16
Kora, Dathani Na Abiramu
Kora mwana wa Ishari, mwana wa Kohathi, mwana wa Lawi, pamoja na baadhi ya Wareubeni, yaani Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu, na Oni mwana wa Pelethi, wakachukua baadhi ya watu, wakainuka dhidi ya Mose. Pamoja nao walikuwepo wanaume wa Kiisraeli 250, watu waliojulikana, viongozi wa jumuiya waliokuwa wameteuliwa kuwa wakuu wa kusanyiko. Wakaja kama kikundi kuwapinga Mose na Aroni, wakawaambia, “Ninyi mmejitukuza sana! Kusanyiko hili lote ni takatifu, kila mmoja wao, naye Bwana yu pamoja nao. Kwa nini basi mmejitukuza wenyewe juu ya kusanyiko la Bwana?”
Mose aliposikia jambo hili, akaanguka kifudifudi. Kisha akamwambia Kora na wafuasi wake wote: “Asubuhi Bwana ataonyesha ni nani aliye wake na ni nani aliye mtakatifu, tena atamtaka mtu huyo aje kwake. Mtu yule ambaye atamchagua atamfanya kuja karibu naye. Wewe Kora na wafuasi wako wote mtafanya hivi: Chukueni vyetezo, kesho wekeni moto na uvumba kwenye hivyo vyetezo mbele za Bwana. Mtu ambaye Bwana atamchagua atakuwa ndiye mtakatifu. Ninyi Walawi mmejitukuza sana!”
Pia Mose akamwambia Kora, “Enyi Walawi! Sasa nisikilizeni. Haiwatoshi ninyi kwamba Mungu wa Israeli amewateua ninyi kutoka kusanyiko lote la Kiisraeli, na kuwaleta karibu naye mpate kufanya kazi kwenye Maskani ya Bwana, na kusimama mbele ya kusanyiko ili kuwahudumia? 10 Amekuleta wewe na ndugu zako Walawi mwe karibu naye, lakini sasa unajaribu kupata na ukuhani pia. 11 Wewe na wafuasi wako wote mmekusanyika pamoja kinyume cha Bwana. Aroni ni nani kwamba ninyi mnungʼunike dhidi yake?”
12 Kisha Mose akawaita Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu. Lakini wao wakasema, “Sisi hatuji! 13 Haitoshi tu kwamba wewe umetuleta kutoka nchi itiririkayo maziwa na asali ili kutuua sisi jangwani? Nawe sasa pia unataka kuwa mkuu juu yetu? 14 Zaidi ya hayo, hujatuingiza katika nchi inayotiririka maziwa na asali, wala hujatupa urithi wa mashamba na mashamba ya mizabibu. Je, utayangʼoa macho ya watu hawa? Hapana, sisi hatuji!”
15 Ndipo Mose akakasirika sana na kumwambia Bwana, “Usiikubali sadaka yao. Mimi sikuchukua chochote, hata punda kutoka kwao, wala sijamkosea hata mmoja wao.”
16 Mose akamwambia Kora, “Wewe na wafuasi wako wote kesho mtatokea mbele za Bwana: yaani wewe na hao wenzako, pamoja na Aroni. 17 Kila mtu atachukua chetezo chake na kuweka uvumba ndani yake, vyetezo 250 kwa jumla, na kukileta mbele za Bwana. Wewe na Aroni mtaleta vyetezo vyenu pia.” 18 Kwa hiyo kila mtu akachukua chetezo chake, akaweka moto na uvumba ndani yake, na kusimama pamoja na Mose na Aroni kwenye mlango wa Hema la Kukutania. 19 Kora alipokuwa amekusanya wafuasi wake wote kuwapinga Mose na Aroni kwenye mlango wa Hema la Kukutania, utukufu wa Bwana ukatokea kwa kusanyiko lote. 20 Bwana akamwambia Mose na Aroni, 21 “Jitengeni kutoka kwenye kusanyiko hili ili nipate kuwaangamiza mara moja.”
22 Lakini Mose na Aroni wakaanguka kufudifudi na kulia kwa sauti, wakasema, “Ee Mungu, Mungu wa roho za wanadamu wote, utakuwa na hasira na kusanyiko lote wakati ni mtu mmoja tu ametenda dhambi?”
23 Ndipo Bwana akamwambia Mose, 24 “Liambie kusanyiko, ‘Ondokeni hapo karibu na mahema ya Kora, Dathani na Abiramu.’ ”
25 Mose akainuka na kuwaendea Dathani na Abiramu, nao wazee wa Israeli wakafuatana naye. 26 Mose akalionya kusanyiko, “Sogeeni nyuma mbali na mahema ya hawa watu waovu! Msiguse kitu chochote kilicho mali yao, la sivyo mtafagiliwa mbali kwa sababu ya dhambi zao zote.” 27 Hivyo wakaondoka karibu na mahema ya Kora, Dathani na Abiramu. Dathani na Abiramu walikuwa wametoka nje, nao walikuwa wamesimama pamoja na wake zao, watoto wao na wale wanyonyao kwenye mlango wa mahema yao.
