12
Miriamu Na Aroni Wampinga Mose
Miriamu na Aroni walianza kuzungumza dhidi ya Mose kwa sababu ya mke wake Mkushi, kwa kuwa alikuwa ameoa Mkushi. Waliuliza, “Je, Bwana amesema kupitia Mose peke yake? Je, hajasema kutupitia sisi pia?” Naye Bwana akasikia hili.
(Basi Mose alikuwa mtu mnyenyekevu sana, mnyenyekevu kuliko mtu mwingine yeyote katika uso wa dunia.)
Ghafula Bwana akawaambia Mose, Aroni na Miriamu, “Njooni katika Hema la Kukutania, ninyi nyote watatu.” Kwa hiyo wote watatu wakaenda. Kisha Bwana akashuka katika nguzo ya wingu, akasimama kwenye ingilio la Hema, akawaita Aroni na Miriamu. Wakati wote wawili waliposogea mbele, Bwana akasema, “Sikilizeni maneno yangu:
“Akiwapo nabii wa Bwana miongoni mwenu,
nitajifunua kwake kwa maono,
nitanena naye katika ndoto.
Lakini sivyo kwa mtumishi wangu Mose;
yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote.
Kwake nitanena naye uso kwa uso,
waziwazi wala si kwa mafumbo;
yeye ataona umbo la Bwana.
Kwa nini basi ninyi hamkuogopa
kuzungumza kinyume cha mtumishi wangu Mose?”
Hasira ya Bwana ikawaka dhidi yao, akawaacha.
10 Wakati hilo wingu liliinuka kutoka juu ya Hema, Miriamu akawa tayari ana ukoma, mweupe kama theluji. Aroni akamgeukia, akaona ana ukoma. 11 Kisha Aroni akamwambia Mose, “Tafadhali, bwana wangu, usituhesabie dhambi hii ambayo tumeifanya kwa upumbavu. 12 Usimwache awe kama mtoto mchanga aliyezaliwa akiwa mfu, ambaye nusu ya mwili wake imeharibika hapo atokapo katika tumbo la mama yake.”
13 Hivyo Mose akamlilia Bwana akisema, “Ee Mungu, nakuomba umponye!”
14 Bwana akamjibu Mose, “Je, kama baba yake angemtemea usoni, asingeona aibu kwa siku saba? Mfungie nje ya kambi kwa siku saba; baada ya hapo anaweza kurudishwa kambini.” 15 Kwa hiyo Miriamu akafungiwa nje ya kambi kwa siku saba, nao watu hawakuendelea na safari mpaka aliporudishwa kambini.
16 Baada ya hayo, watu waliondoka Haserothi, wakapiga kambi katika Jangwa la Parani.