2
Maono Ya Tatu: Mtu Mwenye Kamba Ya Kupimia
Kisha nikatazama juu: pale mbele yangu alikuwepo mtu mwenye kamba ya kupimia mkononi mwake! Nikamuuliza, “Unakwenda wapi?”
Akanijibu, “Kupima Yerusalemu, kupata urefu na upana wake.”
Kisha malaika aliyekuwa akizungumza nami akaondoka, malaika mwingine akaja kukutana naye na kumwambia: “Kimbia, umwambie yule kijana, ‘Yerusalemu utakuwa mji usio na kuta kwa sababu ya wingi wa watu na mifugo iliyomo. Mimi mwenyewe nitakuwa ukuta wa moto kuuzunguka,’ asema Bwana, ‘nami nitakuwa utukufu wake ndani yake.’
“Njooni! Njooni! Kimbieni mtoke katika nchi ya kaskazini,” asema Bwana, “Kwa kuwa nimewatawanya kwenye pande nne za mbingu,” asema Bwana.
“Njoo, ee Sayuni! Kimbia, wewe ukaaye ndani ya Binti Babeli!” Kwa kuwa hivi ndivyo asemavyo Bwana Mwenye Nguvu Zote: “Baada ya yeye kuniheshimu na kunituma mimi dhidi ya mataifa yaliyokuteka nyara, kwa kuwa yeyote awagusaye ninyi, anaigusa mboni ya jicho lake, hakika nitauinua mkono wangu dhidi yao ili watumwa wao wawateke nyara. Ndipo mtakapojua ya kwamba Bwana Mwenye Nguvu Zote amenituma.
10 “Piga kelele na ufurahie, ee Binti Sayuni, kwa maana ninakuja, nami nitaishi miongoni mwenu,” asema Bwana. 11 “Mataifa mengi yataunganishwa na Bwana siku hiyo, nao watakuwa watu wangu. Nitaishi miongoni mwenu nanyi mtajua kwamba Bwana Mwenye Nguvu Zote amenituma kwenu. 12 Bwana atairithi Yuda kama fungu lake katika nchi takatifu na atachagua tena Yerusalemu. 13 Tulieni mbele za Bwana, enyi watu wote, kwa sababu ameinuka kutoka makao yake matakatifu.”