3
Hatima Ya Yerusalemu
Ole mji wa wadhalimu,
waasi na waliotiwa unajisi!
Hautii mtu yeyote,
haukubali maonyo.
Haumtumaini Bwana,
haukaribii karibu na Mungu wake.
Maafisa wake ni simba wangurumao,
watawala wake ni mbwa mwitu wa jioni,
ambao hawabakizi chochote
kwa ajili ya asubuhi.
Manabii wake ni wenye kiburi,
ni wadanganyifu.
Makuhani wake hunajisi patakatifu
na kuihalifu sheria.
Bwana aliye ndani yake ni mwenye haki,
hafanyi kosa.
Asubuhi kwa asubuhi hutoa haki yake,
kila kukipambazuka huitimiza,
bali mtu dhalimu hana aibu.
 
“Nimeyafutilia mbali mataifa,
ngome zao zimebomolewa.
Nimeziacha barabara ukiwa,
hakuna anayepita humo.
Miji yao imeharibiwa;
hakuna mmoja atakayeachwa:
hakuna hata mmoja.
Niliuambia huo mji,
‘Hakika utaniogopa na kukubali maonyo!’
Ndipo makao yake hayatafutiliwa mbali,
wala adhabu zangu zote hazitakuja juu yake.
Lakini walikuwa bado na shauku
kutenda kwa upotovu katika yote waliyofanya.”
Bwana anasema,
“Kwa hiyo ningojee mimi,
siku nitakayosimama kuteka nyara.
Nimeamua kukusanya mataifa,
kukusanya falme
na kumimina ghadhabu yangu juu yao,
hasira yangu kali yote.
Dunia yote itateketezwa
kwa moto wa wivu wa hasira yangu.
 
“Ndipo nitatakasa midomo ya mataifa,
kwamba wote waweze kuliitia jina la Bwana
na kumtumikia kwa pamoja.
10 Kutoka ngʼambo ya mito ya Kushi
watu wangu wanaoniabudu,
watu wangu waliotawanyika,
wataniletea sadaka.
11 Siku hiyo hutaaibishwa
kwa ajili ya makosa yote ulionitendea,
kwa sababu nitawaondoa kutoka mji huu
wale wote wanaoshangilia
katika kiburi chao.
Kamwe hutajivuna tena
katika kilima changu kitakatifu.
12 Lakini nitakuachia ndani yako
wapole na wanyenyekevu,
ambao wanatumaini jina la Bwana.
13 Mabaki ya Israeli hayatafanya kosa;
hawatasema uongo,
wala udanganyifu hautakuwa
katika vinywa vyao.
Watakula na kulala
wala hakuna yeyote
atakayewaogopesha.”
 
14 Imba, ee Binti Sayuni;
paza sauti, ee Israeli!
Furahi na kushangilia kwa moyo wako wote,
ee Binti Yerusalemu!
15 Bwana amekuondolea adhabu yako,
amewarudisha nyuma adui zako.
Bwana, Mfalme wa Israeli, yu pamoja nawe;
kamwe hutaogopa tena madhara yoyote.
16 Katika siku hiyo watauambia Yerusalemu,
“Usiogope, ee Sayuni;
usiiache mikono yako ilegee.
17 Bwana Mungu wako yu pamoja nawe,
yeye ni mwenye nguvu kuokoa.
Atakufurahia kwa furaha kubwa,
atakutuliza kwa pendo lake,
atakufurahia kwa kuimba.”
 
18 “Huzuni katika sikukuu zilizoamriwa
nitaziondoa kwenu;
hizo ni mzigo na fedheha kwenu.
19 Wakati huo nitawashughulikia
wote waliokudhulumu;
nitaokoa vilema na kukusanya
wale ambao wametawanywa.
Nitawapa sifa na heshima
katika kila nchi ambayo waliaibishwa.
20 Wakati huo nitawakusanya;
wakati huo nitawaleta nyumbani.
Nitawapa sifa na heshima
miongoni mwa mataifa yote ya dunia
wakati nitakapowarudishia mateka yenu
mbele ya macho yenu hasa,”
asema Bwana.