Sefania
1
Neno la Bwana lililomjia Sefania mwana wa Kushi, mwana wa Gedalia, mwana wa Amaria, mwana wa Hezekia, wakati wa utawala wa Yosia mwana wa Amoni mfalme wa Yuda:
 
Onyo La Maangamizi Yanayokuja
Bwana asema,
“Nitafagia kila kitu
kutoka kwenye uso wa dunia.”
“Nitafagilia mbali watu na wanyama;
nitafagilia mbali ndege wa angani
na samaki wa baharini.
Wafanyao maovu watapata tu kokoto,
nami nitamkatilia mbali mwanadamu atoke katika dunia,”
asema Bwana.
Dhidi Ya Yuda
“Nitaiadhibu Yuda
na wote wakaao Yerusalemu.
Kutoka mahali hapa nitakatilia mbali
kila mabaki ya Baali,
majina ya wapagani na makuhani
waabuduo sanamu:
wale ambao husujudu juu ya mapaa
kuabudu jeshi la vitu vya angani,
wale ambao husujudu na kuapa kwa Bwana
na ambao pia huapa kwa Malkamu,
wale wanaoacha kumfuata Bwana,
wala hawamtafuti Bwana
wala kutaka shauri lake.
Nyamazeni mbele za Bwana Mwenyezi,
kwa maana siku ya Bwana iko karibu.
Bwana ameandaa dhabihu,
amewaweka wakfu wale aliowaalika.
Katika siku ya dhabihu ya Bwana
nitawaadhibu wakuu
na wana wa mfalme
na wale wote wanaovaa
nguo za kigeni.
Katika siku hiyo nitaadhibu wote ambao
hukwepa kukanyaga kizingiti,
ambao hujaza hekalu la miungu yao
kwa dhuluma na udanganyifu.”
 
10 Bwana asema, “Katika siku hiyo
kilio kitapanda juu kutoka lango la Samaki,
maombolezo kutoka mtaa wa pili,
na mshindo mkubwa kutoka vilimani.
11 Ombolezeni, ninyi mnaoishi katika eneo la sokoni;
wafanyabiashara wenu wote wameangamizwa,
wote ambao wanafanya biashara ya fedha
wataangamizwa.
12 Wakati huo nitasaka mji wa Yerusalemu kwa taa,
na kuwaadhibu wale ambao
wanakaa katika hali ya kuridhika,
ambao ni kama divai
iliyobaki kwenye machicha,
ambao hudhani, ‘Bwana hatafanya lolote,
jema au baya.’
13 Utajiri wao utatekwa nyara,
nyumba zao zitabomolewa.
Watajenga nyumba,
lakini hawataishi ndani yake;
watapanda mizabibu
lakini hawatakunywa divai yake.
Siku Kubwa Ya Bwana
14 “Siku kubwa ya Bwana iko karibu:
iko karibu na inakuja haraka.
Sikilizeni! Kilio katika siku ya Bwana
kitakuwa kichungu,
hata shujaa atapiga kelele.
15 Siku ile ni siku ya ghadhabu,
siku ya fadhaa na dhiki,
siku ya uharibifu na ukiwa,
siku ya giza na utusitusi,
siku ya mawingu na giza nene,
16 siku ya tarumbeta na mlio wa vita
dhidi ya miji yenye ngome
na dhidi ya minara mirefu.
17 Nitawaletea watu dhiki,
nao watatembea kama vipofu,
kwa sababu wametenda dhambi
dhidi ya Bwana.
Damu yao itamwagwa kama vumbi
na matumbo yao kama taka.
18 Fedha yao wala dhahabu yao
hazitaweza kuwaokoa
katika siku hiyo ya ghadhabu ya Bwana.
Katika moto wa wivu wake
dunia yote itateketezwa,
kwa maana ataleta mwisho
wa wote wanaoishi katika dunia ghafula.”