12
Mafundisho Ya Kifamilia Na Ya Kijamii
Yeyote apendaye kuadibishwa hupenda maarifa,
bali yeye achukiaye kuonywa ni mpumbavu.
 
Mtu mwema hupata kibali kutoka kwa Bwana,
bali Bwana humhukumu mwenye hila.
 
Mtu hathibitiki kutokana na uovu,
bali mwenye haki hataondolewa.
 
Mke mwenye tabia nzuri ni taji ya mumewe,
bali aaibishaye ni kama uozo
katika mifupa ya mumewe.
 
Mipango ya mtu mwadilifu ni ya haki,
bali ushauri wa mwovu ni udanganyifu.
 
Maneno ya waovu huotea kumwaga damu,
bali maneno ya waadilifu huwaokoa.
 
Watu waovu huondolewa na kutoweka,
bali nyumba ya mwenye haki husimama imara.
 
Mtu husifiwa kulingana na hekima yake,
bali watu wenye akili zilizopotoka hudharauliwa.
 
Heri mtu wa hali ya chini mwenye mtumishi,
kuliko kujifanya mtu wa hali ya juu nawe huna chakula.
 
10 Mtu mwenye haki hujali mahitaji ya mnyama wake,
bali matendo ya huruma ya mwovu ni ukatili.
 
11 Yeye alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele,
bali yeye afuataye mambo ya upuzi hana akili.
 
12 Waovu hutamani mateka ya watu wabaya,
bali shina la mwenye haki hustawi.
 
13 Mtu mwovu hunaswa kwa mazungumzo yake ya dhambi,
bali mwenye haki huepuka taabu.
 
14 Kutokana na tunda la midomo yake
mtu hujazwa na mambo mema,
hakika kama ilivyo kazi ya mikono yake humtunza.
 
15 Njia ya mpumbavu huonekana sawa
machoni pake mwenyewe,
bali mtu mwenye hekima husikiliza ushauri.
 
16 Mpumbavu huonyesha kuudhika kwake mara moja,
bali mtu wa busara hupuuza matukano.
 
17 Shahidi wa kweli hutoa ushuhuda wa kuaminika,
bali shahidi wa uongo husema uongo.
 
18 Maneno ya kipumbavu huchoma kama upanga,
bali ulimi wa mwenye hekima huleta uponyaji.
 
19 Midomo isemayo kweli hudumu milele,
bali ulimi wa uongo hudumu kwa muda mfupi tu.
 
20 Upo udanganyifu katika mioyo
ya wale ambao hupanga mabaya,
bali kuna furaha kwa wale wanaoleta amani.
 
21 Hakuna dhara linalompata mwenye haki,
bali waovu wana taabu nyingi.
 
22 Bwana anachukia sana midomo idanganyayo,
bali hufurahia watu ambao ni wa kweli.
 
23 Mtu mwenye busara hujihifadhia maarifa yeye mwenyewe,
bali moyo wa wapumbavu hububujika upumbavu.
 
24 Mikono yenye bidii itatawala,
bali uvivu huishia katika kazi za utumwa.
 
25 Moyo wa wasiwasi humlemea mtu,
bali neno la huruma humfurahisha.
 
26 Mtu mwenye haki ni mwangalifu katika urafiki,
bali njia ya waovu huwapotosha.
 
27 Mtu mvivu haoki mawindo yake,
bali mtu mwenye bidii ana mali za thamani.
 
28 Katika njia ya haki kuna uzima;
katika mapito hayo kuna maisha ya milele.