19
Hotuba Ya Sita Ya Ayubu
Ayubu Anajibu: Najua Mkombozi Wangu Yu Hai
Ndipo Ayubu akajibu:
“Je, mtaendelea kunitesa mpaka lini,
na kuniponda kwa maneno yenu?
Mara kumi hizi mmenishutumu;
bila aibu mnanishambulia.
Kama ni kweli nimepotoka,
kosa langu ninabaki kuhusika nalo mwenyewe.
Kama kweli mngejitukuza wenyewe juu yangu,
na kutumia unyonge wangu dhidi yangu,
basi jueni kuwa Mungu amenitendea yaliyo mabaya,
naye amekokota wavu wake kunizunguka.
 
“Ingawa ninalia, ‘Nimetendewa mabaya!’ sipati jibu;
ingawa ninaomba msaada, hakuna haki.
Yeye ameizuia njia yangu hivyo siwezi kupita;
ameyafunika mapito yangu na giza.
Amenivua heshima yangu,
na kuniondolea taji kichwani pangu.
10 Amenibomoa kila upande hadi nimeisha;
amelingʼoa tegemeo langu kama mti.
11 Hasira yake imewaka juu yangu;
amenihesabu kuwa miongoni mwa adui zake.
12 Majeshi yake yananisogelea kwa nguvu;
yamenizingira,
yamepiga kambi kulizunguka hema langu.
 
13 “Amewatenga ndugu zangu mbali nami;
wale tunaojuana nao wamefarakana nami kabisa.
14 Watu wa jamaa yangu wamekwenda mbali;
rafiki zangu wamenisahau.
15 Wageni wangu na watumishi wangu wa kike wananiona kama mgeni;
wananitazama kama mgeni.
16 Namwita mtumishi wangu, wala haitiki,
ingawa namwomba kwa kinywa changu mwenyewe.
17 Pumzi ya kinywa changu ni kinyaa kwa mke wangu;
nimekuwa chukizo mno kwa ndugu zangu mwenyewe.
18 Hata watoto wadogo hunidhihaki;
ninapojitokeza, hunifanyia mzaha.
19 Rafiki zangu wa moyoni wote wananichukia kabisa;
wale niwapendao wamekuwa kinyume nami.
20 Mimi nimebaki mifupa na ngozi tu;
nimeponea nikiwa karibu kufa.
 
21 “Nihurumieni, rafiki zangu, kuweni na huruma,
kwa kuwa mkono wa Mungu umenipiga.
22 Kwa nini mnanifuatia kama Mungu afanyavyo?
Hamtosheki kamwe na mwili wangu?
 
23 “Laiti maneno yangu yangewekwa kwenye kumbukumbu,
laiti kwamba yangeandikwa kwenye kitabu,
24 kwamba yangechorwa kwenye risasi kwa kifaa cha chuma,
au kuyachonga juu ya mwamba milele!
25 Ninajua kwamba Mkombozi*Au: Mtetezi. wangu yu hai,
naye kwamba mwishoni atasimama juu ya nchi.
26 Nami baada ya ngozi yangu kuharibiwa,
bado nikiwa na mwili huu nitamwona Mungu;
27 mimi nitamwona kwa macho yangu mwenyewe:
mimi, wala si mwingine.
Tazama jinsi moyo wangu unavyomtamani sana!
 
28 “Kama mkisema, ‘Tazama tutakavyomwinda,
maadamu mzizi wa tatizo uko ndani yake,’
29 ninyi wenyewe uogopeni upanga,
kwa kuwa ghadhabu italeta adhabu kwa upanga,
nanyi ndipo mtakapojua kwamba kuna hukumu.”

*19:25 Au: Mtetezi.