10
1 Wale waliotia muhuri walikuwa:
Nehemia mtawala, mwana wa Hakalia.
Sedekia, 2 Seraya, Azaria, Yeremia,
3 Pashuri, Amaria, Malkiya,
4 Hatushi, Shebania, Maluki,
5 Harimu, Meremothi, Obadia,
6 Danieli, Ginethoni, Baruku,
7 Meshulamu, Abiya, Miyamini,
8 Maazia, Bilgai na Shemaya.
Hawa ndio waliokuwa makuhani.
9 Walawi:
Yeshua mwana wa Azania, Binui wa wana wa Henadadi, Kadmieli,
10 na wenzao: Shebania,
Hodia, Kelita, Pelaya, Hanani,
11 Mika, Rehobu, Hashabia,
12 Zakuri, Sherebia, Shebania,
13 Hodia, Bani na Beninu.
14 Viongozi wa watu:
Paroshi, Pahath-Moabu, Elamu, Zatu, Bani,
15 Buni, Azgadi, Bebai,
16 Adoniya, Bigwai, Adini,
17 Ateri, Hezekia, Azuri,
18 Hodia, Hashumu, Besai,
19 Harifu, Anathothi, Nebai,
20 Magpiashi, Meshulamu, Heziri,
21 Meshezabeli, Sadoki, Yadua,
22 Pelatia, Hanani, Anaya,
23 Hoshea, Hanania, Hashubu,
24 Haloheshi, Pilha, Shobeki,
25 Rehumu, Hashabna, Maaseya,
26 Ahiya, Hanani, Anani,
27 Maluki, Harimu na Baana.
28 “Watu wengine wote, wakiwa ni makuhani, Walawi, mabawabu, waimbaji, watumishi wa Hekalu,*Yaani Wanethini. na wale wote waliojitenga na mataifa jirani kwa ajili ya Sheria ya Mungu, pamoja na wake zao na wana wao na binti zao wote waliokuwa na uwezo wa kufahamu, 29 basi hawa wote wanajiunga na ndugu zao na wakuu wao, na kujifunga kwa laana na kwa kiapo kufuata Sheria ya Mungu iliyotolewa kupitia kwa Mose mtumishi wa Mungu, na kutii kwa uangalifu amri zote, maagizo na sheria za Bwana, Bwana wetu.
30 “Tunaahidi kutowaoza binti zetu kwa watu wanaotuzunguka, wala kuwaoza wana wetu binti zao.
31 “Wakati mataifa jirani waletapo bidhaa zao au nafaka kuuza siku ya Sabato, hatutazinunua kutoka kwao siku ya Sabato, wala siku nyingine yoyote takatifu. Kila mwaka wa saba, tutaacha kuilima ardhi na tutafuta madeni yote.
32 “Tunakubali wajibu wa kutimiza amri za kutoa theluthi ya shekeli†Theluthi ya shekeli hapa kama gramu 4. kila mwaka kwa ajili ya utumishi wa nyumba ya Mungu: 33 Kwa ajili ya mikate ya Wonyesho, kwa ajili ya sadaka za kawaida za nafaka na sadaka za kuteketezwa, kwa ajili ya sadaka za siku za Sabato, Sikukuu za Mwandamo wa Mwezi na sikukuu nyingine zilizoamriwa, kwa ajili ya sadaka takatifu, kwa ajili ya sadaka za dhambi ili kufanya upatanisho kwa ajili ya Israeli, na kwa ajili ya kazi zote za nyumba ya Mungu wetu.
34 “Sisi makuhani, Walawi na watu, tumepiga kura kuamua kuwa kila mmoja wa jamaa zetu lazima alete katika nyumba ya Mungu wetu kwa nyakati maalum kila mwaka mchango wa kuni za kukokea moto katika madhabahu ya Bwana Mungu wetu, kama ilivyoandikwa katika Sheria.
35 “Pia tunachukua wajibu wa kuleta malimbuko ya mazao yetu na matunda ya kwanza ya kila mti wa matunda katika nyumba ya Bwana kila mwaka.
36 “Kama pia ilivyoandikwa katika Sheria, tutawaleta wazaliwa wetu wa kwanza wa kiume, na wa mifugo yetu, yaani wa ngʼombe wetu na wa makundi yetu ya kondoo na mbuzi, katika nyumba ya Mungu wetu, kwa ajili ya makuhani wanaohudumu huko.
37 “Zaidi ya hayo, tutaleta katika ghala za nyumba ya Mungu wetu, kwa makuhani, vyakula vya kwanza vya mashamba yetu, sadaka zetu za nafaka, matunda ya miti yetu yote, divai yetu mpya na mafuta. Nasi tutaleta zaka za mazao yetu kwa Walawi, kwa kuwa Walawi ndio ambao hukusanya zaka katika miji yote tunakofanya kazi. 38 Kuhani atokanaye na uzao wa Aroni atashirikiana na Walawi wakati wanapopokea zaka, nao Walawi itawapasa kuleta sehemu ya kumi ya zaka katika nyumba ya Mungu wetu katika ghala za hazina. 39 Watu wa Israeli pamoja na Walawi itawapasa kuleta michango yao ya nafaka, divai mpya na mafuta katika vyumba vya ghala, mahali vifaa vya mahali patakatifu vinapohifadhiwa, na wanapokaa makuhani wanaohudumu, na mabawabu na waimbaji.
“Hatutaacha kuijali nyumba ya Mungu wetu.”