Mika
1
Neno la Bwana lilimjia Mika, Mmoreshethi, wakati wa utawala wa Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda; ufunuo aliouona kuhusu Samaria na Yerusalemu.
 
 
Sikieni, enyi mataifa, enyi nyote,
sikilizeni, ee dunia na wote mliomo ndani yake,
ili Bwana Mwenyezi ashuhudie dhidi yenu,
Bwana kutoka Hekalu lake takatifu.
Hukumu Dhidi Ya Samaria Na Yerusalemu
Tazama! Bwana anakuja kutoka mahali pake;
anashuka na kukanyaga
mahali palipoinuka juu pa dunia.
Milima inayeyuka chini yake
na mabonde yanagawanyika
kama nta mbele ya moto,
kama maji yatiririkayo kasi
kwenye mteremko.
Yote haya ni kwa sababu ya kosa la Yakobo,
ni kwa sababu ya dhambi za nyumba ya Israeli.
Kosa la Yakobo ni lipi?
Je, sio Samaria?
Je, mahali pa juu pa Yuda pa kuabudia miungu ni nini?
Je, sio Yerusalemu?
 
“Kwa hiyo nitaufanya Samaria kuwa lundo la kokoto,
mahali pa kuotesha mizabibu.
Nitayamwaga mawe yake katika bonde
na kuacha wazi misingi yake.
Sanamu zake zote
zitavunjwa vipande vipande;
zawadi zake zote za Hekalu
zitachomwa kwa moto;
nitaharibu vinyago vyake vyote.
Kwa kuwa alikusanya zawadi zake
kutokana na ujira wa kahaba,
nazo zitatumika tena
kulipa mishahara ya kahaba.”
Kulia Na Kuomboleza
Kwa ajili ya hili nitalia na kuomboleza;
nitatembea bila viatu na tena uchi.
Nitabweka kama mbweha
na kuomboleza kama bundi.
Kwa sababu jeraha lake halitibiki;
limekuja Yuda.
Limefika hasa kwenye lango la watu wangu,
hata Yerusalemu kwenyewe.
10 Usiliseme hili huko Gathi;
usilie hata kidogo.
Huko Beth-le-Afra
gaagaa mavumbini.
11 Piteni mkiwa uchi na wenye aibu,
ninyi mkaao Shafiri.
Wale waishio Saanani
hawatatoka nje.
Beth-Eseli iko katika maombolezo;
kinga yake imeondolewa kwako.
12 Wale waishio Marothi wanagaagaa kwa maumivu
wakingoja msaada,
kwa sababu maangamizi yamekuja
kutoka kwa Bwana,
hata katika lango la Yerusalemu.
13 Enyi mkaao Lakishi,
fungeni farasi kwenye magari ya vita.
Mlikuwa chanzo cha dhambi
kwa Binti Sayuni,
kwa kuwa makosa ya Israeli
yalikutwa kwako.
14 Kwa hiyo utaipa Moresheth-Gathi
zawadi za kuagana.
Mji wa Akzibu utaonyesha wazi udanganyifu
kwa wafalme wa Israeli.
15 Nitawaleteeni atakayewashinda
ninyi mnaoishi Maresha.
Yeye aliye utukufu wa Israeli
atakuja Adulamu.
16 Nyoeni nywele zenu katika kuomboleza
kwa ajili ya watoto wenu mnaowafurahia;
jifanyieni upara kama tai,
kwa kuwa watawaacha
na kwenda uhamishoni.