16
Kufufuka Kwa Yesu
(Mathayo 28:1-8; Luka 24:1-12; Yohana 20:1-10)
Sabato ilipomalizika, Maria Magdalene, Maria mama yake Yakobo, na Salome walinunua manukato ili wakaupake mwili wa Yesu. Asubuhi na mapema, siku ya kwanza ya juma, mara tu baada ya kuchomoza jua, walikwenda kaburini. Njiani wakawa wanaulizana wao kwa wao, “Ni nani atakayetuvingirishia lile jiwe kutoka kwenye ingilio la kaburi?”
Lakini walipotazama, wakaona lile jiwe, ambalo lilikuwa kubwa sana, limekwisha kuvingirishwa kutoka pale penye ingilio la kaburi. Walipokuwa wakiingia mle kaburini, wakamwona kijana mmoja aliyevaa joho jeupe akiwa ameketi upande wa kuume, nao wakastaajabu.
Yule malaika akawaambia, “Msistaajabu. Mnamtafuta Yesu, Mnazareti, aliyesulubiwa. Amefufuka! Hayuko hapa. Tazameni mahali walipomlaza. Lakini nendeni mkawaambie wanafunzi wake pamoja na Petro, kwamba, ‘Anawatangulia kwenda Galilaya. Huko ndiko mtamwona, kama alivyowaambia.’ ”
Hivyo wakatoka, wakakimbia kutoka mle kaburini wakiwa na hofu kuu na mshangao. Nao hawakumwambia mtu yeyote neno lolote, kwa sababu waliogopa.
Yesu Anamtokea Maria Magdalene
(Mathayo 28:9-10; Yohana 20:11-18)
Yesu alipofufuka alfajiri na mapema siku ya kwanza ya juma alimtokea kwanza Maria Magdalene, yule ambaye alikuwa amemtoa pepo wachafu saba. 10 Maria akaenda, naye akawaambia wale waliokuwa wamefuatana na Yesu, waliokuwa wanaomboleza na kulia. 11 Lakini waliposikia kwamba Yesu yu hai na kwamba Maria alikuwa amemwona, hawakusadiki.
Yesu Awatokea Wanafunzi Wawili
(Luka 24:13-35)
12 Baadaye Yesu akawatokea wawili miongoni mwa wanafunzi wake walipokuwa wakienda shambani akiwa katika sura nyingine. 13 Nao wakarudi na kuwaambia wenzao. Lakini hawakuwasadiki wao pia.
Yesu Awaagiza Wale Wanafunzi Kumi Na Mmoja
(Mathayo 28:16-20; Luka 24:36-49; Yohana 20:19-23; Matendo 1:6-8)
14 Baadaye Yesu akawatokea wale wanafunzi kumi na mmoja walipokuwa wakila chakula. Akawakemea kwa kutoamini kwao na kwa ugumu wa mioyo yao kwa kutosadiki wale waliomwona baada yake kufufuka.
15 Akawaambia, “Enendeni ulimwenguni kote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. 16 Yeyote aaminiye na kubatizwa ataokoka. Lakini yeyote asiyeamini atahukumiwa. 17 Nazo ishara hizi zitafuatana na wanaoamini: Kwa Jina langu watatoa pepo wachafu; watasema kwa lugha mpya; 18 watashika nyoka kwa mikono yao; na hata wakinywa kitu chochote cha kuua, hakitawadhuru kamwe; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapona.”
[Yesu Apaa Kwenda Mbinguni
(Luka 24:50-53; Matendo 1:9-11)
19 Baada ya Bwana Yesu kusema nao, alichukuliwa juu mbinguni na kuketi mkono wa kuume wa Mungu. 20 Kisha wanafunzi wake wakatoka, wakahubiri kila mahali, naye Bwana akatenda kazi pamoja nao na kulithibitisha neno lake kwa ishara zilizofuatana nalo.]