25
Bildadi Anasema: Mwanadamu Awezaje Kuwa Mwadilifu Mbele Za Mungu? 
  1 Ndipo Bildadi Mshuhi akajibu:   
 2 “Mamlaka na kuheshimiwa ni vyake Mungu;  
yeye huthibitisha amani katika mbingu juu.   
 3 Je, majeshi yake yaweza kuhesabika?  
Ni nani asiyeangaziwa na nuru yake?   
 4 Mtu awezaje kuwa mwadilifu mbele za Mungu?  
Awezaje mtu aliyezaliwa na mwanamke kuwa safi?   
 5 Ikiwa hata mwezi sio mwangavu  
nazo nyota si safi machoni pake,   
 6 sembuse mtu ambaye ni funza:  
mwanadamu ambaye ni buu tu!”