22
Mfano Wa Karamu Ya Arusi
(Luka 14:15-24)
1 Yesu akasema nao tena kwa mifano, akawaambia, 2 “Ufalme wa Mbinguni unaweza kufananishwa na mfalme mmoja aliyemwandalia mwanawe karamu ya arusi. 3 Akawatuma watumishi wake kuwaita wale waliokuwa wamealikwa karamuni, lakini wakakataa kuja.
4 “Kisha akawatuma watumishi wengine akisema, ‘Waambieni wale walioalikwa kwamba nimeandaa chakula. Nimekwisha kuchinja mafahali wangu na vinono, karamu iko tayari. Karibuni kwa karamu ya arusi.’
5 “Lakini hawakuzingatia, wakaenda zao: huyu shambani mwake na mwingine kwenye biashara zake. 6 Wengine wao wakawakamata wale watumishi wake, wakawatesa na kuwaua. 7 Yule mfalme akakasirika sana, akapeleka jeshi lake likawaangamiza wale wauaji na kuuteketeza mji wao kwa moto.
8 “Kisha akawaambia watumishi wake, ‘Karamu ya arusi imeshakuwa tayari, lakini wale niliowaalika hawakustahili kuja. 9 Kwa hiyo nendeni katika njia panda mkamwalike karamuni yeyote mtakayemwona.’ 10 Wale watumishi wakaenda barabarani, wakawakusanya watu wote waliowaona, wema na wabaya. Ukumbi wa arusi ukajaa wageni.
11 “Lakini mfalme alipoingia ndani ili kuwaona wageni, akamwona mle mtu mmoja ambaye hakuwa amevaa vazi la arusi. 12 Mfalme akamuuliza, ‘Rafiki, uliingiaje humu bila vazi la arusi?’ Yule mtu hakuwa na la kusema.
13 “Ndipo mfalme akawaambia watumishi wake, ‘Mfungeni mikono na miguu mkamtupe nje, kwenye giza. Huko kutakuwa na kilio na kusaga meno.’
14 “Kwa maana walioitwa ni wengi, lakini walioteuliwa ni wachache.”
Kulipa Kodi Kwa Kaisari
(Marko 12:13-17; Luka 20:20-26)
15 Ndipo Mafarisayo wakatoka nje wakaandaa mpango wa kumtega Yesu katika maneno yake. 16 Wakatuma wanafunzi wao kwake pamoja na Maherode. Nao wakasema, “Mwalimu, tunajua kwamba wewe ni mtu mwadilifu na unafundisha njia ya Mungu katika kweli bila kuyumbishwa na mtu wala kuonyesha upendeleo. 17 Tuambie basi, wewe unaonaje? Je, ni halali kulipa kodi kwa Kaisari, au la?”
18 Lakini Yesu, akijua makusudi yao mabaya, akawaambia, “Enyi wanafiki, kwa nini mnajaribu kunitega? 19 Nionyesheni hiyo sarafu inayotumika kwa kulipia kodi.” Wakamletea dinari. 20 Naye akawauliza, “Sura hii ni ya nani? Na maandishi haya ni ya nani?”
21 Wakamjibu, “Ni vya Kaisari.”
Basi Yesu akawaambia, “Mpeni Kaisari kilicho cha Kaisari, naye Mungu mpeni kilicho cha Mungu.”
22 Waliposikia hili, wakashangaa. Hivyo wakamwacha, wakaenda zao.
Ndoa Na Ufufuo
(Marko 12:18-27; Luka 20:27-40)
23 Siku hiyo hiyo Masadukayo, wale wasemao kwamba hakuna ufufuo wa wafu, wakamjia Yesu na kumuuliza swali, wakisema, 24 “Mwalimu, Mose alisema, ‘Kama mtu akifa bila kuwa na watoto, ndugu yake inampasa amwoe huyo mjane ili ampatie watoto huyo nduguye aliyekufa.’ 25 Basi palikuwa na ndugu saba miongoni mwetu. Yule wa kwanza akaoa mke, naye akafa, na kwa kuwa hakuwa na watoto, akamwachia nduguye yule mjane. 26 Ikatokea vivyo hivyo kwa yule ndugu wa pili, na wa tatu, hadi wote saba. 27 Hatimaye, yule mwanamke naye akafa. 28 Sasa basi, siku ya ufufuo, yeye atakuwa mke wa nani miongoni mwa wale ndugu saba, kwa kuwa wote walikuwa wamemwoa huyo mwanamke?”
29 Yesu akawajibu, “Mwapotoka kwa sababu hamjui Maandiko wala uweza wa Mungu. 30 Wakati wa ufufuo, watu hawataoa wala kuolewa, bali watakuwa kama malaika wa mbinguni. 31 Lakini kuhusu ufufuo wa wafu, hamjasoma kile Mungu alichowaambia, kwamba, 32 ‘Mimi ni Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaki, na Mungu wa Yakobo’? Yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai.”
33 Ule umati wa watu uliposikia hayo, ulishangaa sana kwa mafundisho yake.
Amri Kuu Kuliko Zote
(Marko 12:28-34; Luka 10:25-28)
34 Mafarisayo waliposikia kwamba Yesu alikuwa amewanyamazisha Masadukayo, Mafarisayo wakakusanyika pamoja. 35 Mmoja wao, mtaalamu wa sheria, akamuuliza swali ili kumjaribu, akisema, 36 “Mwalimu, ni amri ipi katika Sheria iliyo kuu kuliko zote?”
37 Yesu akamjibu, “ ‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote na kwa akili zako zote.’ 38 Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. 39 Nayo ya pili ni kama hiyo, nayo ni hii: ‘Mpende jirani yako kama nafsi yako.’ 40 Amri hizi mbili ndizo msingi wa Sheria na Manabii.”
Swali Kuhusu Mwana Wa Daudi
(Marko 12:35-37; Luka 20:41-44)
41 Wakati Mafarisayo walikuwa wamekusanyika pamoja, Yesu akawauliza, 42 “Mnaonaje kuhusu Kristo?*Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta.Yeye ni mwana wa nani?”
Wakamjibu, “Yeye ni mwana wa Daudi.”
43 Akawaambia, “Inakuwaje basi kwamba Daudi, akinena kwa kuongozwa na Roho, anamwita Kristo ‘Bwana’? Kwa maana asema,
44 “ ‘Bwana alimwambia Bwana wangu:
“Keti mkono wangu wa kuume,
hadi nitakapowaweka adui zako
chini ya miguu yako.” ’
45 Kama basi Daudi anamwita yeye ‘Bwana,’ awezaje kuwa mwanawe?” 46 Hakuna mtu aliyeweza kumjibu Yesu neno. Tena tangu siku hiyo hakuna aliyethubutu kumuuliza tena maswali.