5
Barua Ya Tatenai Kwa Dario
1 Ndipo nabii Hagai na nabii Zekaria mzao wa Ido, wakawatolea unabii Wayahudi waliokuwa Yuda na Yerusalemu kwa jina la Mungu wa Israeli, aliyekuwa pamoja nao. 2 Ndipo Zerubabeli mwana wa Shealtieli na Yeshua mwana wa Yosadaki wakaanza kujenga tena nyumba ya Mungu huko Yerusalemu. Nao manabii wa Mungu walikuwa pamoja nao, wakiwasaidia.
3 Wakati ule Tatenai mtawala wa ngʼambo ya mto Frati na Shethar-Bozenai na wenzao waliwaendea, wakawauliza, “Ni nani aliyewapa ruhusa ya kujenga tena Hekalu hili na kurudishia upya kama lilivyokuwa?” 4 Pia waliwauliza, “Je, majina ya watu wanaofanya ujenzi huu ni nani?” 5 Lakini jicho la Mungu wao lilikuwa likiwaangalia wazee wa Wayahudi, nao hawakuzuiliwa kujenga mpaka taarifa ikaandikwa kwa Dario na majibu yake kupokelewa.
6 Hii ni nakala ya barua ile Tatenai, mtawala wa ngʼambo ya mto Frati na Shethar-Bozenai na wenzao maafisa wa ngʼambo ya mto Frati waliyompelekea Mfalme Dario. 7 Taarifa waliyompelekea ilisomeka kama ifuatavyo:
Kwa Mfalme Dario:
Salamu kwa moyo mkunjufu.
8 Inampasa Mfalme ajue kwamba tulikwenda katika eneo la Yuda, kwenye Hekalu la Mungu mkuu. Watu wanalijenga kwa mawe makubwa na kuweka mbao kwenye kuta. Kazi inafanyika kwa bidii na inaendelea kwa haraka chini ya uongozi wao.
9 Tuliwauliza viongozi, “Ni nani aliyewapa ruhusa kujenga upya Hekalu hili na kurejeza hali ya jengo kama lilivyokuwa?” 10 Pia tuliwauliza majina yao, ili tukuandikie kukujulisha majina ya viongozi wao.
11 Hili ndilo jibu walilotupa:
“Sisi ni watumishi wa Mungu wa mbingu na nchi, nasi tunalijenga upya Hekalu ambalo lilijengwa miaka mingi iliyopita, lile ambalo mfalme mkuu wa Israeli alilijenga na kulikamilisha. 12 Lakini kwa sababu baba zetu walimkasirisha Mungu wa mbinguni, basi aliwatia mkononi mwa Nebukadneza, Mkaldayo, mfalme wa Babeli, ambaye aliliharibu Hekalu hili na kuwaondoa watu na kuwapeleka uhamishoni huko Babeli.
13 “Pamoja na hayo, katika mwaka wa kwanza wa kutawala Koreshi mfalme wa Babeli, Mfalme Koreshi alitoa amri ya kujengwa upya nyumba hii ya Mungu. 14 Yeye hata aliviondoa vyombo vya dhahabu na fedha vya nyumba ya Mungu, kutoka Hekalu la Babeli ambavyo Nebukadneza alikuwa amevichukua kutoka ndani ya Hekalu huko Yerusalemu na kuvileta katika Hekalu la Babeli.
“Vyombo hivyo Mfalme Koreshi alimkabidhi mtu aliyeitwa Sheshbaza, ambaye Koreshi alikuwa amemteua awe mtawala, 15 naye akamwambia, ‘Chukua vyombo hivi uende ukaviweke ndani ya Hekalu huko Yerusalemu. Nawe uijenge upya nyumba ya Mungu mahali pake.’ 16 Hivyo huyu Sheshbaza alikuja na kuweka misingi ya nyumba ya Mungu iliyoko Yerusalemu. Tangu siku hiyo hadi sasa imekuwa ikiendelea kujengwa lakini bado haijamalizika.”
17 Sasa kama ikimpendeza mfalme, uchunguzi na ufanyike katika kumbukumbu za maandishi ya ufalme mjini Babeli, kuona kama kweli Mfalme Koreshi alitoa amri ya kujenga upya nyumba ya Mungu katika Yerusalemu. Kisha tunaomba mfalme na atutumie uamuzi wake kuhusu jambo hili.