Zaburi 104
Kumsifu Muumba
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.
 
Ee Bwana Mungu wangu, wewe ni mkuu sana,
umejivika utukufu na enzi.
Amejifunika katika nuru kama vile kwa vazi,
amezitandaza mbingu kama hema
na kuziweka nguzo za orofa yake juu ya maji.
Huyafanya mawingu kuwa gari lake,
na hupanda kwenye mbawa za upepo.
Huzifanya pepo kuwa wajumbe*Au: malaika. wake,
miali ya moto watumishi wake.
 
Ameiweka dunia kwenye misingi yake,
haiwezi kamwe kuondoshwa.
Uliifunika kwa kilindi kama kwa vazi,
maji yalisimama juu ya milima.
Lakini kwa kukemea kwako maji yalikimbia,
kwa sauti ya radi yako yakatoroka,
yakapanda milima, yakateremka mabondeni,
hadi mahali pale ulipoyakusudia.
Uliyawekea mpaka ambao hayawezi kuuvuka,
kamwe hayataifunika dunia tena.
 
10 Huzifanya chemchemi zimwage maji mabondeni,
hutiririka kati ya milima.
11 Huwapa maji wanyama wote wa kondeni,
punda-mwitu huzima kiu yao.
12 Ndege wa angani hufanya viota kando ya maji,
huimba katikati ya matawi.
13 Huinyeshea milima kutoka orofa zake,
dunia inatoshelezwa kwa matunda ya kazi yake.
14 Huyafanya majani ya mifugo yaote,
na mimea kwa watu kulima,
wajipatie chakula kutoka ardhini:
15 divai ya kuufurahisha moyo wa mwanadamu,
mafuta kwa ajili ya kungʼarisha uso wake,
na mkate wa kutia mwili nguvu.
16 Miti ya Bwana inanyeshewa vizuri,
mierezi ya Lebanoni aliyoipanda.
17 Humo ndege hufanya viota vyao,
korongo ana nyumba yake kwenye msunobari.
18 Milima mirefu ni makao ya mbuzi-mwitu,
majabali ni kimbilio la pelele.
 
19 Mwezi hugawanya majira,
na jua hutambua wakati wake wa kutua.
20 Unaleta giza, kunakuwa usiku,
wanyama wote wa mwituni huzurura.
21 Simba hunguruma kwa mawindo yao,
na kutafuta chakula chao kutoka kwa Mungu.
22 Jua huchomoza, nao huondoka,
hurudi na kulala katika mapango yao.
23 Kisha mwanadamu huenda kazini mwake,
katika kazi yake mpaka jioni.
 
24 Ee Bwana, jinsi matendo yako yalivyo mengi!
Kwa hekima ulizifanya zote,
dunia imejaa viumbe vyako.
25 Pale kuna bahari, kubwa na yenye nafasi tele,
imejaa viumbe visivyo na idadi,
vitu vyenye uhai vikubwa na vidogo.
26 Huko meli huenda na kurudi,
pia Lewiathani,Lewiathani ni mnyama mkubwa wa baharini mwenye magamba anayefanana na joka kubwa, mwenye umbo la kutisha, asiyeweza kuvuliwa. uliyemuumba acheze ndani yake.
 
27 Hawa wote wanakutazamia wewe,
uwape chakula chao kwa wakati wake.
28 Wakati unapowapa,
wanakikusanya,
unapofumbua mkono wako,
wao wanashibishwa mema.
29 Unapoficha uso wako,
wanapata hofu,
unapoondoa pumzi yao,
wanakufa na kurudi mavumbini.
30 Unapopeleka Roho wako,
wanaumbwa,
nawe huufanya upya uso wa dunia.
 
31 Utukufu wa Bwana na udumu milele,
Bwana na azifurahie kazi zake:
32 yeye aitazamaye dunia, nayo ikatetemeka,
aigusaye milima, nayo ikatoa moshi.
 
33 Nitamwimbia Bwana maisha yangu yote;
nitaimba sifa kwa Mungu wangu muda wote ninaoishi.
34 Kutafakari kwangu na kumpendeze yeye,
ninapofurahi katika Bwana.
35 Lakini wenye dhambi na watoweke katika dunia
na waovu wasiwepo tena.
 
Ee nafsi yangu, msifu Bwana.
 
Msifuni Bwana.Msifuni Bwana kwa Kiebrania ni Hallelu Yah.

*Zaburi 104:4 Au: malaika.

Zaburi 104:26 Lewiathani ni mnyama mkubwa wa baharini mwenye magamba anayefanana na joka kubwa, mwenye umbo la kutisha, asiyeweza kuvuliwa.

Zaburi 104:35 Msifuni Bwana kwa Kiebrania ni Hallelu Yah.