16
Mabakuli Saba Ya Ghadhabu Ya Mungu
Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka mle Hekaluni ikiwaambia wale malaika saba, “Nendeni, mkayamwage duniani hayo mabakuli saba ya ghadhabu ya Mungu.”
Malaika wa kwanza akaenda akalimwaga hilo bakuli lake juu ya nchi. Majipu mabaya yenye maumivu makali yakawapata wale watu wote waliokuwa na chapa ya yule mnyama na walioabudu sanamu yake.
Malaika wa pili akalimwaga bakuli lake baharini, nayo ikabadilika kuwa damu kama ya mtu aliyekufa na kila kiumbe hai kilichokuwa ndani ya bahari kikafa.
Malaika wa tatu akalimwaga bakuli lake katika mito na chemchemi za maji, nazo zikawa damu. Ndipo nikamsikia malaika msimamizi wa maji akisema:
“Wewe una haki katika hukumu hizi ulizotoa,
wewe uliyeko, uliyekuwako, Uliye Mtakatifu,
kwa sababu umehukumu hivyo;
kwa kuwa walimwaga damu ya watakatifu wako
na manabii wako,
nawe umewapa damu wanywe
kama walivyostahili.”
Nikasikia madhabahu ikiitikia,
“Naam, Bwana Mungu Mwenyezi,
hukumu zako ni kweli na haki.”
Malaika wa nne akamimina bakuli lake kwenye jua, nalo likapewa nguvu za kuwaunguza watu kwa moto. Watu wakaunguzwa na hilo joto kali, wakalaani Jina la Mungu, aliyekuwa na uwezo juu ya mapigo haya, tena wakakataa kutubu na kumtukuza Mungu.
10 Malaika wa tano akamimina bakuli lake kwenye kiti cha enzi cha yule mnyama, nao ufalme wake ukagubikwa na giza. Watu wakatafuna ndimi zao kwa ajili ya maumivu, 11 wakamlaani Mungu wa mbinguni kwa sababu ya maumivu na majeraha yao, wala hawakutubu kwa ajili ya matendo yao maovu.
12 Malaika wa sita akamimina bakuli lake kwenye mto mkubwa Frati, maji yake yakakauka ili kutayarisha njia kwa ajili ya wafalme watokao Mashariki. 13 Kisha nikaona roho wachafu watatu waliofanana na vyura wakitoka katika kinywa cha lile joka na katika kinywa cha yule mnyama na katika kinywa cha yule nabii wa uongo. 14 Hizo ndizo roho za pepo wachafu zitendazo miujiza. Nazo huwaendea wafalme wa ulimwengu wote na kuwakusanya tayari kwa ajili ya vita katika siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi.
15  “Tazama, naja kama mwizi! Amebarikiwa yeye akeshaye na kuziweka tayari nguo zake ili asiende uchi na kuonekana aibu yake.”
16 Ndipo wakawakusanya wafalme pamoja mahali paitwapo Armagedoni* Armagedoni au Har-Magedoni ina maana Mlima Megido, mahali pa kinabii ambapo wafalme wote wa dunia watakusanyika kwa vita katika siku ya Mungu Mwenyezi. kwa Kiebrania.
17 Malaika wa saba akamimina bakuli lake angani na sauti kubwa ikatoka mle hekaluni katika kile kiti cha enzi, ikisema, “Imekwisha kuwa!” 18 Kukawa na mianga ya umeme wa radi, ngurumo, radi na tetemeko kubwa la ardhi. Hapajawa kamwe na tetemeko la ardhi kama hilo tangu mwanadamu awepo duniani, hivyo lilikuwa tetemeko kubwa ajabu. 19 Ule mji mkubwa ukagawanyika katika sehemu tatu, nayo miji ya mataifa ikaanguka. Mungu akaukumbuka Babeli Mkuu na kumpa kikombe kilichojaa mvinyo wa ghadhabu ya hasira yake. 20 Kila kisiwa kikatoweka wala milima haikuonekana. 21 Mvua kubwa ya mawe yenye uzito wa talanta moja Talanta moja ni kama kilo 34. ikashuka kutoka mbinguni, ikawaangukia wanadamu. Nao wanadamu wakamlaani Mungu kwa ajili ya hayo mapigo ya mvua ya mawe, kwa sababu pigo hilo lilikuwa la kutisha.

*16:16 Armagedoni au Har-Magedoni ina maana Mlima Megido, mahali pa kinabii ambapo wafalme wote wa dunia watakusanyika kwa vita katika siku ya Mungu Mwenyezi.

16:21 Talanta moja ni kama kilo 34.