24
Kubomolewa Kwa Hekalu Kwatabiriwa
(Marko 13:1-2; Luka 21:5-6)
1 Yesu akatoka Hekaluni na alipokuwa akienda zake, wanafunzi wake wakamwendea ili kumwonyesha majengo ya Hekalu. 2 Ndipo Yesu akawauliza, “Je, mnayaona haya yote? Amin, nawaambia, hakuna hata jiwe moja hapa litakalobaki juu ya jingine, bali kila moja litabomolewa.”
Ishara Za Nyakati Za Mwisho
(Marko 13:3-23; Luka 21:7-24)
3 Yesu alipokuwa ameketi kwenye Mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake wakamjia faraghani, wakamuuliza, “Tuambie, mambo haya yatatukia lini, nayo dalili ya kuja kwako na ya mwisho wa dunia ni gani?”
4 Yesu akawajibu, “Jihadharini, mtu yeyote asiwadanganye. 5 Kwa maana wengi watakuja kwa Jina langu, wakidai, ‘Mimi ndiye Kristo,’*Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta.nao watawadanganya wengi. 6 Mtasikia habari za vita na matetesi ya vita. Angalieni msitishike, kwa maana haya hayana budi kutukia. Lakini ule mwisho bado. 7 Taifa litainuka dhidi ya taifa, na ufalme dhidi ya ufalme. Kutakuwa na njaa na mitetemeko ya ardhi sehemu mbalimbali. 8 Haya yote yatakuwa ndio mwanzo wa utungu.
9 “Ndipo mtasalitiwa, ili mteswe na kuuawa, nanyi mtachukiwa na mataifa yote kwa ajili yangu. 10 Wakati huo, wengi wataacha imani yao, nao watasalitiana kila mmoja na mwenzake na kuchukiana. 11 Watatokea manabii wengi wa uongo, nao watawadanganya watu wengi. 12 Kwa sababu ya kuongezeka kwa uovu upendo wa watu wengi utapoa, 13 lakini yule atakayevumilia hadi mwisho ataokolewa. 14 Injili ya Ufalme itahubiriwa ulimwenguni kote kuwa ushuhuda kwa mataifa yote. Ndipo mwisho utakapokuja.
15 “Hivyo mtakapoona lile ‘chukizo la uharibifu’ lililonenwa na nabii Danieli limesimama mahali patakatifu (asomaye na afahamu), 16 basi wale walioko Uyahudi wakimbilie milimani. 17 Yeyote aliye juu ya dari ya nyumba asishuke ili kuchukua chochote kutoka ndani ya nyumba. 18 Aliye shambani asirudi nyumbani kuchukua vazi lake. 19 Ole wao wenye mimba na wale wanaonyonyesha watoto siku hizo! 20 Ombeni ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi au siku ya Sabato. 21 Kwa maana wakati huo kutakuwa na dhiki kuu ambayo haijapata kuwako tangu mwanzo wa dunia mpaka sasa: wala haitakuwako tena kamwe. 22 Kama siku hizo zisingefupishwa, hakuna hata mtu mmoja ambaye angeokoka. Lakini kwa ajili ya wateule, siku hizo zitafupizwa. 23 Wakati huo kama mtu yeyote akiwaambia, ‘Tazama, Kristo huyu hapa!’ Au, ‘Kristo yuko kule,’ msisadiki. 24 Kwa maana watatokea makristo wa uongo na manabii wa uongo, nao watafanya ishara kubwa na maajabu mengi ili kuwapotosha, ikiwezekana, hata wale wateule hasa. 25 Angalieni, nimekwisha kuwaambia mapema.
26 “Kwa hiyo mtu yeyote akiwaambia, ‘Yule kule nyikani,’ msiende huko. Au akisema, ‘Yuko kwenye chumba,’ msisadiki. 27 Kwa maana kama vile umeme utokeavyo mashariki na kuonekana hata magharibi, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. 28 Kwa maana popote ulipo mzoga, huko ndiko wakusanyikapo tai.
Kuja Kwa Mwana Wa Adamu
(Marko 13:24-31; Luka 21:25-33)
29 “Mara baada ya dhiki ya siku zile,
“ ‘jua litatiwa giza,
nao mwezi hautatoa nuru yake;
nazo nyota zitaanguka kutoka angani,
na nguvu za anga zitatikisika.’
30 “Ndipo itakapotokea ishara ya Mwana wa Adamu angani, na makabila yote ya dunia yataomboleza. Nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya angani, katika uwezo na utukufu mkuu. 31 Naye atawatuma malaika zake kwa sauti kuu ya tarumbeta, nao watawakusanya wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka mwisho mmoja wa mbingu hadi mwisho mwingine.
32 “Basi jifunzeni somo hili kutokana na mtini: Matawi yake yanapoanza kuchipua na kutoa majani, mnatambua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia. 33 Vivyo hivyo, myaonapo mambo haya yote, mnatambua kwamba wakati u karibu, hata malangoni. 34 Amin, nawaambia, kizazi hiki hakitapita hadi mambo haya yote yawe yametimia. 35 Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
Hakuna Ajuaye Siku Wala Saa
(Marko 13:32-37; Luka 17:26-30, 34-36)
36 “Kwa habari ya siku ile na saa, hakuna ajuaye, hata malaika walio mbinguni wala Mwana, ila Baba peke yake. 37 Kama ilivyokuwa wakati wa Noa, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. 38 Kwa maana siku zile kabla ya gharika, watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa, mpaka siku ile Noa alipoingia katika safina. 39 Nao hawakujua lolote mpaka gharika ilipokuja ikawakumba wote. Hivyo ndivyo itakavyokuwa atakapokuja Mwana wa Adamu. 40 Watu wawili watakuwa shambani, naye mmoja atatwaliwa na mwingine ataachwa. 41 Wanawake wawili watakuwa wanasaga pamoja, naye mmoja atatwaliwa na mwingine ataachwa.
42 “Basi kesheni, kwa sababu hamjui ni siku gani atakapokuja Bwana wenu. 43 Lakini fahamuni jambo hili: Kama mwenye nyumba angejua ni wakati gani wa usiku ambao mwizi atakuja, angekesha na hangekubali nyumba yake kuvunjwa. 44 Kwa hiyo ninyi pia hamna budi kuwa tayari, kwa sababu Mwana wa Adamu atakuja saa msiyotazamia.
Mfano Wa Mtumishi Mwaminifu
(Luka 12:41-48)
45 “Ni nani basi aliye mtumishi mwaminifu na mwenye busara, ambaye bwana wake amemweka kusimamia watumishi wengine katika nyumba yake, ili awape chakula chao kwa wakati unaofaa? 46 Heri mtumishi yule ambaye bwana wake atakaporudi atamkuta akifanya hivyo. 47 Amin, nawaambia, atamweka mtumishi huyo kuwa msimamizi wa mali yake yote. 48 Lakini kama huyo mtumishi ni mwovu, naye akasema moyoni mwake, ‘Bwana wangu atakawia muda mrefu,’ 49 kisha akaanza kuwapiga watumishi wenzake, na kula na kunywa pamoja na walevi. 50 Basi bwana wa mtumishi huyo atakuja siku asiyodhani na saa asiyoijua. 51 Atamkata vipande vipande na kumweka katika sehemu moja pamoja na wanafiki, mahali ambako kutakuwa ni kulia na kusaga meno.