Wimbo Ulio Bora
1
Wimbo ulio bora wa Solomoni.
 
Shairi La Kwanza
Mpendwa
Unibusu kwa busu la kinywa chako,
kwa maana upendo wako unafurahisha kuliko divai.
Manukato yako yananukia vizuri,
jina lako ni kama manukato yaliyomiminwa.
Ndiyo sababu wanawali wanakupenda!
Nichukue twende nawe, na tufanye haraka!
Mfalme na anilete ndani ya vyumba vyake.
Marafiki
Tunakushangilia na kukufurahia,
tutasifu upendo wako zaidi kuliko divai.
Mpendwa
Tazama jinsi ilivyo bora wakupende!
Mimi ni mweusi, lakini napendeza,
enyi binti za Yerusalemu,
mweusi kama mahema ya Kedari,
kama mapazia ya hema la Solomoni.
Usinikazie macho kwa sababu mimi ni mweusi,
kwa sababu nimefanywa mweusi na jua.
Wana wa mama yangu walinikasirikia
na kunifanya niwe mtunza mashamba ya mizabibu.
Shamba langu mwenyewe la mizabibu nimeliacha.
Niambie, wewe ambaye ninakupenda,
unalisha wapi kundi lako la kondoo
na ni wapi unapowapumzisha kondoo wako adhuhuri.
Kwa nini niwe kama mwanamke aliyefunikwa shela
karibu na makundi ya rafiki zako?
Marafiki
Kama hujui, ewe mwanamke mzuri kuliko wote,
fuata nyayo za kondoo,
na kulisha wana-mbuzi wako
karibu na hema za wachungaji.
Mpenzi
Mpenzi wangu, ninakufananisha na farasi jike
aliyefungwa katika mojawapo ya magari ya vita ya Farao.
10 Mashavu yako yanapendeza yakiwa na vipuli,
shingo yako ikiwa na mikufu ya vito.
11 Tutakufanyia vipuli vya dhahabu,
vyenye kupambwa kwa fedha.
Mpendwa
12 Wakati mfalme alipokuwa mezani pake,
manukato yangu yalisambaza harufu yake nzuri.
13 Mpenzi wangu kwangu mimi ni kifuko cha manemane
kati ya matiti yangu.
14 Mpenzi wangu kwangu mimi ni kama kishada cha maua ya mhina
kutoka mashamba ya mizabibu ya En-Gedi.
Mpenzi
15 Tazama jinsi ulivyo mzuri, mpenzi wangu!
Tazama jinsi ulivyo mzuri!
Macho yako ni kama ya hua.
Mpendwa
16 Tazama jinsi ulivyo mzuri, mpenzi wangu!
Ee, tazama jinsi unavyopendeza!
Na kitanda chetu ni cha majani mazuri.
Mpenzi
17 Nguzo za nyumba yetu ni mierezi,
na mapao yetu ni miberoshi.