matendo ya uasherati. 10 Ndani yako wako wale wanaovunjia heshima vitanda vya baba zao, ndani yako wamo wale wanaowatendea wanawake jeuri wakiwa katika hedhi, wakati wakiwa si safi. 11 Ndani yako mtu hufanya mambo ya machukizo na mke wa jirani yake, mwingine kwa aibu kubwa hukutana kimwili na mke wa mwanawe, mwingine humtenda jeuri dada yake, binti wa baba yake hasa. 12 Ndani yako watu hupokea rushwa ili kumwaga damu, mnapokea riba na faida ya ziada na kupata faida isiyokuwa halali kutoka kwa jirani ili kupata faida kubwa kupita kiasi. Nawe umenisahau mimi, asema Bwana Mwenyezi.
13 “ ‘Hakika nitapiga makofi kwa ajili ya faida isiyo halali uliyojipatia na kwa damu uliyoimwaga ndani yako. 14 Je, ujasiri wako utadumu au mikono yako itakuwa na nguvu siku hiyo nitakapokushughulikia? Mimi Bwana nimesema na nitalifanya. 15 Nitakutawanya miongoni mwa mataifa na kukutapanya katika nchi mbalimbali nami nitakomesha unajisi wako. 16 Ukiisha kunajisika mbele ya mataifa, utajua kuwa Mimi ndimi Bwana.’ ”
17 Ndipo neno la Bwana likanijia kusema: 18 “Mwanadamu, nyumba ya Israeli imekuwa kwangu takataka ya chuma, wote kwangu wamekuwa shaba, bati, chuma na risasi iliyoachwa kalibuni. Wao ni taka ya madini ya fedha tu. 19 Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: ‘Kwa kuwa wote mmekuwa takataka ya chuma, nitawakusanya Yerusalemu. 20 Kama vile watu wakusanyavyo fedha, shaba, chuma, risasi na bati kalibuni ili kuyeyusha kwa moto mkali, ndivyo nitakavyowakusanya katika hasira yangu na ghadhabu yangu kuwaweka ndani ya mji na kuwayeyusha. 21 Nitawakusanya na kupuliza juu yenu moto wa hasira yangu na ghadhabu yangu nanyi mtayeyushwa ndani ya huo mji. 22 Kama fedha iyeyukavyo kalibuni, ndivyo mtakavyoyeyuka ndani ya huo mji, nanyi mtajua kuwa Mimi Bwana nimemwaga ghadhabu yangu juu yenu.’ ”
23 Neno la Bwana likanijia tena kusema: 24 “Mwanadamu, iambie nchi, ‘Wewe ni nchi ambayo haijapata mvua wala manyunyu katika siku ya ghadhabu.’ 25 Kuna hila mbaya ya wakuu ndani yake kama simba angurumaye akirarua mawindo yake, wanakula watu, wanachukua hazina na vitu vya thamani na kuongeza idadi ya wajane ndani yake. 26 Makuhani wake wameihalifu sheria yangu na kunajisi vitu vyangu vitakatifu, hawatofautishi kati ya vitu vitakatifu na vitu vya kawaida. Wanafundisha kuwa hakuna tofauti kati ya vitu vilivyo najisi na visivyo najisi, nao wanafumba macho yao katika kutunza Sabato zangu, hivyo katikati yao nimetiwa unajisi. 27 Maafisa wake walioko ndani yake ni kama mbwa mwitu wararuao mawindo yao, wanamwaga damu na kuua watu ili kupata faida ya udhalimu. 28 Manabii wake wanapaka chokaa matendo haya kwa maono ya uongo na utabiri wa udanganyifu. Wanasema, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo,’ wakati Bwana hajasema. 29 Watu wa nchi wanatoza kwa nguvu na kufanya unyangʼanyi, wanawatenda jeuri maskini na wahitaji na kuwaonea wageni, wakiwanyima haki.
30 “Nami nikatafuta mtu miongoni mwao, ambaye angejenga ukuta na kusimama mbele zangu mahali palipobomoka kwa ajili ya watu wa nchi ili nisije nikaiangamiza, lakini sikumwona mtu yeyote. 31 Hivyo nitaimwaga ghadhabu yangu juu yao na kuwateketeza kwa moto wa hasira yangu, nikiyaleta juu ya vichwa vyao yale yote waliyotenda, asema Bwana Mwenyezi.”