16
Sanduku lawekwa ndani ya hema
Wakaleta Sanduku la Mungu na kuliweka ndani ya hema ambalo Daudi alikuwa amelisimamisha kwa ajili yake, na wakatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani mbele za Mungu. Baada ya Daudi kumaliza kutoa hizo sadaka za kuteketezwa na hizo sadaka za amani, akawabariki watu katika jina la Mwenyezi Mungu. Kisha akamgawia kila Mwisraeli mwanaume na mwanamke mkate, andazi la tende na andazi la zabibu kavu.
Akawaweka pia baadhi ya Walawi ili wahudumu mbele ya Sanduku la Mwenyezi Mungu kufanya maombi, kumshukuru na kumsifu Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: Asafu ndiye alikuwa mkuu wao, akisaidiwa na Zekaria, Yeieli, Shemiramothi, Yehieli, Matithia, Eliabu, Benaya, Obed-Edomu na Yeieli. Hawa ndio wangepiga zeze na vinubi, Asafu angepiga matoazi, nao Benaya na Yahazieli makuhani, ndio wangepiga tarumbeta mara kwa mara mbele ya Sanduku la Agano la Mungu.
Zaburi ya Daudi ya shukrani
(Zaburi 105:1-15; 96:1-13; 106:1, 47-48)
Siku ile, kitu cha kwanza Daudi alichofanya ni kumkabidhi Asafu na wenzake zaburi hii ya shukrani kwa Mwenyezi Mungu:
Mshukuruni Mwenyezi Mungu, liitieni jina lake;
wajulisheni mataifa yale aliyoyatenda.
Mwimbieni yeye, mwimbieni yeye sifa;
waambieni matendo yake yote ya ajabu.
10 Lishangilieni jina lake takatifu;
mioyo ya wale wanaomtafuta Mwenyezi Mungu na ifurahi.
11 Mtafuteni Mwenyezi Mungu na nguvu zake;
utafuteni uso wake siku zote.
12 Kumbuka matendo ya ajabu aliyoyafanya,
miujiza yake na hukumu alizozitamka,
13 enyi wazao wa Israeli mtumishi wake,
enyi wana wa Yakobo, wateule wake.
14 Yeye ndiye Mwenyezi Mungu, Mungu wetu;
hukumu zake ziko duniani kote.
15 Hulikumbuka agano lake milele,
neno ambalo aliamuru, kwa vizazi elfu,
16 agano alilolifanya na Ibrahimu,
kiapo alichomwapia Isaka.
17 Alilithibitisha kwa Yakobo kuwa amri,
kwa Israeli liwe agano la milele:
18 “Nitakupa wewe nchi ya Kanaani
kuwa sehemu utakayoirithi.”
 
19 Walipokuwa wachache kwa idadi,
wachache sana na wageni ndani yake,
20 walitangatanga kutoka taifa moja hadi lingine,
kutoka ufalme mmoja hadi mwingine.
21 Hakuruhusu mtu yeyote awadhulumu;
kwa ajili yao aliwakemea wafalme, akisema:
22 “Msiwaguse niliowapaka mafuta;
msiwadhuru manabii wangu.”
 
23 Mwimbieni Mwenyezi Mungu dunia yote;
tangazeni wokovu wake siku baada ya siku.
24 Tangazeni utukufu wake katika mataifa,
matendo yake ya ajabu miongoni mwa mataifa yote.
25 Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ni mkuu,
mwenye kustahili kusifiwa kuliko wote;
yeye ni wa kuogopwa kuliko miungu yote.
26 Kwa maana miungu yote ya mataifa ni sanamu,
lakini Mwenyezi Mungu aliziumba mbingu.
27 Fahari na enzi viko mbele yake;
nguvu na utukufu vimo patakatifu pake.
28 Mpeni Mwenyezi Mungu, enyi jamaa za mataifa,
mpeni Mwenyezi Mungu utukufu na nguvu,
29 mpeni Mwenyezi Mungu utukufu unaostahili jina lake.
Leteni sadaka na mje katika nyua zake.
Mwabuduni Mwenyezi Mungu katika uzuri wa utakatifu wake.
30 Dunia yote na itetemeke mbele zake!
Ulimwengu ameuweka imara; hauwezi kusogezwa.
31 Mbingu na zishangilie, nchi na ifurahi;
semeni katika mataifa, “Mwenyezi Mungu anatawala!”
32 Bahari na ivume, na vyote vilivyo ndani yake;
mashamba na yashangilie, na vyote vilivyomo.
33 Kisha miti ya msituni itaimba,
itaimba kwa furaha mbele za Mwenyezi Mungu,
kwa maana anakuja kuihukumu dunia.
 
34 Mshukuruni Mwenyezi Mungu kwa kuwa ni mwema;
fadhili zake zadumu milele.
35 Mlilieni, “Ee Mungu Mwokozi wetu, tuokoe.
Tukusanye tena na utukomboe kutoka kwa mataifa,
ili tuweze kulishukuru jina lako takatifu,
na kushangilia katika sifa zako.”
36 Atukuzwe Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli,
tangu milele na hata milele.
Nao watu wote wakasema, “Amen,” na “Msifuni Mwenyezi Mungu.”
 
37 Daudi akamwacha Asafu na wenzake mbele ya Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu, ili wahudumu humo mara kwa mara, kulingana na mahitaji ya kila siku. 38 Pia akamwacha Obed-Edomu pamoja na wenzake sitini na wanane wahudumu pamoja nao. Obed-Edomu mwana wa Yeduthuni na pia Hosa walikuwa mabawabu wa lango.
39 Daudi akamwacha kuhani Sadoki pamoja na makuhani wenzake mbele ya hema la ibada la Mwenyezi Mungu katika mahali pa juu pa kuabudia huko Gibeoni 40 ili kutoa sadaka za kuteketezwa kwa Mwenyezi Mungu kwenye madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa mara kwa mara, asubuhi na jioni, sawasawa na kila kitu kilichoandikwa katika Torati ya Mwenyezi Mungu ambayo alikuwa amempa Israeli. 41 Waliohudumu pamoja nao walikuwa Hemani, Yeduthuni na wale wote waliochaguliwa na kutajwa kwa jina kumpa Mwenyezi Mungu shukrani, “Kwa maana fadhili zake zadumu milele.” 42 Hemani na Yeduthuni walikuwa na wajibu wa kupiga tarumbeta, matoazi na kutumia vyombo vingine kwa ajili ya nyimbo za sifa kwa Mungu. Wana wa Yeduthuni waliwekwa langoni.
43 Kisha watu wote wakaondoka, kila mmoja akarudi nyumbani mwake, naye Daudi akarudi nyumbani kuibariki jamaa yake.