20
Mfano Wa Wafanyakazi Katika Shamba La Mizabibu
1 “Kwa maana Ufalme wa Mbinguni unafanana na mtu mwenye shamba aliyetoka alfajiri ili kwenda kuajiri vibarua kufanya kazi katika shamba lake la mizabibu. 2 Baada ya kukubaliana na hao vibarua kuwalipa ujira wa dinari*Dinari moja ilikuwa kama mshahara wa kibarua wa siku moja.moja kwa siku, akawapeleka kwenye shamba lake la mizabibu.
3 “Mnamo saa tatu akatoka tena, akawakuta wengine wamesimama sokoni bila kazi. 4 Akawaambia, ‘Ninyi nanyi nendeni mkafanye kazi katika shamba langu la mizabibu, nami nitawalipa chochote kilicho haki yenu.’ 5 Kwa hiyo wakaenda.
“Akatoka tena mnamo saa sita na pia saa tisa akafanya vivyo hivyo. 6 Mnamo saa kumi na moja akatoka tena akawakuta wengine bado wamesimama bila kazi. Akawauliza, ‘Kwa nini mmesimama hapa kutwa nzima pasipo kufanya kazi?’
7 “Wakamjibu, ‘Ni kwa sababu hakuna yeyote aliyetuajiri.’
“Akawaambia, ‘Ninyi nanyi nendeni mkafanye kazi katika shamba langu la mizabibu.’
8 “Ilipofika jioni, yule mwenye shamba la mizabibu akamwambia msimamizi, ‘Waite hao vibarua na uwalipe ujira wao, ukianzia na wale walioajiriwa mwisho na kuishia na wale walioajiriwa kwanza.’
9 “Wale vibarua walioajiriwa mnamo saa kumi na moja, wakaja na kila mmoja wao akapokea dinari moja. 10 Hivyo wale walioajiriwa kwanza walipofika, walidhani watalipwa zaidi. Lakini kila mmoja wao pia alipokea dinari moja. 11 Walipoipokea, wakaanza kulalamika dhidi ya yule mwenye shamba, 12 wakisema, ‘Hawa watu walioajiriwa mwisho wamefanya kazi kwa muda wa saa moja tu, nawe umewafanya sawa na sisi ambao tumestahimili taabu na joto lote la mchana kutwa?’
13 “Yule mwenye shamba akamjibu mmoja wao, ‘Rafiki, sijakudhulumu. Je, hukukubaliana nami kwa ujira wa kawaida wa dinari moja? 14 Chukua ujira wako na uende. Mimi nimeamua kumlipa huyu mtu aliyeajiriwa mwisho kama nilivyokupa wewe. 15 Je, sina haki yangu kufanya kile nitakacho na mali yangu mwenyewe? Au unaona wivu kwa kuwa nimekuwa mkarimu?’
16 “Vivyo hivyo, wa mwisho watakuwa wa kwanza, na wa kwanza watakuwa wa mwisho.”
Yesu Atabiri Tena Kuhusu Kifo Chake
(Marko 10:32-34; Luka 18:31-34)
17 Basi Yesu alipokuwa anapanda kwenda Yerusalemu, aliwachukua kando wale wanafunzi wake kumi na wawili na kuwaambia, 18 “Tunapanda kwenda Yerusalemu, na Mwana wa Adamu atatiwa mikononi mwa viongozi wa makuhani na walimu wa sheria. Nao watamhukumu kifo 19 na kumtia mikononi mwa watu wa Mataifa ili wamdhihaki na kumpiga mijeledi na kumsulubisha msalabani. Naye atafufuliwa siku ya tatu!”
Ombi La Mama Yake Yakobo Na Yohana
(Marko 10:35-45)
20 Kisha mama yao wana wa Zebedayo akamjia Yesu pamoja na wanawe, naye akapiga magoti mbele yake, akamwomba Yesu amfanyie jambo fulani.
21 Yesu akamuuliza, “Unataka nini?” Akajibu, “Tafadhali, wajalie wanangu hawa ili mmoja aketi upande wako wa kuume, na mwingine upande wako wa kushoto katika Ufalme wako.”
22 Yesu akawaambia, “Ninyi hamjui mnaloliomba. Je, mnaweza kukinywea kikombe nitakachonywea mimi?”
Wakajibu, “Tunaweza.”
23 Yesu akawaambia, “Kwa kweli kikombe changu mtakinywea, lakini kuketi upande wangu wa kuume au wa kushoto si langu mimi kuwapa. Nafasi hizo ni za wale ambao wameandaliwa na Baba yangu.”
24 Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia haya, waliwakasirikia hao ndugu wawili. 25 Lakini Yesu akawaita wote pamoja na kuwaambia, “Mnafahamu kuwa watawala wa watu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, nao wenye vyeo huonyesha mamlaka yao. 26 Isiwe hivyo kwenu. Badala yake, yeyote anayetaka kuwa mkuu miongoni mwenu hana budi kuwa mtumishi wenu, 27 naye anayetaka kuwa wa kwanza miongoni mwenu hana budi kuwa mtumwa wenu: 28 kama vile ambavyo Mwana wa Adamu hakuja ili kutumikiwa, bali kutumika na kuutoa uhai wake uwe fidia kwa ajili ya wengi.”
Yesu Awaponya Vipofu Wawili
(Marko 10:46-52; Luka 18:35-43)
29 Yesu na wanafunzi wake walipokuwa wakiondoka Yeriko, umati mkubwa wa watu ulimfuata. 30 Vipofu wawili walikuwa wameketi kando ya barabara. Waliposikia kwamba Yesu alikuwa anapita, wakapiga kelele wakisema, “Bwana, Mwana wa Daudi, tuhurumie!”
31 Ule umati wa watu ukawakemea na kuwaambia wanyamaze, lakini wao wakazidi kupaza sauti, wakisema, “Bwana, Mwana wa Daudi, tuhurumie.”
32 Yesu akasimama na kuwaita, akawauliza, “Mnataka niwafanyie nini?”
33 Wakamjibu, “Bwana, tunataka kuona.”
34 Yesu akawahurumia na kuwagusa macho yao. Mara macho yao yakapata kuona, nao wakamfuata.