6
Maono Ya Nane: Magari Manne Ya Vita
Nikatazama juu tena: nikaona mbele yangu magari manne ya vita yakija kutoka kati ya milima miwili, milima ya shaba! Gari la kwanza lilivutwa na farasi wekundu, la pili lilivutwa na farasi weusi, la tatu lilivutwa na farasi weupe na gari la nne lilivutwa na farasi wa madoadoa ya kijivu, wote wenye nguvu. Nikamuuliza malaika aliyekuwa akizungumza nami, “Hawa ni nani bwana wangu?”
Malaika akanijibu, “Hizi ni roho nne za mbinguni zisimamazo mbele ya uwepo wa Bwana wa dunia yote, zinatoka kwenda kufanya kazi yake. Gari linalovutwa na farasi weusi linaelekea katika nchi ya kaskazini, la farasi weupe linaelekea magharibi na la farasi wa madoadoa ya kijivu linaelekea kusini.”
Wakati hao farasi wenye nguvu walipokuwa wakitoka, walikuwa wakijitahidi kwenda duniani kote. Akasema, “Nenda duniani kote!” Kwa hiyo wakaenda duniani kote.
Kisha akaniita, “Tazama, wale wanaokwenda kuelekea nchi ya kaskazini wamepumzisha Roho yangu katika nchi ya kaskazini.”
Taji Kwa Ajili Ya Yoshua
Neno la Bwana likanijia kusema: 10 “Chukua fedha na dhahabu kutoka kwa watu waliohamishwa, yaani Heldai, Tobia na Yedaya ambao wamefika kutoka Babeli. Siku iyo hiyo nenda nyumbani kwa Yosia mwana wa Sefania. 11 Chukua fedha na dhahabu utengeneze taji, nawe uiweke kichwani mwa kuhani mkuu Yoshua, mwana wa Yehosadaki. 12 Umwambie, hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote: ‘Huyu ndiye mtu ambaye jina lake ni Tawi, naye atachipua kutoka mahali pake na kujenga Hekalu la Bwana. 13 Ni yeye atakayejenga Hekalu la Bwana, naye atavikwa utukufu na ataketi kumiliki katika kiti cha enzi naye atakuwa kuhani katika kiti chake cha enzi. Hapo patakuwa amani kati ya hao wawili.’ 14 Taji itatolewa kwa Heldai, Tobia, Yedaya na Heni mwana wa Sefania kama kumbukumbu ndani ya Hekalu la Bwana. 15 Wale walio mbali sana watakuja na kusaidia kulijenga Hekalu la Bwana, nanyi mtajua ya kwamba Bwana Mwenye Nguvu Zote amenituma kwenu. Hili litatokea ikiwa mtamtii Bwana Mungu wenu kwa bidii.”