42
Vyumba Vya Makuhani
1 Ndipo yule mtu akaniongoza kuelekea kaskazini mpaka kwenye ua wa nje na kunileta mpaka kwenye vyumba vinavyoelekeana na ua wa Hekalu na kuelekeana na ukuta wa nje upande wa kaskazini. 2 Jengo ambalo mlango wake ulielekea kaskazini lilikuwa na urefu wa dhiraa mia moja na upana wa dhiraa hamsini. 3 Mbele ya zile dhiraa ishirini za ule ua wa ndani unaoelekeana na ile njia ya ua wa nje, kuliinuka vyumba virefu kimoja baada ya kingine vya ghorofa tatu. 4 Mbele ya hivi vyumba kulikuwa na njia ya ndani yenye upana wa dhiraa kumi na urefu wa dhiraa mia moja. Milango yake ilikuwa upande wa kaskazini. 5 Basi vyumba vya juu vilikuwa vyembamba zaidi, kwa kuwa ujia*Ujia ina maana ya njia ndani ya nyumba. ulichukua nafasi zaidi ndani yake kuliko katika vyumba vya sakafu ya chini na vya katikati ya jengo. 6 Vyumba katika ghorofa ya tatu havikuwa na nguzo, kama kumbi zilivyokuwa nazo, kwa hiyo eneo la sakafu ya vyumba vya juu lilikuwa ni dogo kuliko la sakafu ya chini na ya kati. 7 Kulikuwa na ukuta wa nje uliokuwa sambamba na vile vyumba na ukumbi wa nje, ulitokeza urefu wa dhiraa hamsini. 8 Wakati safu ya vyumba katika ua wa nje vilikuwa na urefu wa dhiraa hamsini, vile vyumba vilivyokuwa karibu zaidi na Hekalu vilikuwa na urefu wa dhiraa mia moja. 9 Vyumba vya chini vilikuwa na ingilio upande wa mashariki unapoingia kutoka ukumbi wa nje.
10 Upande wa kusini kufuata urefu wa ukuta wa ukumbi wa nje, unaopakana na ukumbi wa Hekalu na kuelekeana na ukuta wa nje, kulikuwa na vyumba 11 vyenye ujia unayopita mbele yake. Hivi vilifanana na vile vyumba vya upande wa kaskazini, vilikuwa na urefu na upana ulio sawa, mahali pa kutokea na vipimo vyake vilikuwa sawa. Kama ilivyokuwa milango ya upande wa kaskazini, 12 ndivyo ilivyokuwa milango ya vyumba vya upande wa kusini. Kulikuwa na ingilio kuanzia mwanzo wa njia ambao ulikuwa sambamba na ukuta wa pili uliokuwa upande wa mashariki, ambako ndiko kwa kuingia vyumbani.
13 Kisha akaniambia, “Vyumba vya upande wa kaskazini na vya upande wa kusini ambavyo vinaelekeana na ukumbi wa Hekalu ni vyumba vya makuhani, mahali ambapo wale makuhani ambao humkaribia Bwana watakula zile sadaka takatifu sana. Huko ndiko watakakoweka zile sadaka takatifu sana, yaani, sadaka za nafaka, sadaka za dhambi na sadaka za hatia, kwa kuwa mahali ni patakatifu. 14 Mara makuhani waingiapo mahali patakatifu, hawaruhusiwi kwenda kwenye ukumbi wa nje mpaka wayaache mavazi ambayo walivaa wakiwa wanahudumu, kwa kuwa hayo mavazi ni matakatifu. Inawapasa kuvaa mavazi mengine kabla hawajakaribia eneo lililo wazi kwa ajili ya watu.”
15 Alipomaliza kupima vile vilivyokuwa katika eneo la ndani la Hekalu, akanitoa nje kupitia lango la upande wa mashariki na kupima eneo lote linalozunguka: 16 Akapima upande wa mashariki kwa ule ufito wa kupimia, nao ulikuwa dhiraa 500†Dhiraa 500 ni sawa na mita 225. 17 Akapima upande wa kaskazini, nao ulikuwa dhiraa 500 kwa ufito ule wa kupimia. 18 Tena akapima upande wa kusini, nao ulikuwa dhiraa 500 kwa ufito ule wa kupimia. 19 Kisha akageukia upande wa magharibi na kuupima, ulikuwa dhiraa 500 kwa ufito ule wa kupimia. 20 Hivyo akapima eneo katika pande zote nne. Lilikuwa na ukuta kulizunguka wenye urefu wa dhiraa 500 na upana wa dhiraa 500, uliotenganisha mahali Patakatifu na eneo la watu wote.