8
Laiti ungelikuwa kwangu kama ndugu wa kiume,
ambaye aliyanyonya matiti ya mama yangu!
Kisha, kama ningekukuta huko nje,
ningelikubusu,
wala hakuna mtu yeyote angelinidharau.
Ningelikuongoza na kukuleta
katika nyumba ya mama yangu,
yeye ambaye amenifundisha.
Ningelikupa divai iliyokolezwa unywe,
asali ya maua ya mikomamanga yangu.
Mkono wake wa kushoto uko chini ya kichwa changu,
na mkono wake wa kuume unanikumbatia.
Binti za Yerusalemu, ninawaagiza:
msichochee wala kuamsha mapenzi
hata yatakapotaka yenyewe.
 
Shairi La Sita
Marafiki
Ni nani huyu anayekuja kutoka nyikani
akimwegemea mpenzi wake?
Mpendwa
Nilikuamsha chini ya mtofaa,
huko mama yako alipotunga mimba yako,
huko yeye alipata utungu akakuzaa.
Nitie kama muhuri moyoni mwako,
kama muhuri kwenye mkono wako;
kwa maana upendo una nguvu kama mauti,
wivu wake ni mkatili kama kuzimu.
Unachoma kama mwali wa moto,
kama mwali mkubwa wa moto wa Bwana hasa.
Maji mengi hayawezi kuuzimisha upendo,
mito haiwezi kuugharikisha.
Kama mtu angelitoa mali yote ya nyumbani mwake
kwa ajili ya upendo,
angelidharauliwa kabisa.
Marafiki
Tunaye dada mdogo,
matiti yake hayajakua bado.
Tutafanya nini kwa ajili ya dada yetu
wakati atakapokuja kuposwa?
Kama yeye ni ukuta,
tutajenga minara ya fedha juu yake.
Na kama yeye ni mlango,
tutamzungushia mbao za mierezi.
Mpendwa
10 Mimi ni ukuta,
nayo matiti yangu ni kama minara.
Ndivyo ambavyo nimekuwa machoni pake
kama yule anayeleta utoshelevu.
11 Solomoni alikuwa na shamba la mizabibu huko Baal-Hamoni;
alikodisha shamba lake la mizabibu kwa wapangaji.
Kila mmoja angeleta kwa ajili ya matunda yake
shekeli 1,000* Shekeli 1,000 ni kama kilo 11.5. za fedha.
12 Lakini shamba langu la mizabibu
ambalo ni langu mwenyewe
ni langu kutoa;
hizo shekeli 1,000 ni kwa ajili yako, ee Solomoni,
na shekeli mia mbili Shekeli 200 ni kama kilo 2.3. ni kwa ajili
ya wale wanaotunza matunda yake.
Mpenzi
13 Wewe ukaaye bustanini
pamoja na marafiki mliohudhuria,
hebu nisikie sauti yako!
Mpendwa
14 Njoo, mpenzi wangu,
uwe kama swala
au kama ayala kijana
juu ya milima iliyojaa vikolezo.

*8:11 Shekeli 1,000 ni kama kilo 11.5.

8:12 Shekeli 200 ni kama kilo 2.3.