32
Maombolezo Kwa Ajili Ya Farao
Katika mwaka wa kumi na mbili, mwezi wa kumi na mbili, siku ya kwanza ya mwezi, neno la Bwana likanijia, kusema: “Mwanadamu, fanya maombolezo kwa ajili ya Farao mfalme wa Misri na umwambie:
“ ‘Wewe ni kama simba miongoni mwa mataifa,
wewe ni kama joka kubwa baharini,
unayevuruga maji kwa miguu yako
na kuchafua vijito.
“ ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo:
“ ‘Nikiwa pamoja na wingi mkubwa wa watu
nitautupa wavu wangu juu yako,
nao watakukokota katika wavu wangu.
Nitakutupa nchi kavu
na kukuvurumisha uwanjani.
Nitawafanya ndege wote wa angani watue juu yako
na wanyama wote wa nchi
watajishibisha nyama yako.
Nitatawanya nyama yako juu ya milima
na kujaza mabonde kwa mabaki yako.
Nitailowanisha nchi kwa damu yako inayotiririka
njia yote hadi milimani,
nayo mabonde yatajazwa na nyama yako.
Nitakapokuzimisha, nitafunika mbingu
na kuzitia nyota zake giza;
nitalifunika jua kwa wingu,
nao mwezi hautatoa nuru yake.
Mianga yote itoayo nuru angani
nitaitia giza juu yako;
nitaleta giza juu ya nchi yako,
asema Bwana Mwenyezi.
Nitaifadhaisha mioyo ya mataifa mengi
nitakapokuangamiza miongoni mwa mataifa,
nikikuleta uhamishoni miongoni mwa nchi
ambazo haujapata kuzijua.
10 Nitayafanya mataifa mengi wakustaajabie,
wafalme wao watatetemeka
kwa hofu kwa ajili yako
nitakapotikisa upanga wangu mbele yao.
Siku ya anguko lako
kila mmoja wao atatetemeka
kila dakika kwa ajili ya maisha yake.
11 “ ‘Kwa kuwa hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo:
“ ‘Upanga wa mfalme wa Babeli
utakuja dhidi yako.
12 Nitafanya makundi yako ya wajeuri kuanguka
kwa panga za watu mashujaa,
taifa katili kuliko mataifa yote.
Watakivunjavunja kiburi cha Misri,
nayo makundi yake yote
ya wajeuri yatashindwa.
13 Nitaangamiza mifugo yake yote
wanaojilisha kando ya maji mengi,
hayatavurugwa tena kwa mguu wa mwanadamu
wala kwato za mnyama
hazitayachafua tena.
14 Kisha nitafanya maji yake yatulie
na kufanya vijito vyake
vitiririke kama mafuta,
asema Bwana Mwenyezi.
15 Nitakapoifanya Misri kuwa ukiwa
na kuiondolea nchi kila kitu
kilichomo ndani yake,
nitakapowapiga wote waishio humo,
ndipo watakapojua kuwa
Mimi ndimi Bwana.’
16 “Hili ndilo ombolezo watakalomwimbia. Binti za mataifa wataliimba, kwa kuwa Misri na makundi yake yote ya wajeuri wataliimba, asema Bwana Mwenyezi.”
 
17 Katika mwaka wa kumi na mbili, mwezi wa kwanza, siku ya kumi na tano ya mwezi, neno la Bwana likanijia kusema: 18 “Mwanadamu, omboleza kwa ajili ya makundi ya wajeuri wa Misri na uwatupe kuzimu yeye na binti za mataifa yenye nguvu, waende huko pamoja nao washukao shimoni. 19 Je, ninyi mnamzidi nani kwa uzuri? Shukeni chini! Nanyi mkalazwe pamoja na hao wasiotahiriwa! 20 Wataanguka miongoni mwa wale waliouawa kwa upanga. Upanga umefutwa, mwache aburutwe mbali pamoja na hao wajeuri wake wote. 21 Kutoka kuzimu viongozi hodari watanena kuhusu Misri pamoja na wale walioungana nao, ‘Wameshuka chini, nao wamelala kimya pamoja na hao wasiotahiriwa, pamoja na wale waliouawa kwa upanga.’
22 “Ashuru yuko huko pamoja na jeshi lake lote, amezungukwa na makaburi ya watu wake wote waliouawa, wale wote walioanguka kwa upanga. 23 Makaburi yao yako kwenye kina cha chini cha shimo na jeshi lake limelala kulizunguka kaburi lake. Wote waliokuwa wameeneza hofu kuu katika nchi ya walio hai wameuawa, wameanguka kwa upanga.
24 “Elamu yuko huko, pamoja na makundi yake yote ya wajeuri wakiwa wamelizunguka kaburi lake. Wote wameuawa, wameanguka kwa upanga. Wote waliokuwa wameeneza hofu katika nchi ya walio hai walishuka kuzimu bila kutahiriwa. Wanaichukua aibu yao pamoja na wale washukao shimoni. 25 Kitanda kimetandikwa kwa ajili yake miongoni mwa waliouawa, pamoja na makundi yake yote ya wajeuri wakiwa wamelizunguka kaburi lake. Wote ni watu wasiotahiriwa, wameuawa kwa upanga. Kwa sababu vitisho vyao vilienea katika nchi ya walio hai, wameichukua aibu yao pamoja na wale washukao shimoni, nao wamewekwa miongoni mwa waliouawa.
26 “Mesheki na Tubali wako humo, pamoja na makundi yao ya wajeuri wakiwa wameyazunguka makaburi yao. Wote hawakutahiriwa, wameuawa kwa upanga kwa sababu walieneza vitisho vyao katika nchi ya walio hai. 27 Je, hawakulala na mashujaa wengine wasiotahiriwa waliouawa, ambao wameshuka kaburini wakiwa na silaha zao za vita, ambao panga zao ziliwekwa chini ya vichwa vyao na uovu wao juu ya mifupa yao? Adhabu kwa ajili ya dhambi zao ilikuwa juu ya mifupa yao, ingawa vitisho vya mashujaa hawa vilikuwa vimeenea hadi kwenye nchi ya walio hai.
28 “Wewe pia, ee Farao, utavunjwa nawe utalala miongoni mwa wasiotahiriwa, pamoja na wale waliouawa kwa upanga.
29 “Edomu yuko humo, wafalme wake wote na wakuu wake wote, ambao ijapokuwa wana nguvu, wamelazwa pamoja na wale waliouawa kwa upanga. Wamelala pamoja na wasiotahiriwa, pamoja na wale washukao shimoni.
30 “Wakuu wote wa kaskazini na Wasidoni wote wako huko, wameshuka chini pamoja na waliouawa kwa aibu ijapokuwa kuna vitisho vilivyosababishwa na nguvu zao. Wamelala bila kutahiriwa pamoja na wale waliouawa kwa upanga na kuchukua aibu yao pamoja na wale washukao chini shimoni.
31 “Farao, yeye pamoja na jeshi lake lote, atakapowaona atafarijiwa kwa ajili ya makundi yake yote ya wajeuri, wale waliouawa kwa upanga, asema Bwana Mwenyezi. 32 Ingawa nilimfanya Farao aeneze vitisho vyake katika nchi ya walio hai, Farao pamoja na makundi yake yote ya wajeuri watalazwa miongoni mwa wasiotahiriwa, pamoja na wale waliouawa kwa upanga, asema Bwana Mwenyezi.”