Maombolezo
1
* Sura hii imetungwa kila beti likianzia, na pia kila mstari katika lile beti, na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22. Tazama jinsi mji ulivyoachwa ukiwa,
mji ambao zamani ulikuwa umejaa watu!
Jinsi ambavyo umekuwa kama mama mjane,
ambaye wakati fulani alikuwa maarufu miongoni mwa mataifa!
Yule ambaye alikuwa malkia miongoni mwa majimbo
sasa amekuwa mtumwa.
 
Kwa uchungu, hulia sana usiku,
machozi yapo kwenye mashavu yake.
Miongoni mwa wapenzi wake wote
hakuna yeyote wa kumfariji.
Rafiki zake wote wamemsaliti,
wamekuwa adui zake.
 
Baada ya mateso na kufanyishwa kazi kikatili,
Yuda amekwenda uhamishoni.
Anakaa miongoni mwa mataifa,
hapati mahali pa kupumzika.
Wote ambao wanamsaka wamemkamata
katikati ya dhiki yake.
 
Barabara zielekeazo Sayuni zaomboleza,
kwa kuwa hakuna yeyote anayekuja
kwenye sikukuu zake zilizoamriwa.
Malango yake yote yamekuwa ukiwa,
makuhani wake wanalia kwa uchungu,
wanawali wake wanahuzunika,
naye yuko katika uchungu wa maumivu makuu.
 
Adui zake wamekuwa mabwana zake,
watesi wake wana raha.
Bwana amemletea huzuni
kwa sababu ya dhambi zake nyingi.
Watoto wake wamekwenda uhamishoni,
mateka mbele ya adui.
 
Fahari yote imeondoka
kutoka kwa Binti Sayuni.
Wakuu wake wako kama ayala
ambaye hapati malisho,
katika udhaifu wamekimbia
mbele ya anayewasaka.
 
Katika siku za mateso yake na kutangatanga,
Yerusalemu hukumbuka hazina zote
ambazo zilikuwa zake siku za kale.
Wakati watu wake walipoanguka katika mikono ya adui,
hapakuwepo na yeyote wa kumsaidia.
Watesi wake walimtazama
na kumcheka katika maangamizi yake.
 
Yerusalemu ametenda dhambi sana
kwa hiyo amekuwa najisi.
Wote waliomheshimu wanamdharau,
kwa maana wameuona uchi wake.
Yeye mwenyewe anapiga kite
na kugeukia mbali.
 
Uchafu wake umegandamana na nguo zake;
hakuwaza juu ya maisha yake ya baadaye.
Anguko lake lilikuwa la kushangaza,
hapakuwepo na yeyote wa kumfariji.
“Tazama, Ee Bwana, teso langu,
kwa maana adui ameshinda.”
 
10 Adui ametia mikono
juu ya hazina zake zote,
aliona mataifa ya kipagani
wakiingia mahali patakatifu pake,
wale uliowakataza kuingia
kwenye kusanyiko lako.
 
11 Watu wake wote wanalia kwa uchungu
watafutapo chakula;
wanabadilisha hazina zao kwa chakula
ili waweze kuendelea kuishi.
“Tazama, Ee Bwana, ufikiri,
kwa maana nimedharauliwa.”
 
12 “Je, si kitu kwenu, ninyi nyote mpitao kando?
Angalieni kote mwone.
Je, kuna maumivu kama maumivu yangu
yale yaliyotiwa juu yangu,
yale Bwana aliyoyaleta juu yangu
katika siku ya hasira yake kali?
 
13 “Kutoka juu alipeleka moto,
akaushusha katika mifupa yangu.
Aliitandia wavu miguu yangu
na akanirudisha nyuma.
Akanifanya mkiwa,
na mdhaifu mchana kutwa.
 
14 “Dhambi zangu zimefungwa kwenye nira,
kwa mikono yake zilifumwa pamoja.
Zimefika shingoni mwangu
na Bwana ameziondoa nguvu zangu.
Amenitia mikononi mwa wale
ambao siwezi kushindana nao.
 
15 “Bwana amewakataa wapiganaji wa vita
wote walio kati yangu,
ameagiza jeshi dhidi yangu
kuwaponda vijana wangu wa kiume.
Katika shinikizo lake la divai Bwana amemkanyaga
Bikira Binti Yuda.
 
16 “Hii ndiyo sababu ninalia
na macho yangu yanafurika machozi.
Hakuna yeyote aliye karibu kunifariji,
hakuna yeyote wa kuhuisha roho yangu.
Watoto wangu ni wakiwa
kwa sababu adui ameshinda.”
 
17 Sayuni ananyoosha mikono yake,
lakini hakuna yeyote wa kumfariji.
Bwana ametoa amri kwa ajili ya Yakobo
kwamba majirani zake wawe adui zake;
Yerusalemu umekuwa
kitu najisi miongoni mwao.
 
18 Bwana ni mwenye haki,
hata hivyo niliasi dhidi ya amri yake.
Sikilizeni, enyi mataifa yote,
tazameni maumivu yangu.
Wavulana wangu na wasichana wangu
wamekwenda uhamishoni.
 
19 “Niliita washirika wangu
lakini walinisaliti.
Makuhani wangu na wazee wangu
waliangamia mjini
walipokuwa wakitafuta chakula
ili waweze kuishi.
 
20 “Angalia, Ee Bwana, jinsi nilivyo katika dhiki!
Nina maumivu makali ndani yangu,
nami ninahangaika moyoni mwangu,
kwa kuwa nimekuwa mwasi sana.
Huko nje, upanga unaua watu,
ndani, kipo kifo tu.
 
21 “Watu wamesikia ninavyolia kwa uchungu,
lakini hakuna yeyote wa kunifariji.
Adui zangu wote wamesikia juu ya dhiki yangu,
wanafurahia lile ulilolitenda.
Naomba uilete siku uliyoitangaza
ili wawe kama mimi.
 
22 “Uovu wao wote na uje mbele zako;
uwashughulikie wao
kama vile ulivyonishughulikia mimi
kwa sababu ya dhambi zangu zote.
Kulia kwangu kwa uchungu ni kwingi
na moyo wangu umedhoofika.”

*^ Sura hii imetungwa kila beti likianzia, na pia kila mstari katika lile beti, na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22.