12
Mfano Wa Wapangaji Waovu
(Mathayo 21:33-46; Luka 20:9-19)
1 Yesu akaanza kusema nao kwa mifano, akawaambia: “Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu. Akajenga ukuta kulizunguka, akachimba shimo ndani yake kwa ajili ya shinikizo la kusindika divai, na akajenga mnara wa ulinzi. Kisha akalikodisha shamba hilo la mizabibu kwa wakulima fulani, kisha akasafiri kwenda nchi nyingine. 2 Wakati wa mavuno ulipofika, mwenye shamba akamtuma mtumishi wake kwa hao wapangaji ili kuchukua sehemu yake ya mavuno ya shamba la mizabibu kutoka kwa hao wapangaji. 3 Lakini wale wakulima walimkamata yule mtumishi, wakampiga, wakamfukuza mikono mitupu. 4 Kisha yule mwenye shamba akamtuma mtumishi mwingine kwao; nao wale wakulima wakampiga kichwani na kumfanyia mambo ya aibu. 5 Kisha akamtuma mtumishi mwingine, naye huyo wakamuua. Akawatuma wengine wengi; baadhi yao wakawapiga, na wengine wakawaua.
6 “Mwenye shamba alikuwa bado na mmoja wa kumtuma, mwanawe aliyempenda. Hatimaye akamtuma akisema, ‘Watamheshimu mwanangu.’
7 “Lakini wale wapangaji wakasemezana pamoja, ‘Huyu ndiye mrithi. Njooni tumuue, nao urithi utakuwa wetu.’ 8 Hivyo wakamchukua na kumuua, wakamtupa nje ya lile shamba la mizabibu.
9 “Sasa basi yule mwenye shamba atafanya nini? Atakuja na kuwaua hao wapangaji, kisha atawapa wapangaji wengine hilo shamba la mizabibu. 10 Je, hamjasoma Andiko hili:
“ ‘Jiwe walilolikataa waashi
limekuwa jiwe kuu la pembeni;
11 Bwana ndiye alitenda jambo hili,
nalo ni ajabu machoni petu’?”
12 Walipotambua kuwa amesema mfano huo kwa ajili yao, wakataka kumkamata, lakini wakaogopa ule umati wa watu. Wakamwacha, wakaondoka, wakaenda zao.
Swali Kuhusu Kulipa Kodi
(Mathayo 22:15-22; Luka 20:20-26)
13 Baadaye wakawatuma baadhi ya Mafarisayo na Maherode ili kwenda kumtega Yesu katika yale anayosema. 14 Wakamjia, wakamwambia, “Mwalimu, tunajua kwamba wewe ni mtu mwadilifu. Wewe huyumbishwi na wanadamu, kwa kuwa huna upendeleo. Lakini wewe huifundisha njia ya Mungu katika kweli. Je, ni halali kulipa kodi kwa Kaisari, au la? 15 Je, tulipe kodi au tusilipe?”
Lakini Yesu alijua unafiki wao. Akawauliza “Mbona mnajaribu kunitega? Nileteeni hiyo dinari*Dinari moja ilikuwa sawa na mshahara wa kibarua wa siku moja.niione.” 16 Wakamletea hiyo sarafu. Naye akawauliza, “Sura hii ni ya nani? Na maandishi haya ni ya nani?”
Wakamjibu, “Ni vya Kaisari.”
17 Ndipo Yesu akawaambia, “Mpeni Kaisari kilicho cha Kaisari, naye Mungu mpeni kilicho cha Mungu.”
Nao wakamstaajabia sana.
Ndoa Wakati Wa Ufufuo
(Mathayo 22:23-33; Luka 20:27-40)
18 Kisha Masadukayo, wale wasemao kuwa hakuna ufufuo wa wafu, wakamjia Yesu, 19 wakasema, “Mwalimu, Mose alituandikia kuwa kama ndugu wa mtu akifa na kumwacha mkewe bila mtoto, basi huyo mtu inampasa amwoe huyo mjane ili amzalie ndugu yake watoto. 20 Basi palikuwepo ndugu saba. Yule wa kwanza akaoa mke, naye akafa pasipo kuwa na mtoto yeyote. 21 Wa pili akamwoa yule mjane, lakini naye akafa bila kuacha mtoto yeyote. Ikawa vivyo hivyo kwa yule wa tatu. 22 Hakuna hata mmojawapo wa hao ndugu wote saba aliyeacha mtoto. Hatimaye yule mwanamke naye akafa. 23 Kwa hiyo wakati wa ufufuo, yeye atakuwa mke wa nani, maana aliolewa na ndugu wote saba?”
