3
Faida Nyingine Za Hekima
Mwanangu, usisahau mafundisho yangu,
bali zitunze amri zangu moyoni mwako,
kwa kuwa zitakuongezea miaka mingi ya maisha yako
na kukuletea mafanikio.
 
Usiache kamwe upendo na uaminifu vitengane nawe;
vifunge shingoni mwako,
viandike katika ubao wa moyo wako.
Ndipo utapata kibali na jina zuri
mbele za Mungu na mwanadamu.
 
Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote
wala usizitegemee akili zako mwenyewe;
katika njia zako zote mkiri yeye,
naye atayanyoosha mapito yako.
 
Usiwe mwenye hekima machoni pako mwenyewe;
mche Bwana ukajiepushe na uovu.
Hii itakuletea afya mwilini mwako,
na mafuta kwenye mifupa yako.
 
Mheshimu Bwana kwa mali zako na
kwa malimbuko ya mazao yako yote;
10 ndipo ghala zako zitakapojaa hadi kufurika,
viriba vyako vitafurika kwa mvinyo mpya.
 
11 Mwanangu, usiidharau adhabu ya Bwana
na usichukie kukaripiwa naye,
12 kwa sababu Bwana huwaadibisha wale awapendao,
kama vile baba afanyavyo
kwa mwana apendezwaye naye.
 
13 Heri mtu yule aonaye hekima,
mtu yule apataye ufahamu,
14 kwa maana hekima ana faida kuliko fedha
na mapato yake ni bora kuliko ya dhahabu safi.
15 Hekima ana thamani kuliko marijani;
hakuna chochote unachokitamani
kinachoweza kulinganishwa naye.
16 Maisha marefu yako katika mkono wake wa kuume;
katika mkono wake wa kushoto
kuna utajiri na heshima.
17 Njia zake zinapendeza,
mapito yake yote ni amani.
18 Yeye ni mti wa uzima kwa wale wanaomkumbatia;
wale wamshikao watabarikiwa.
 
19 Kwa hekima Bwana aliiweka misingi ya dunia,
kwa ufahamu aliziweka mbingu mahali pake;
20 kwa maarifa yake vilindi viligawanywa,
nayo mawingu yanadondosha umande.
 
21 Mwanangu, hifadhi maamuzi mema na busara,
usiache vitoke machoni pako;
22 ndipo vitakapokuwa uzima nafsini mwako
na pambo la neema shingoni mwako.
23 Kisha utaenda katika njia yako salama,
wala mguu wako hautajikwaa;
24 ulalapo, hautaogopa;
ulalapo usingizi wako utakuwa mtamu.
 
25 Usiogope maafa ya ghafula
au maangamizi yanayowapata waovu,
26 kwa kuwa Bwana atakuwa tumaini lako
na kuepusha mguu wako kunaswa katika mtego.
 
27 Usizuie wema kwa wale wanaostahili
ikiwa katika uwezo wako kutenda.
28 Usimwambie jirani yako,
“Njoo baadaye, nitakupa kesho”:
wakati wewe unacho kitu kile karibu nawe.
 
29 Usifanye hila ya kumdhuru jirani yako,
ambaye anaishi karibu na wewe akikuamini.
30 Usimshtaki mtu bila sababu,
wakati hajakutenda dhara lolote.
 
31 Usimwonee wivu mtu mwenye jeuri
wala kuchagua njia yake iwayo yote,
32 kwa kuwa Bwana humchukia mtu mpotovu,
lakini siri yake iko kwa mwenye haki.
 
33 Laana ya Bwana i juu ya nyumba ya mwovu,
lakini yeye huibariki nyumba ya mwenye haki.
34 Huwadhihaki wale wanaodhihaki,
lakini huwapa neema wale wanyenyekevu.
35 Wenye hekima hurithi heshima,
bali huwaaibisha wapumbavu.