7
Onyo Dhidi Ya Mwanamke Mzinzi
1 Mwanangu, shika maneno yangu
na kuzihifadhi amri zangu ndani yako.
2 Shika amri zangu nawe utaishi;
linda mafundisho yangu kama mboni ya jicho lako.
3 Yafunge katika vidole vyako;
yaandike katika kibao cha moyo wako.
4 Mwambie hekima, “Wewe ni dada yangu,”
uite ufahamu jamaa yako;
5 watakuepusha na mwanamke mzinzi,
kutokana na mwanamke mpotovu
na maneno yake ya kubembeleza.
6 Kwenye dirisha la nyumba yangu
nilitazama nje kupitia upenyo
kwenye mwimo wa dirisha.
7 Niliona miongoni mwa wajinga,
nikagundua miongoni mwa wanaume vijana,
kijana asiye na akili.
8 Alikuwa akishuka njiani karibu na pembe ya kwake,
akielekea kwenye nyumba ya huyo mwanamke
9 wakati wa machweo, jua likipungua nuru yake,
giza la usiku lilipokuwa likiingia.
10 Ndipo huyo mwanamke akatoka kumlaki,
hali amevaa kama kahaba akiwa na nia ya udanganyifu.
11 (Ni mwanamke mwenye makelele na mkaidi,
miguu yake haitulii nyumbani;
12 mara kwenye barabara za mji,
mara kwenye viwanja vikubwa,
kwenye kila pembe huvizia.)
13 Huyo mwanamke alimkumbatia kijana na kumbusu,
na kwa uso usio na haya akamwambia:
14 “Nina sadaka za amani nyumbani;
leo nimetimiza nadhiri zangu.
15 Kwa hiyo nimetoka nje kukulaki;
nimekutafuta na nimekupata!
16 Nimetandika kitanda changu
kwa kitani za rangi kutoka Misri.
17 Nimetia manukato kitanda changu
kwa manemane, udi na mdalasini.
18 Njoo, tuzame katika mapenzi mpaka asubuhi;
tujifurahishe wenyewe kwa mapenzi!
19 Mume wangu hayupo nyumbani;
amekwenda safari ya mbali.
20 Amechukua mkoba uliojazwa fedha
na hatakuwepo nyumbani karibuni.”
21 Kwa maneno laini yule mwanamke akampotosha;
alimshawishi kwa maneno yake laini.
22 Mara huyo kijana alimfuata yule mwanamke
kama fahali aendaye machinjoni,
kama kulungu aingiaye kwenye kitanzi,
23 mpaka mshale umchome ini lake,
kama ndege anayenaswa kwenye mtego,
bila kujua itamgharimu maisha yake.
24 Sasa basi wanangu, nisikilizeni;
sikilizeni kwa makini nisemalo.
25 Usiruhusu moyo wako ugeukie njia za huyo mwanamke,
wala usitangetange katika mapito yake.
26 Aliowaangusha ni wengi;
aliowachinja ni kundi kubwa.
27 Nyumba yake ni njia kuu iendayo kaburini,*Kaburini hapa maana yake ni Kuzimu, kwa Kiebrania ni Sheol.
ielekeayo chini kwenye vyumba vya mauti.