Habakuki
1
Neno alilopokea nabii Habakuki.
 
Lalamiko La Habakuki
Ee Bwana, hata lini nitakuomba msaada,
lakini wewe husikilizi?
Au kukulilia, “Udhalimu!”
Lakini hutaki kuokoa?
Kwa nini unanifanya nitazame dhuluma?
Kwa nini unavumilia makosa?
Uharibifu na udhalimu viko mbele yangu;
kuna mabishano na mapambano kwa wingi.
Kwa hiyo sheria imepotoshwa,
nayo haki haipo kabisa.
Waovu wanawazunguka wenye haki,
kwa hiyo haki imepotoshwa.
Jibu La Bwana
“Yatazame mataifa,
uangalie na ushangae kabisa.
Kwa sababu katika siku zako nitafanya kitu
ambacho hungeamini,
hata kama ungeambiwa.
Nitawainua Wakaldayo,
watu hao wakatili na wenye haraka,
ambao hupita dunia yote
kuteka mahali pa kuishi pasipo pao wenyewe.
Ni watu wanoogopwa na wanaotisha;
wenyewe ndio sheria yao,
na huinua heshima yao wenyewe.
Farasi wao ni wepesi kuliko chui,
na wakali kuliko mbwa mwitu wakati wa machweo.
Askari wapanda farasi wao huenda mbio;
waendesha farasi wao wanatoka mbali.
Wanaruka kasi kama tai ili kurarua;
wote wanakuja tayari kwa fujo.
Makundi yao ya wajeuri yanasonga mbele
kama upepo wa jangwani,
na kukusanya wafungwa
kama mchanga.
10 Wanawabeza wafalme,
na kuwadhihaki watawala.
Wanaicheka miji yote iliyozungushiwa maboma;
wanafanya malundo ya udongo na kuiteka hiyo miji.
11 Kisha wanapita kasi kama upepo na kusonga mbele:
watu wenye hatia, ambao nguvu zao ndio mungu wao.”
Lalamiko La Pili La Habakuki
12 Ee Bwana, je, wewe sio wa tangu milele?
Mungu wangu, Uliye Mtakatifu wangu, hatutakufa.
Ee Bwana, umewachagua wao ili watekeleze hukumu;
Ee Mwamba, umewaamuru watuadhibu.
13 Macho yako ni safi mno hata yasiweze kuutazama uovu,
wala huwezi kuvumilia makosa.
Kwa nini basi unawavumilia wadanganyifu?
Kwa nini unakuwa kimya wakati waovu
wanawameza wale wenye haki
kuliko wao wenyewe?
14 Umewafanya watu kama samaki baharini,
kama viumbe wa bahari wasio na mtawala.
15 Adui mwovu anawavuta wote kwa ndoana,
anawakamata katika wavu wake,
anawakusanya katika juya lake;
kwa hiyo anashangilia na anafurahi.
16 Kwa hiyo anatoa kafara kwa wavu wake,
na kuchoma uvumba kwa juya lake,
kwa kuwa kwa wavu wake anaishi kwa starehe,
na anafurahia chakula kizuri.
17 Je, aendelee kuwatoa walio katika wavu wake,
akiangamiza mataifa bila huruma?