25
Miaka Sabini Ya Kuwa Mateka
Neno likamjia Yeremia kuhusu watu wote wa Yuda, katika mwaka wa nne wa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda, ambao ulikuwa mwaka wa kwanza wa utawala wa Nebukadneza mfalme wa Babeli. Hivyo nabii Yeremia akawaambia watu wote wa Yuda na wale wote waishio Yerusalemu: Kwa miaka ishirini na mitatu, kuanzia mwaka wa kumi na tatu wa utawala wa Yosia mwana wa Amoni mfalme wa Yuda, hadi siku hii ya leo, neno la Bwana limekuwa likinijia, nami nimesema nanyi mara kwa mara, lakini hamkusikiliza.
Ingawa Bwana amewatuma watumishi wake wote hao manabii kwenu mara kwa mara, hamkusikiliza wala hamkujali. Walisema, “Geukeni sasa, kila mmoja wenu kutoka njia yake mbaya na matendo yake maovu, ndipo mtaweza kukaa katika nchi ambayo Bwana aliwapa ninyi na baba zenu milele. Msiifuate miungu mingine ili kuitumikia na kuiabudu. Msinikasirishe kwa vitu ambavyo mmevitengeneza kwa mikono yenu.”
“Lakini ninyi hamkunisikiliza mimi, tena mkanikasirisha kwa vitu mlivyovitengeneza kwa mikono yenu, nanyi mmejiletea madhara juu yenu wenyewe,” asema Bwana.
Kwa hiyo Bwana Mwenye Nguvu Zote asema hivi: “Kwa sababu hamkuyasikiliza maneno yangu, nitayaita mataifa yote ya kaskazini na mtumishi wangu Nebukadneza mfalme wa Babeli,” asema Bwana. “Nitawaleta waishambulie nchi hii na wakazi wake wote, na dhidi ya mataifa yote yanayowazunguka. Nitawaangamiza kabisa na kuwafanya kitu cha kuchukiwa na kudharauliwa, na kuwa magofu daima. 10 Nitawaondolea sauti ya shangwe na furaha, sauti ya bibi na bwana arusi, sauti ya mawe ya kusagia, na mwanga wa taa. 11 Nchi hii yote itakuwa ukiwa na isiyofaa kitu, nayo mataifa haya yatamtumikia mfalme wa Babeli kwa miaka sabini.”
12 “Lakini miaka sabini itakapotimia, nitamwadhibu mfalme wa Babeli na taifa lake na nchi ya Wakaldayo kwa ajili ya hatia yao,” asema Bwana. “Nitaifanya kuwa ukiwa milele. 13 Nitaleta juu ya nchi hiyo mambo yote niliyosema dhidi yake, yote yaliyoandikwa katika kitabu hiki, na kutolewa unabii na Yeremia dhidi ya mataifa yote. 14 Wao wenyewe watakuwa watumwa wa mataifa mengi na wafalme wakuu. Nitawalipizia sawasawa na matendo yao na kazi ya mikono yao.”
Kikombe Cha Ghadhabu Ya Mungu
15 Hili ndilo Bwana, Mungu wa Israeli, aliloniambia: “Chukua kutoka mkononi mwangu kikombe hiki kilichojaa divai ya ghadhabu yangu, na kuyanywesha mataifa yote ambayo ninakutuma kwao. 16 Watakapoinywa, watapepesuka na kukasirika sana kwa sababu ya upanga nitakaoupeleka katikati yao.”
17 Hivyo nikakichukua kikombe kutoka mkononi mwa Bwana, na kuyafanya mataifa yote aliyonituma kwao kukinywa: 18 Yaani Yerusalemu na miji ya Yuda, wafalme wake na maafisa wake, kuwafanya magofu na kuwa kitu cha kuchukiza, cha dhihaka na laana, kama walivyo leo; 19 pia Farao mfalme wa Misri, watumishi wake, maafisa wake na watu wake wote, 20 pia wageni wote walioko huko; wafalme wote wa nchi ya Usi; wafalme wote wa Wafilisti (wale wa Ashkeloni, Gaza, Ekroni na watu walioachwa huko Ashdodi); 21 Edomu, Moabu na Amoni; 22 wafalme wote wa Tiro na Sidoni; wafalme wa nchi za pwani ngʼambo ya bahari; 23 Dedani, Tema, Buzi na wote walio maeneo ya mbali; 24 wafalme wote wa Arabuni na wafalme wote wa watu wageni wanaoishi katika jangwa; 25 wafalme wote wa Zimri, Elamu na Umedi; 26 na wafalme wote wa pande za kaskazini, wa karibu na wa mbali, mmoja baada ya mwingine; yaani falme zote juu ya uso wa dunia. Baada ya hao wote, mfalme wa Sheshaki*Sheshaki ni Babeli kwa fumbo. atakunywa pia.
27 “Kisha uwaambie, ‘Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: Kunyweni, mlewe na mtapike; angukeni, wala msiinuke tena kwa sababu ya upanga nitakaotuma miongoni mwenu.’ 28 Lakini kama wakikataa kupokea kikombe kutoka mikononi mwako na kunywa, waambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote: Ni lazima mnywe! 29 Tazama, nimeanza kuleta maafa juu ya mji ulio na Jina langu, na je, kweli ninyi mtaepuka kuadhibiwa? Hamwezi kuepuka kuadhibiwa, kwa maana nitaleta vita juu ya wote waishio duniani, asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.’
30 “Basi sasa toa unabii kwa maneno haya yote dhidi yao, uwaambie:
“ ‘Bwana atanguruma kutoka juu;
atatoa sauti ya ngurumo
kutoka makao yake matakatifu
na kunguruma kwa nguvu sana
dhidi ya nchi yake.
Atapiga kelele kama wao wakanyagao zabibu,
atapiga kelele dhidi ya wote waishio duniani.
31 Ghasia zitasikika hadi miisho ya dunia,
kwa maana Bwana ataleta mashtaka dhidi ya mataifa;
ataleta hukumu juu ya wanadamu wote
na kuwaua waovu wote,’ ”
asema Bwana.
32 Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote asemalo:
“Tazama! Maafa yanaenea
kutoka taifa moja hadi jingine;
tufani kubwa inainuka
kutoka miisho ya dunia.”
33 Wakati huo, hao waliouawa na Bwana watatapakaa kila mahali, kuanzia mwisho mmoja wa dunia hadi mwisho mwingine. Hawataombolezewa wala kukusanywa au kuzikwa, lakini watakuwa kama mavi yaliyoenea juu ya ardhi.
34 Lieni na kuomboleza, enyi wachungaji,
mgaagae mavumbini,
ninyi viongozi wa kundi.
Kwa maana wakati wenu wa kuchinjwa umewadia;
mtaanguka na kuvunjavunjwa
kama vyombo vizuri vya udongo.
35 Wachungaji hawatakuwa na mahali pa kukimbilia,
viongozi wa kundi hawatapata mahali pa kutorokea.
36 Sikia kilio cha wachungaji, maombolezo ya viongozi wa kundi,
kwa maana Bwana anayaharibu malisho yao.
37 Makao yao ya amani yataharibiwa
kwa sababu ya hasira kali ya Bwana.
38 Kama simba ataacha pango lake,
nchi yao itakuwa ukiwa
kwa sababu ya upanga wa mdhalimu,
na kwa sababu ya hasira kali ya Bwana Mungu.

*25:26 Sheshaki ni Babeli kwa fumbo.