Zaburi 109
Lalamiko La Mtu Aliyeko Kwenye Shida
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.
Ee Mungu, ambaye ninakusifu,
usiwe kimya,
kwa maana watu waovu na wadanganyifu
wamefungua vinywa vyao dhidi yangu;
wasema dhidi yangu
kwa ndimi za udanganyifu.
Wamenizunguka kwa maneno ya chuki,
wananishambulia bila sababu.
Wanachonilipa badala ya urafiki wangu ni kunishtaki,
lakini mimi ninawaombea.
Wananilipiza mabaya kwa mema,
chuki badala ya urafiki wangu.
 
Agiza mtu mwovu ampinge,
mshtaki*Mshtaki hapa maana yake ni Shetani. asimame mkono wake wa kuume.
Anapohukumiwa, apatikane na hatia,
nayo maombi yake yamhukumu.
Siku zake za kuishi na ziwe chache,
nafasi yake ya uongozi ichukuliwe na mtu mwingine.
Watoto wake na waachwe yatima,
mke wake na awe mjane.
10 Watoto wake na watangetange wakiomba,
na wafukuzwe kwenye magofu ya nyumba zao.
11 Mtu anayemdai na ateke vyote alivyo navyo,
matunda ya kazi yake yatekwe nyara na wageni.
12 Asiwepo mtu yeyote wa kumtendea mema
wala wa kuwahurumia yatima wake.
13 Uzao wake na ukatiliwe mbali,
majina yao yafutike katika kizazi kifuatacho.
14 Maovu ya baba zake na yakumbukwe
mbele za Bwana,
dhambi ya mama yake
isifutwe kamwe.
15 Dhambi zao na zibaki daima mbele za Bwana,
ili apate kukatilia mbali kumbukumbu lao duniani.
 
16 Kwa maana kamwe hakuweza kutenda wema,
bali alimfukuza mnyonge na mhitaji,
aliwafanyia jeuri wahitaji na waliovunjika moyo.
17 Alipenda kulaani,
nayo laana ikampata;
hakupenda kubariki,
kwa hiyo baraka na ikae mbali naye.
18 Alivaa kulaani kama vazi lake,
nayo laana ikamwingia mwilini mwake kama maji,
kwenye mifupa yake kama mafuta.
19 Na iwe kama joho alilozungushiwa,
kama mshipi aliofungiwa daima.
20 Haya na yawe malipo ya Bwana kwa washtaki wangu,
kwa wale wanaoninenea mabaya.
 
21 Lakini wewe, Ee Bwana Mwenyezi,
unitendee wema kwa ajili ya jina lako,
uniokoe kwa wema wa pendo lako.
22 Maana mimi ni maskini na mhitaji,
moyo wangu umejeruhiwa ndani yangu.
23 Ninafifia kama kivuli cha jioni,
nimerushwa-rushwa kama nzige.
24 Magoti yangu yamelegea kwa kufunga,
mwili wangu umedhoofika na kukonda.
25 Nimekuwa kitu cha kudharauliwa kwa washtaki wangu,
wanionapo, hutikisa vichwa vyao.
 
26 Ee Bwana, Mungu wangu nisaidie,
niokoe sawasawa na upendo wako.
27 Watu na wafahamu kuwa ni mkono wako,
kwamba wewe, Ee Bwana, umetenda hili.
28 Wanaweza kulaani, lakini wewe utabariki,
watakaposhambulia wataaibishwa,
lakini mtumishi wako atashangilia.
29 Washtaki wangu watavikwa fedheha,
na kufunikwa na aibu kama joho.
 
30 Kwa kinywa changu nitamtukuza sana Bwana,
katika umati mkubwa nitamsifu.
31 Kwa maana husimama mkono wa kuume wa mhitaji,
kuokoa maisha yake kutoka kwa wale wanaomhukumu.

*Zaburi 109:6 Mshtaki hapa maana yake ni Shetani.