14
Toba Iletayo Baraka
Rudi, ee Israeli, kwa Bwana Mungu wako.
Dhambi zako zimekuwa
ndilo anguko lako!
Chukueni maneno pamoja nanyi,
mkamrudie Bwana.
Mwambieni:
“Samehe dhambi zetu zote
na utupokee kwa neema,
ili tuweze kutoa matunda yetu
kama sadaka za mafahali.
Ashuru hawezi kutuokoa,
hatutapanda farasi wa vita.
Kamwe hatutasema tena ‘Miungu yetu’
kwa kile ambacho mikono yetu wenyewe imetengeneza,
kwa kuwa kwako wewe yatima hupata huruma.”
 
“Nitaponya ukaidi wao
na kuwapenda kwa hiari yangu,
kwa kuwa hasira yangu imeondoka kwao.
Nitakuwa kama umande kwa Israeli;
atachanua kama yungiyungi.
Kama mwerezi wa Lebanoni
atashusha mizizi yake chini;
matawi yake yatatanda.
Fahari yake itakuwa kama mti wa mzeituni,
harufu yake nzuri kama mwerezi wa Lebanoni.
Watu wataishi tena kwenye kivuli chake.
Atastawi kama nafaka.
Atachanua kama mzabibu,
nao umaarufu wake utakuwa
kama divai itokayo Lebanoni.
Ee Efraimu, nina shughuli gani tena na sanamu?
Nitamjibu na kumtunza.
Mimi ni kama msunobari wenye majani mabichi;
kuzaa kwako matunda kunatoka kwangu.”
 
Ni nani mwenye hekima? Atayatambua mambo haya.
Ni nani mwenye ufahamu? Huyu atayaelewa.
Njia za Bwana ni adili;
wenye haki huenda katika njia hizo,
lakini waasi watajikwaa ndani yake.