Zaburi 92
Wimbo Wa Kumsifu Mungu
Zaburi. Wimbo wa siku ya Sabato.
1 Ni vyema kumshukuru Bwana
na kuliimbia jina lako, Ee Uliye Juu Sana,
2 kuutangaza upendo wako asubuhi,
na uaminifu wako wakati wa usiku,
3 kwa zeze yenye nyuzi kumi
na kwa sauti ya kinubi.
4 Ee Bwana, kwa kuwa matendo yako yamenifurahisha,
nitaziimba kwa shangwe kazi za mikono yako.
5 Ee Bwana, tazama jinsi yalivyo makuu matendo yako,
tazama jinsi yalivyo ya kina mawazo yako!
6 Mjinga hafahamu,
mpumbavu haelewi,
7 ingawa waovu huchipua kama majani
na wote watendao mabaya wanastawi,
wataangamizwa milele.
8 Bali wewe, Ee Bwana,
utatukuzwa milele.
9 Ee Bwana, hakika adui zako,
hakika adui zako wataangamia.
Wote watendao mabaya watatawanyika.
10 Umeitukuza pembe*Pembe inawakilisha nguvu. yangu kama ile ya nyati dume,
mafuta mazuri yamemiminwa juu yangu.
11 Macho yangu yamewaona adui zangu wakishindwa,
masikio yangu yamesikia maangamizi ya adui zangu waovu.
12 Wenye haki watastawi kama mtende,
watakuwa kama mwerezi wa Lebanoni,
13 waliopandwa katika nyumba ya Bwana,
watastawi katika nyua za Mungu wetu.
14 Wakati wa uzee watakuwa bado wanazaa matunda,
watakuwa wabichi tena wamejaa nguvu,
15 wakitangaza, “Bwana ni mkamilifu;
yeye ni Mwamba wangu,
na ndani yake hamna uovu.”