16
Salamu Kwa Watu Binafsi
Napenda kumtambulisha kwenu dada yetu Foibe, mtumishi katika kanisa la Kenkrea. Naomba mpokeeni katika Bwana ipasavyo watakatifu na kumpa msaada wowote atakaohitaji kutoka kwenu, kwa maana yeye amekuwa msaada kwa watu wengi, mimi nikiwa miongoni mwao.
 
Wasalimuni Prisila*Prisila kwa Kiyunani ni Priska, hivyo tafsiri nyingine zimemuita Priska. na Akila, watumishi wenzangu katika Kristo Yesu. Wao walihatarisha maisha yao kwa ajili yangu; wala si mimi tu ninayewashukuru bali pia makanisa yote ya watu wa Mataifa.
Lisalimuni pia kanisa linalokutana nyumbani mwao.
Msalimuni rafiki yangu mpendwa Epaineto, aliyekuwa mtu wa kwanza kumwamini Kristo huko Asia.
Msalimuni Maria, aliyefanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu.
Wasalimuni Androniko na Yunia, jamaa zangu ambao wamekuwa gerezani pamoja nami. Wao ni maarufu miongoni mwa mitume, nao walikuwa katika Kristo kabla yangu.
Msalimuni Ampliato, yeye nimpendaye katika Bwana.
Msalimuni Urbano, mtendakazi mwenzetu katika Kristo, pamoja na rafiki yangu mpendwa Stakisi.
10 Msalimuni Apele aliyejaribiwa na akaithibitisha imani yake katika Kristo.
Wasalimuni wote walio nyumbani mwa Aristobulo.
11 Msalimuni ndugu yangu Herodioni.
Wasalimuni wote walio nyumbani mwa Narkisi walio katika Bwana.
12 Wasalimuni Trifaina na Trifosa, wale wanawake wanaofanya kazi kwa bidii katika Bwana.
Msalimuni rafiki yangu mpendwa Persisi, mwanamke mwingine aliyefanya kazi kwa bidii katika Bwana.
13 Msalimuni Rufo, mteule katika Bwana, pamoja na mama yake, ambaye amekuwa mama kwangu pia.
14 Wasalimuni Asinkrito, Flegoni, Herme, Patroba, Herma na ndugu wote walio pamoja nao.
15 Wasalimuni Filologo, Yulia, Nerea na dada yake, na Olimpa na watakatifu wote walio pamoja nao.
16 Salimianeni ninyi kwa ninyi kwa busu takatifu.
Makanisa yote ya Kristo yanawasalimu.
Maelekezo Ya Mwisho
17 Ndugu zangu, nawasihi mjihadhari na kujiepusha na wale watu waletao matengano na kuweka vikwazo mbele yenu dhidi ya mafundisho mliyojifunza. 18 Kwa maana watu kama hao hawamtumikii Bwana Kristo, bali wanatumikia tamaa zao wenyewe. Kwa kutumia maneno laini na ya kubembeleza, hupotosha mioyo ya watu wajinga. 19 Kila mtu amesikia juu ya utii wenu, nami nimejawa na furaha tele kwa ajili yenu. Lakini nataka mwe na hekima katika mambo mema na bila hatia katika mambo maovu.
20 Mungu wa amani atamponda Shetani chini ya miguu yenu upesi.
Neema ya Bwana wetu Yesu iwe nanyi. Amen.
21 Timotheo, mtendakazi mwenzangu anawasalimu. Vivyo hivyo Lukio, Yasoni, na Sosipatro, ndugu zangu.
22 Mimi, Tertio, niliye mwandishi wa waraka huu, nawasalimu katika Bwana.
23 Gayo, ambaye ni mwenyeji wangu na wa kanisa lote, anawasalimu.
Erasto, mweka hazina wa mji huu, pamoja na Kwarto ndugu yetu pia wanawasalimu.
[ 24 Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe pamoja nanyi nyote. Amen.]
Maneno Ya Mwisho Ya Kumsifu Mungu
25 Sasa atukuzwe yeye awezaye kuwafanya ninyi imara kwa Injili yangu na kuhubiriwa kwa Yesu Kristo, kutokana na kufunuliwa siri zilizofichika tangu zamani za kale. 26 Lakini sasa siri hiyo imefunuliwa na kujulikana kupitia maandiko ya kinabii kutokana na amri ya Mungu wa milele, ili mataifa yote yaweze kumwamini na kumtii 27 Mungu aliye pekee, mwenye hekima, ambaye kwa njia ya Yesu Kristo utukufu ni wake milele na milele! Amen.

*16:3 Prisila kwa Kiyunani ni Priska, hivyo tafsiri nyingine zimemuita Priska.