24 Yesu akawajibu, “Je, hampotoki kwa sababu hamfahamu Maandiko wala uweza wa Mungu? 25 Wafu watakapofufuka, hawataoa wala kuolewa, bali watakuwa kama malaika wa mbinguni. 26 Basi kuhusu wafu kufufuliwa, je hamjasoma katika Kitabu cha Mose jinsi Mungu alivyosema na Mose kutoka kile kichaka akisema, ‘Mimi ni Mungu wa Abrahamu, na Mungu wa Isaki, na Mungu wa Yakobo?’ 27 Yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai. Kwa hiyo mmekosea kabisa.”
Amri Iliyo Kuu
(Mathayo 22:34-40; Luka 10:25-28)
28 Mwalimu mmoja wa sheria akaja, akawasikia wakijadiliana. Akiona kwamba Yesu amewajibu vyema, naye akamuuliza, “Katika amri zote, ni ipi iliyo kuu?”
29 Yesu akajibu, “Amri iliyo kuu ndiyo hii: ‘Sikia ee Israeli. Bwana Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja. 30 Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote.’ 31 Ya pili ndiyo hii: ‘Mpende jirani yako kama nafsi yako.’ Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi.”
32 Yule mwalimu wa sheria akamwambia Yesu, “Mwalimu, umejibu vyema kwamba Mungu ni mmoja, wala hakuna mwingine ila yeye. 33 Kumpenda Mungu kwa moyo wote na kwa akili zote na kwa nguvu zote, na kumpenda jirani kama mtu anavyojipenda mwenyewe ni bora zaidi kuliko kutoa sadaka za kuteketezwa na dhabihu zote.”
34 Yesu alipoona kwamba amejibu kwa busara, akamwambia, “Wewe hauko mbali na Ufalme wa Mungu.” Tangu wakati huo, hakuna mtu yeyote aliyethubutu kumuuliza maswali tena.
Kristo Ni Mwana Wa Nani?
(Mathayo 22:41-46; Luka 20:41-44)
35 Yesu alipokuwa akifundisha Hekaluni, akauliza, “Imekuwaje walimu wa sheria wanasema kwamba Kristo†Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta.ni Mwana wa Daudi? 36 Kwa maana Daudi mwenyewe, akinena kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu, alisema:
“ ‘Bwana alimwambia Bwana wangu:
“Keti mkono wangu wa kuume,
hadi nitakapowaweka adui zako
chini ya miguu yako.” ’
37 Kwa hiyo Daudi mwenyewe anamwita ‘Bwana.’ Awezaje basi yeye kuwa mwanawe?”
Ule umati wote wa watu wakamsikiliza kwa furaha.
Yesu Awatahadharisha Watu Kuhusu Walimu Wa Sheria
(Mathayo 23:1-36; Luka 20:45-47)
38 Alipokuwa akifundisha, Yesu alisema, “Jihadharini na walimu wa sheria. Wao hupenda kutembea wakiwa wamevaa mavazi marefu, na kusalimiwa kwa heshima masokoni. 39 Pia wao hupenda kukaa kwenye viti vya mbele katika masinagogi, na kupewa nafasi za heshima katika karamu. 40 Wao hula nyumba za wajane, na ili waonekane kuwa wema wanasali sala ndefu. Watu kama hawa watapata hukumu iliyo kuu sana.”
Sadaka Ya Mjane
(Luka 21:1-4)
41 Kisha Yesu akaketi mkabala na sehemu ambapo sadaka zilikuwa zinawekwa na kuangalia umati wa watu wakiweka fedha zao kwenye sanduku la hazina ya Hekalu. Matajiri wengi wakaweka kiasi kikubwa cha fedha. 42 Lakini mjane mmoja maskini akaja na kuweka sarafu mbili ndogo za shaba zenye thamani ya senti mbili.
43 Yesu akawaita wanafunzi wake, akawaambia, “Amin, nawaambia, huyu mjane maskini ameweka katika sanduku la hazina zaidi ya watu wengine wote. 44 Wengine wote wametoa kutokana na ziada ya mali zao. Lakini huyu mjane ametoa kutokana na umaskini wake, akaweka kila kitu alichokuwa nacho, hata kile alichohitaji ili kuishi.”