*Zaburi hii imetungwa kila mstari (ikiwa ni pamoja na 13b) ukianzia na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22.
Zaburi 145
Wimbo Wa Kusifu Ukuu Na Wema Wa Mungu
Wimbo wa Sifa. Wa Daudi.
Nitakutukuza wewe, Mungu wangu Mfalme,
nitalisifu jina lako milele na milele.
Kila siku nitakusifu
na kulitukuza jina lako milele na milele.
 
Bwana ni mkuu, anayestahili kusifiwa sana,
ukuu wake haupimiki.
Kizazi kimoja kitasifia kazi zako kwa kizazi kingine,
watasimulia matendo yako makuu.
Watasema juu ya utukufu wa fahari ya ukuu wako,
nami nitatafakari juu ya kazi zako za ajabu.
Watasimulia uwezo wa kazi zako za kutisha,
nami nitatangaza matendo yako makuu.
Wataadhimisha wema wako mwingi,
na wataimba kwa shangwe juu ya haki yako.
 
Bwana ni mwenye neema na mwingi wa huruma,
si mwepesi wa hasira, bali ni mwingi wa upendo.
Bwana ni mwema kwa wote,
ana huruma kwa vyote alivyovifanya.
10 Ee Bwana, vyote ulivyovifanya vitakusifu,
watakatifu wako watakutukuza.
11 Watasimulia utukufu wa ufalme wako
na kusema juu ya ukuu wako,
12 ili watu wote wajue matendo yako makuu
na utukufu wa fahari ya ufalme wako.
13 Ufalme wako ni ufalme wa milele,
mamlaka yako hudumu vizazi vyote.
 
Bwana ni mwaminifu kwa ahadi zake zote
na mwenye upendo kwa vyote alivyovifanya.
14 Bwana huwategemeza wote waangukao,
na huwainua wote waliolemewa na mizigo yao.
15 Macho yao wote yanakutazama wewe,
nawe huwapa chakula chao wakati wake.
16 Waufumbua mkono wako,
watosheleza haja ya kila kitu kilicho hai.
 
17 Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote,
na mwenye upendo kwa vyote alivyovifanya.
18 Bwana yu karibu na wote wamwitao,
karibu na wote wamwitao kwa uaminifu.
19 Huwatimizia wamchao matakwa yao,
husikia kilio chao na kuwaokoa.
20 Bwana huwalinda wote wampendao,
bali waovu wote atawaangamiza.
 
21 Kinywa changu kitazinena sifa za Bwana.
Kila kiumbe na kilisifu jina lake takatifu
milele na milele.

*^ Zaburi hii imetungwa kila mstari (ikiwa ni pamoja na 13b) ukianzia na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22.