25
Moabu Yashawishi Israeli
Israeli alipokuwa akikaa Shitimu, wanaume wa Israeli walianza kuzini na wanawake wa Kimoabu, ambao waliwaalika kushiriki katika kutoa kafara kwa miungu yao. Watu wakala na kusujudu mbele ya miungu hii. Kwa hiyo Israeli akaungana katika kumwabudu Baali wa Peori. Hasira ya Bwana ikawaka dhidi yao.
Bwana akamwambia Mose, “Uwachukue viongozi wote wa watu hawa, uwaue na uwaweke hadharani mchana peupe mbele za Bwana, ili hasira kali ya Bwana iweze kuondoka kwa Israeli.”
Kwa hiyo Mose akawaambia waamuzi wa Israeli, “Kila mmoja wenu lazima awaue wale wanaume wenu, walioshiriki katika kumwabudu Baali wa Peori.”
Ndipo mwanaume wa Kiisraeli akamleta mwanamke wa Kimidiani katika jamaa yake palepale mbele ya Mose na mkutano wote wa Israeli walipokuwa wakilia kwenye lango la Hema la Kukutania. Finehasi mwana wa Eleazari, mwana wa kuhani Aroni, alipoona jambo hili, akaondoka kwenye kusanyiko, akachukua mkuki mkononi mwake, akamfuata yule Mwisraeli ndani ya hema. Akawachoma mkuki wote wawili kwa pamoja, ukapenya kwenye mwili wa yule Mwisraeli na mwili wa yule mwanamke. Ndipo tauni iliyokuwepo dhidi ya Waisraeli ikakoma. Lakini wale waliokufa kwa hiyo tauni walikuwa watu 24,000.
10 Bwana akamwambia Mose, 11 “Finehasi mwana wa Eleazari, mwana wa kuhani Aroni, amegeuza hasira yangu mbali na Waisraeli, kwa sababu alikuwa na wivu kama nilio nao kwa heshima yangu miongoni mwao, hata kwamba kwa wivu wangu sikuwaangamiza. 12 Kwa hiyo mwambie Finehasi ninafanya Agano langu la amani naye. 13 Yeye pamoja na wazao wake watakuwa na Agano la ukuhani milele, kwa sababu alikuwa na wivu kwa ajili ya heshima ya Mungu wake, na akafanya upatanisho kwa Waisraeli.”
14 Jina la Mwisraeli ambaye aliuawa pamoja na mwanamke wa Kimidiani ni Zimri mwana wa Salu, kiongozi wa jamaa ya Simeoni. 15 Jina la mwanamke wa Kimidiani aliyeuawa ni Kozbi binti wa Suri, aliyekuwa mkuu wa kabila la jamaa ya Wamidiani.
16 Bwana akamwambia Mose, 17 “Watendeeni Wamidiani kama adui na mwaue, 18 kwa sababu wao waliwatendea kama adui wakati waliwadanganya katika tukio la Peori na dada yao Kozbi, binti wa kiongozi wa Kimidiani, mwanamke ambaye aliuawa wakati tauni ilikuja kama matokeo ya tukio la Peori.”