2
Mlima Wa Bwana
(Mika 4:1-3)
Hili ndilo aliloliona Isaya mwana wa Amozi kuhusu Yuda na Yerusalemu:
Katika siku za mwisho
mlima wa Hekalu la Bwana utaimarishwa
kama mlima mkuu miongoni mwa milima yote,
utainuliwa juu ya vilima,
na mataifa yote yatamiminika huko.
Mataifa mengi yatakuja na kusema,
“Njooni, twendeni mlimani mwa Bwana,
kwenye nyumba ya Mungu wa Yakobo.
Atatufundisha njia zake,
ili tuweze kuenenda katika mapito yake.”
Sheria itatoka Sayuni,
neno la Bwana litatoka Yerusalemu.
Atahukumu kati ya mataifa
na ataamua migogoro ya mataifa mengi.
Watafua panga zao ziwe majembe,
na mikuki yao kuwa miundu ya kukata matawi.
Taifa halitainua upanga dhidi ya taifa jingine,
wala hawatajifunza vita tena.
 
Njooni, enyi nyumba ya Yakobo,
tutembeeni katika nuru ya Bwana.
Siku Ya Bwana
Umewatelekeza watu wako,
nyumba ya Yakobo.
Wamejaa ushirikina utokao Mashariki,
wanapiga ramli kama Wafilisti
na wanashikana mikono na wapagani.
Nchi yao imejaa fedha na dhahabu,
hakuna mwisho wa hazina zao.
Nchi yao imejaa farasi,
hakuna mwisho wa magari yao.
Nchi yao imejaa sanamu,
wanasujudia kazi za mikono yao,
vitu vile vidole vyao vimevitengeneza.
Kwa hiyo mwanadamu atashushwa
na binadamu atanyenyekezwa:
usiwasamehe.
 
10 Ingieni kwenye miamba,
jificheni ardhini
kutokana na utisho wa Bwana
na utukufu wa enzi yake!
11 Macho ya mtu mwenye majivuno yatanyenyekezwa
na kiburi cha wanadamu kitashushwa,
Bwana peke yake ndiye atakayetukuzwa siku hiyo.
 
12 Bwana Mwenye Nguvu Zote anayo siku aliyoiweka akiba
kwa wote wenye kujivuna na wenye kiburi,
kwa wote wanaojikweza
(nao watanyenyekezwa),
13 kwa mierezi yote ya Lebanoni iliyo mirefu sana,
na mialoni yote ya Bashani,
14 kwa milima yote mirefu
na vilima vyote vilivyoinuka,
15 kwa kila mnara ulio mrefu sana
na kila ukuta wenye ngome,
16 kwa kila meli ya biashara,*Au: ya Tarshishi (ona pia 1Fal 10:22; 22:48; 2Nya 9:21; 20:36; Isa 60:9.)
na kila chombo cha baharini cha fahari.
17 Majivuno ya mwanadamu yatashushwa,
na kiburi cha wanadamu kitanyenyekezwa,
Bwana peke yake ndiye atatukuzwa siku hiyo,
18 nazo sanamu zitatoweka kabisa.
 
19 Watu watakimbilia kwenye mapango ndani ya miamba,
na kwenye mahandaki ardhini
kutokana na utisho wa Bwana
na utukufu wa enzi yake,
ainukapo kuitikisa dunia.
20 Siku ile, watu watawatupia
panya na popo
sanamu zao za fedha na za dhahabu,
walizozitengeneza ili waziabudu.
21 Watakimbilia kwenye mapango miambani
na kwenye nyufa za miamba
kutokana na utisho wa Bwana
na utukufu wa enzi yake,
ainukapo kuitikisa dunia.
 
22 Acheni kumtumainia mwanadamu,
ambaye hana kitu ila pumzi katika pua zake.
Yeye ana thamani gani?

*2:16 Au: ya Tarshishi (ona pia 1Fal 10:22; 22:48; 2Nya 9:21; 20:36; Isa 60:9.)