Mithali
1
Utangulizi: Kusudi Na Kiini
Mithali za Solomoni mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli:
Kwa kupata hekima na nidhamu;
kwa kufahamu maneno ya busara;
kwa kujipatia nidhamu na busara,
kufanya lililo sawa, haki na bila kupendelea;
huwapa busara wajinga,
maarifa na akili kwa vijana;
wenye hekima na wasikilize nao waongeze elimu yao,
wenye kupambanua na wapate mwongozo;
kwa kufahamu mithali na mifano,
misemo na vitendawili vya wenye hekima.
 
Kumcha Bwana ndicho chanzo cha maarifa,
lakini wapumbavu hudharau hekima na adabu.
Onyo Dhidi Ya Ushawishi Wa Marafiki Waovu
Mwanangu, sikiliza mwongozo wa baba yako,
wala usiyaache mafundisho ya mama yako.
Hayo yatakuwa taji la maua la neema kichwani pako,
na mkufu wa kuipamba shingo yako.
 
10 Mwanangu, kama wenye dhambi wakikushawishi,
usikubaliane nao.
11 Kama wakisema, “Twende tufuatane;
tukamvizie mtu na kumwaga damu,
njoo tukavizie nafsi isiyo na hatia;
12 tuwameze wakiwa hai kama kaburi,* Kaburi hapa maana yake ni Kuzimu, kwa Kiebrania ni Sheol.
wakiwa wazima kama wale wanaotumbukia shimoni.
13 Tutapata aina zote za vitu vya thamani
na kujaza nyumba zetu kwa nyara.
14 Njoo ushirikiane nasi,
vitu vyote tutakavyopata tutagawana.”
15 Mwanangu, usiandamane nao.
Usiweke mguu wako katika njia zao,
16 kwa kuwa miguu yao hukimbilia kwenye dhambi,
ni wepesi kumwaga damu.
17 Tazama ni jinsi gani ilivyo kazi bure kutandaza wavu
wakati ndege wote wanakuona!
18 Watu hawa huvizia kumwaga damu yao wenyewe;
hujivizia tu wenyewe!
19 Huu ndio mwisho wa wote ambao wanajipatia mali kwa hila;
huuondoa uhai wa wale wenye mali.
Onyo Dhidi Ya Kukataa Hekima
20 Hekima huita kwa sauti kuu barabarani,
hupaza sauti yake kwenye viwanja vikubwa;
21 kwenye makutano ya barabara za mji
zenye makelele mengi hupaza sauti,
kwenye malango ya mji hutoa hotuba yake:
 
22 “Enyi wajinga, mtangʼangʼania ujinga wenu hadi lini?
Mpaka lini wenye mizaha watafurahia mizaha,
na wapumbavu kuchukia maarifa?
23 Kama mngekuwa mmeitikia karipio langu,
ningekuwa nimemimina roho yangu kwenu
na kuwafahamisha maneno yangu.
24 Lakini kwa kuwa mlinikataa nilipowaita
na hakuna yeyote aliyekubali
niliponyoosha mkono wangu,
25 kwa kuwa mliyapuuza mashauri yangu yote
na hamkukubali karipio langu,
26 mimi nami nitawacheka katika maafa yenu,
nitawadhihaki wakati janga litawapata:
27 wakati janga litawapata kama tufani,
wakati maafa yatawazoa kama upepo wa kisulisuli,
wakati dhiki na taabu zitawalemea.
 
28 “Ndipo watakaponiita lakini sitawajibu;
watanitafuta lakini hawatanipata.
29 Kwa kuwa walichukia maarifa,
wala hawakuchagua kumcha Bwana,
30 kwa kuwa hawakukubali mashauri yangu,
na kukataa maonyo yangu,
31 watakula matunda ya njia zao,
na watashibishwa matunda ya hila zao.
32 Kwa kuwa ukaidi wa wajinga utawaua,
nako kuridhika kwa wajinga kutawaangamiza.
33 Lakini yeyote anisikilizaye ataishi kwa usalama,
atatulia, bila kuwa na hofu ya madhara.”

*1:12 Kaburi hapa maana yake ni Kuzimu, kwa Kiebrania ni Sheol.