28 Ndipo Mose akasema, “Hivi ndivyo mtakavyojua kuwa Bwana amenituma kufanya mambo haya, na kwamba halikuwa wazo langu. 29 Ikiwa watu hawa watakufa kifo cha kawaida na kupatwa na yale ya kawaida yanayowapata wanadamu, basi Bwana hakunituma mimi. 30 Lakini ikiwa Bwana ataleta jambo jipya kabisa, ardhi ikifunua kinywa chake na kuwameza wao, pamoja na kila kitu kilicho mali yao, nao washuke chini kaburini*Kaburini hapa maana yake ni Kuzimu, kwa Kiebrania ni Sheol. wakiwa hai, ndipo mtafahamu kuwa watu hawa wamemdharau Bwana.”
31 Mara Mose alipomaliza kusema haya yote, ardhi iliyokuwa chini yao ikapasuka, 32 nchi ikafunua kinywa chake na kuwameza wao, pamoja na jamaa zao, na watu wote wa Kora na mali zao zote. 33 Wakashuka chini kaburini wakiwa hai, pamoja na kila kitu walichokuwa nacho; nchi ikajifunika juu yao, nao wakaangamia wakatoweka kutoka kusanyiko. 34 Kutoka kilio chao, Waisraeli wote waliowazunguka walikimbia, wakipaza sauti, “Nchi inatumeza na sisi pia!”
35 Moto ukaja kutoka kwa Bwana, ukawateketeza wale watu 250 waliokuwa wakifukiza uvumba.
36 Bwana akamwambia Mose, 37 “Mwambie Eleazari mwana wa kuhani Aroni, atoe vyetezo kwenye mabaki ya moto na kutawanya makaa mbali kiasi, kwa maana vyetezo ni vitakatifu: 38 vyetezo vya watu waliofanya dhambi iliyowagharimu maisha yao. Fua vyetezo hivyo kuwa bamba ili kufunika madhabahu, kwa maana vimeletwa mbele za Bwana na vimekuwa vitakatifu. Navyo viwe ishara kwa Waisraeli.”
39 Hivyo kuhani Eleazari akavikusanya vile vyetezo vya shaba vilivyoletwa na wale waliokuwa wameteketezwa kwa moto, naye akavifua kufunika madhabahu, 40 kama vile Bwana alivyomwelekeza kupitia Mose. Hili lilikuwa kuwakumbusha Waisraeli kwamba hakuna mtu hata mmoja, isipokuwa mzao wa Aroni, awezaye kuja kufukiza uvumba mbele za Bwana, la sivyo, angekuwa kama Kora na wafuasi wake.
41 Siku iliyofuata jumuiya yote ya Kiisraeli wakanungʼunika dhidi ya Mose na Aroni, wakisema, “Mmewaua watu wa Bwana.”
42 Lakini wakati kusanyiko lilipokusanyika kupingana na Mose na Aroni, nalo likageuka kuelekea Hema la Kukutania, ghafula wingu likafunika Hema, nao utukufu wa Bwana ukatokea. 43 Ndipo Mose na Aroni wakaenda mbele ya Hema la Kukutania, 44 naye Bwana akamwambia Mose, 45 “Jitenge mbali na kusanyiko hili ili niweze kuwaangamiza mara moja.” Wakaanguka chini kifudifudi.
46 Kisha Mose akamwambia Aroni, “Chukua chetezo chako na uweke uvumba ndani yake, pamoja na moto kutoka madhabahuni, nawe uende haraka kwenye kusanyiko ili kufanya upatanisho kwa ajili yao. Ghadhabu imekuja kutoka kwa Bwana, na tauni imeanza.” 47 Hivyo Aroni akafanya kama Mose alivyosema, akakimbilia katikati ya kusanyiko. Tauni ilikuwa tayari imeanza miongoni mwa watu, lakini Aroni akafukiza uvumba na kufanya upatanisho kwa ajili yao. 48 Aroni akasimama kati ya waliokuwa hai na waliokufa, nayo tauni ikakoma. 49 Lakini walikufa watu 14,700 kutokana na tauni hiyo, licha ya wale waliokuwa wamekufa kwa sababu ya Kora. 50 Ndipo Aroni akamrudia Mose kwenye mlango wa Hema la Kukutania, kwa maana tauni ilikuwa imekoma.

*16:30 Kaburini hapa maana yake ni Kuzimu, kwa Kiebrania ni Sheol.